Kocha Mkuu wa muda wa Orlando Pirates inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), Fadlu Davids, amesema wanaamini timu yao itashinda mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Simba SC ya Tanzania.
Miamba hiyo kesho Jumapili (April 24) itakutana uso kwa macho Uwanja wa Orlando mjini Johannesburg-Afrika Kusini, kumalizia ungwe ya pili ya kuwania kutinga hatua ya Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku Simba SC ikishinda ungwe ya kwanza kwa bao 1-0, jijini Dar es salaam.
Kocha Fadlu amesema pamoja na kuwa na matumaini ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo, kitu ambacho wanatakiwa kuwa nacho makini ni mabadiliko ya eneo la kiungo.
Kocha huyo anayefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na kocha Mandla Ncikazi ambaye alichafua hali ya hewa mara baada ya mchezo wa Mkonso wa Kwanza jijini Dar es Salaam, amesema anafahamu kwamba Simba SC itamrudisha kikosini kiungo kutoka nchini Mali Sadio Kanoute ambaye uwepo wake utaongeza ubora katika eneo la kiungo la Wekundu hao.
Kocha huyo anayeheshimika kwa kazi ya kujua kuwasoma wapinzani ameongeza kuwa wamewaambia wachezaji wao kwamba lazima wawe bora katika dakika 45 za kwanza kuweza kupata mabao huku pia wakitakiwa kuwa makini na viungo washambuliaji wa pembeni wa timu hiyo pamoja na mabeki wao.
“Tunafahamu Kanoute atarudi uwanjani katika mechi hii huyu ni kiungo mzuri ambaye anacheza kisasa, nikwambie tu kuna wakati tulikaribia kumsajili wakati akitoka mashindano ya Afrika (CHAN), lakini tulibadili mawazo,” amesema Davids na kuongeza;
“Watakuwa na maboresho katika safu yao ya kiungo tunachotakiwa na tumewaambia wachezaji ni kwamba lazima tupate mabao katika dakika 45 za kwanza lakini itategemea na ubora wetu kuweza kufungua eneo lao la kiungo na lile la ulinzi.
“Kuna beki wao pia atarudi yule wa Kenya (Joash Onyango), hatupaswi kudharau watu wa kule mbele Simba kuna watu wana kasi sana hasa wale wa pembeni sambamba na wale mabeki wao wa pembeni pia.”
Katika mchezo huo Orlando Pirates itapaswa kusaka ushindi wa mabao mawili ama zaidi ili kujihakikishai nafasi ya kutinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku Simba SC ikipaswa kupambana kusaka ushindi wowote ama kulinda ushindi walioupata Dar es salaam wa bao 1-0.