Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Osimhen atakavyotibua msimamo wa Ligi ya pesa England

Dili Za Pesa Osimhen atakavyotibua msimamo wa Ligi ya pesa England

Tue, 27 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Victor Osimhen atakwenda kabisa kuvuruga msimamo wa mastaa wanaolipwa pesa nyingi kwenye Ligi Kuu England endapo kama atakamilisha dili la kwenda kujiunga na Chelsea huko Stamford Bridge kabla dirisha halijafungwa Ijumaa wiki hii.

Straika huyo wa Napoli mwenye umri wa miaka 25, yupo kwenye hatua za mwisho za kujiunga na Chelsea kwa ada ya Pauni 39 milioni, wakati Romelu Lukaku akijiandaa kwenda upande wa pili huko Napoli.

Osimhen mabao yake 76 katika mechi zake 133 akiwa na miamba hiyo ya Serie A yanamfanya kuwa mshambuliaji anayesakwa na klabu nyingi kubwa za huko Ulaya. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca anaamini akinasa huduma yake atakuja kufanya safu ya ushambuliaji ya The Blues kuwa tishio zaidi na kuwa kwenye orodha ya timu zinazofukuzia ubingwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Osimhen atakapotua Stamford Bridge atakuwa kwenye presha kubwa ya kuhakikisha anafanya vizuri uwanjani kutokana na mshahara anaotaka kulipwa kwa wiki. Mnigeria huyo anataka alipwe Pauni Nusu Milioni kwa wiki.

Kiwango hicho cha mshahara kitamfanya staa huyo afunike mastaa wote kwenye Ligi Kuu England na kukamatia namba moja kwenye orodha ya wanasoka watakaokuwa wanavuna mkwanja wa maana kwa kila juma kwa huduma wanazotokea kwenye timu zao.

Na kama Osimhen atatua Chelsea, msimamo wa mastaa wanaoongoza kwa mishahara mikubwa utakuwa hivi.

10) Jack Grealish - Pauni 300,000 kwa wiki

Jack Grealish, 28, alisaini mkataba wa kulipwa Pauni 300,000 kwa wakati alipojiunga na Manchester City mwaka 2021 alitokea Aston Villa kwa dili la Pauni 100 milioni. Anashika namba tatu kwenye orodha ya wanaolipwa pesa nyingi kwenye kikosi cha Pep Guardiola, amechangia mabao 32 katika mechi 126 alichezea miamba hiyo ya Etihad.

9) Bruno Fernandes - Pauni 300,000 kwa wiki

Bruno Fernandes, 29, alisaini mkataba mpya Manchester United mapema mwezi huu utakaomfanya kuendelea kuwapo Old Trafford hadi 2027. Kuna wachezaji wawili tu wanaolipwa mishahara mikubwa kumzidi Mreno huyo, ambaye amefunga mabao 79 na kuasisti 67 katika mechi 236 alichezea mabingwa hao mara 20 wa England.

8) Marcus Rashford - Pauni 325,000 kwa wiki

Marcus Rashford analipwa Pauni 25,000 zaidi kwa wiki kuliko nahodha wake Fernandes, hivyo anakuwa mchezaji wa pili kwenye kitabu cha hesabu za Man United anayelipwa mshahara mkubwa. Staa huyo wa kimataifa wa England alifunga mara nane tu kwenye michuano yote msimu uliopita na hilo linamfanya kuwa kwenye presha kubwa ya kuhakikisha anafanya vyema msimu huu.

7) Raheem Sterling - Pauni 325,000 kwa wiki

Winga wa Chelsea, Raheem Sterling ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa huko Stamford Bridge, lakini staa huyo kwa sasa anahusishwa na mpango wa kuachana na timu hiyo baada ya kocha mpya, Enzo Maresca kumwambia hana nafasi kwenye timu yake. Juventus imeripotiwa kufukuzia saini ya mchezaji huyo, ambaye pia imeelezwa anaweza kutumika kwenye dili la Chelsea kumsajili Jadon Sancho.

6) Romelu Lukaku - Pauni 325,000 kwa wiki

Straika Romelu Lukaku, 31, anajiandaa kujiunga na Napoli baada ya miaka mitatu ya mapito makubwa huko Chelsea. Mbelgiji huyo alijiunga na Chelsea kwa ada ya Pauni 97.5 milioni na kulipwa mshahara, Pauni 325,000 kwa wiki, kama ambavyo amekuwa akilipwa Sterling kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge, lakini kwa Lukaku hajachezea timu yake kwa miaka miwili, akitolewa kwa mkopo Inter Milan na Roma.

5) Mohamed Salah - Pauni 350,000 kwa wiki

Gwiji wa Liverpool, Mo Salah yupo kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake huko Anfield, ambao unamshuhudia akiwa analipwa Pauni 350,000 kwa wiki kutokana na dili alilosaini mwaka 2022. Bado haijafahamiki kama staa huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye alijiunga na Liverpool mwaka 2017 atasaini mkataba mpya kwenye kikosi hicho au atashawishika kwenda kujiunga na klabu za Saudi Arabia.

4) Casemiro - Pauni 350,000 kwa wiki

Casemiro, 32, alimaliza msimu wa 2023/24 kwa kiwango cha hovyo sana na kukosolewa kila mpya, huku beki wa zamani wa Liverpool, anayefanya kazi ya uchambuzi wa soka kwa sasa, Jamie Carragher akimtaka aondoke kabisa kwenye soka la Ulaya muda wake umeshakwishi. Lakini, amerejea msimu huu akiwa kwenye kiwango bora na bila shaka ataendelea kubaki kwenye kikosi cha Man United na kuendelea kulipwa pesa ndefu.

3) Erling Haaland - Pauni 375,000 kwa wiki

Erling Haaland, 22, alifunga hat-trick yake ya 10 akiwa na Manchester City Jumamosi iliyopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Ipswich Town na hivyo kumfanya afikishe mabao 94 katika mechi 101 alizochezea mabingwa hao wa England. Hakika, Haaland ni kama analipa inavyostahili kwa maana ya malipo halali ya Pauni 375,000 kwa wiki anazolipwa kwa ajili ya huduma yake.

2) Kevin De Bruyne - Pauni 400,000 kwa wiki

Kevin de Bruyne huenda akalitema taji la kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England endapo kama Osimhen atatua Chelsea. Kiungo huyo mshambuliaji wa Man City, akiwa na umri wa miaka 33 kama ataondoka mwishoni mwa msimu huu basi atakuwa ametimiza miaka yake 10 ya kuitumikia kwa mafaikio makubwa miamba hiyo ya Etihad.

1) Victor Osimhen - Pauni 500,000 kwa wiki

Osimhen ameripotiwa kutaka alipwe mshahara wa Pauni 500,000 kwa wiki ili akamilishe uhamisho wake wa kujiunga na Chelsea. Na kama mabosi wa Chelsea watakubali kumpa Osimhen kiwango anachotaka, basi atakwenda kumzidi De Bruyne kwa Pauni 100,000 kwa wiki kwenye mshahara na hivyo atavuruga kabisa msimamo wa ligi hiyo ya mkwanja ilivyo na kuwa mchezaji bosi zaidi kwa mshahara mkubwa kwenye Ligi Kuu England.

Chanzo: Mwanaspoti