Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Osimhen atakavyotikisa Ulaya dirisha lijalo

Victor Osimhen.jpeg Victor Osimhen

Fri, 26 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

VICTOR Osimhen ni jina linalotajwa kwenye klabu nyingi kubwa za Ulaya kwa miaka ya karibuni, lakini hakuna timu iliyofanikiwa kuinasa huduma ya straika huyo wa kimataifa wa Nigeria.

Sababu za kushindwa kumnasa bado hazijafahamika, lakini hakuna ubishi maisha yake huko Naples yanaelekea ukingoni na bila ya shaka kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi atang’oka Napoli.

Mshambuliaji huyo wa kati, ambaye amefunga mabao 67 na kuasisti mara 17 katika mechi 119 alizochezea Napoli, aliisaidia timu hiyo kushinda taji la ubingwa wa Serie A msimu uliopita – ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kipindi cha miaka 33.

Mtaalamu wa masuala ya usajili Ulaya, Fabrizio Romano, alisema tetesi ni nyingi za kumhusu mshambuliaji huyo, lakini mahali ambako atakwenda pameshajulikana. Ni wapi?

Hizi hapa timu saba ambazo Osimhen anaweza kwenda kucheza soka lake kwa msimu wa 2023-24!

Barcelona

Mastraika waliopo: Robert Lewandowski, Ferran Torres, Marc Guiu

Kwa sasa Robert Lewandowski ndiye anayeongoza safu hiyo ya ushambuliaji, lakini Barcelona inahitaji kufanya maboresho makubwa katika eneo hilo. Licha ya mastaa waliopo kuwa na uwezo wa kufunga mabao, Barca bado inahitaji kuwa na wafungaji wengi zaidi na kwenye hilo, Osimhen anaweza kuwa chaguo sahihi katika kutafuta wachezaji wa kwenda kuongeza nguvu kwenye fowadi yao huko Nou Camp.

Chelsea

Mastraika waliopo: Nicolas Jackson, Armando Broja, Christopher Nkunku

Kikosi hicho cha Kocha Mauricio Pochettino, Chelsea kimekuwa kikihusishwa sana na mpango wa kumsajili Osimhen kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya baridi huko Ulaya. Hata hivyo, kuipata saini ya Osimhen kwenye dirisha hili ni ngumu, itaibidi isubiri hadi mwishoni mwa msimu. Mastraika waliopo Chelsea kwa sasa Nicolas Jackson, Armando Broja na Christopher Nkunku wanahitaji waletewe mtu.

Real Madrid

Mastraika waliopo: Vinicius Jr, Rodrygo, Joselu

Ni suala la wazi kabisa Real Madrid ipo sokoni kutafuta straika mpya baada ya kumpoteza Karim Benzema kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Imekuwa ikiwatumia washambuliaji wa Kibrazili Vinicius Jr na Rodrygo, lakini wanahitaji straika wa kiwango cha dunia aje kupiga kazi na kwenye hilo, Osimhen anapewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba. Kylian Mbappe na Erling Haaland wanawindwa pia.

Man United

Mastraika waliopo: Rasmus Hojlund, Anthony Martial, Marcus Rashford

Kocha Erik ten Hag alitumia pesa nyingi kumsajili straika kinda Rasmus Hojlund kwenye dirisha lililopita, lakini bado Manchester United haijamaliza tatizo lake kwenye eneo hilo la ushambuliaji. Washambuliaji wengine, Marcus Rashford, Anthony Martial na Alejandro Garnacho bado hawajafanya kitu cha maana, hivyo straika kama Osimhen anahitajika kuja kumaliza tatizo la mabao kwenye timu hiyo.

Tottenham

Mastraika waliopo: Son Heung-min na Richarlison

Kuondoka kwa straika Harry Kane kwenye dirisha lililopita kuliacha pengo kubwa Tottenham Hotspur, lakini iliingiza pia pesa zaidi ya Pauni 100 milioni kwenye mauzo hayo. Son Heung-min na Richarlison wanajaribu kupambana kuokoa jahazi, lakini kwa miamba hiyo ya London kuwa na ushindani mkali kwenye Ligi Kuu England, inahitaji huduma ya straika wa kiwango cha dunia kama Osimhen.

Arsenal

Mastraika waliopo: Gabriel Jesus, Eddie Nketiah

Hakuna kificho kwamba Arsenal inahitaji straika wa kiwango cha dunia kwenda kuifanya kuwa timu ya kibingwa zaidi kwenye Ligi Kuu England. Mastraika waliopo kwenye kikosi hicho kwa sasa wanashindwa kuonyesha viwango bora kabisa, hivyo Kocha Mikel Arteta naye anahitaji kuwa na mtu wake makini kama ambavyo Pep Guardiola anavyotamba na Erling Haaland, hivyo Osimhen atamfaa zaidi kwenye hilo.

PSG

Mastraika waliopo: Kylian Mbappe, Goncalo Ramos, Randal Kolo Muani

Kama Kylian Mbappe ataamua kuondoka kwenye kikosi hicho wakati wa dirisha lijalo la uhamisho, bila ya shaka Paris Saint-Germain itaingia sokoni kutafuta mtu wa kwenda kuziba pengo lake na Osimhen atakuwa chaguo sahihi.

Washambuliaji Goncalo Ramos na Randal Kolo Muani ni wazuri, lakini hawakupi uhakika mkubwa wa kufunga mabao tofauti na unapokuwa na huduma ya straika matata kabisa kama Osimhen.

Chanzo: Mwanaspoti