Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Onyango vipi tena huko Singida FG?

Onyangoz Onyango vipi tena huko Singida FG?

Mon, 21 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya ushindi wa mabao 4-1 ilioupata Singida Big Stars dhidi ya JKU katika mchezo wa hatua ya kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika, kocha Hans Pluijm hajafurahishwa na namna ambavyo beki wake Joash Onyango alivyofanya makosa na wapinzani wao kupata bao.

Katika dakika ya 60 ya mchezo huo, Onyango alipigiwa pasi na kipa Benedict Haule na yeye alitoka ndani ya boksi na mpira lakini hakuchukua maamuzi ya mapema kuondoa hatari na badala yake alipokonywa mpira na mchezaji wa JKU ambaye alipiga shuti lilioenda kumgonga mkononi beki wa Singida, Biemes Carno na kuwa penalti iliyozaa bao.

Tukio hilo limemfanya Pluijm aseme ni makosa ya kitoto kufanyika katika mechi za mashindano makubwa na mbaya zaidi kosa hilo kufanywa na mchezaji mzoefu.

“Sawa mpira ni mchezo wa makosa lakini kwa mchezaji mwenye uzoefu kama yeye hauwezi ukafanya makosa haya katika mechi hizi za CAF, ” alisema Pluijm ambaye ni Mholanzi lakini makazi yake ya kudumu ni Ghana.

Akizungumzia mchezo kiujumla, Pluijm alisema ni bora mpira uchezwe mbali na goli lao kwani inakuwa ngumu kupatikana makosa madogo madogo.

“Kipindi cha kwanza tulicheza vizuri lakini dakika za 60 tulianza kujiamini, 4-0 ni bora kuliko 4-1 na sio kwamba naogopa mchezo wa marudiano hapa, lengo letu ni kushinda pia mechi ya pili,”alisema Pluijm.

Kocha huyo alifunguka zaidi na kusema kipindi cha pili hawakuwa na mchezo mzuri na mwisho zaidi wakawa wamejiweka upande wa presha.

Singida baada ya mchezo huo iliondoka jijini Dar es Salaam na kurejea Singida kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa saa 10:00 jioni katika uwanja wa Liti.

Wakati huo huo, Singida itarudiana na JKU katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Agosti 27 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam utakaochezwa saa 1:30 usiku.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live