Uongozi wa Simba umefikia makubaliano mazuri ya kuvunja mkataba na beki wake wa kati, Joash Onyango ambaye raia wa nchini Kenya.
Mkenya huyo hivi karibuni ilielezwa kuuandikia uongozi wa timu hiyo barua ya kuomba kuondoka baada kutokana na ufinyu wa nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Huyo ni mchezaji wa tatu hadi hivi sasa ndani ya Simba kuomba kuvunja mkataba wake mwingine ni Mghana, Augustine Okrah na Mohammed Ouattara huku Ismael Sawadogo akiwa katika hatua za mwisho za kuvunja.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Simba zimesema kuwa Onyango na uongozi huo wamefanya mazungumzo ya kuuvunja mkataba wa mwaka mmoja wa beki huyo ambayo yamekamilika kwa asilimia mia moja.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa beki huyo tayari ana ofa nzuri klabu ya Gor Mahia ya Kenya ambayo hivi karibuni iliwasilisha ofa ya kumuhitaji beki huyo kabla ya msimu kumalizika.
“Mazungumzo ya Onyango na uongozi wa Simba juu ya kuvunja mkataba wake yamekamilika, na hivi sasa yupo huru kwenda kuichezea klabu yoyote atakayohitaji kuichezea.
“Pande zote mbili kwa maana ya uongozi na mchezaji mwenyewe mazungumzo yalikwenda vizuri na kufikia muafaka mzuri wa kuuvunja mkataba huo wa mwaka mmoja,” kilisema chanzo hicho.