Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Onyango aahidi makubwa Simba

C8a1274015b7ccdc7d943a9af6793a51.jpeg Onyango aahidi makubwa Simba

Tue, 6 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MLINZI wa kati wa Simba, Joash Onyango ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa Machi wa mashabiki na kuzawadiwa Sh 1,000,000 kutoka kwa wadhamini Emirate Aluminium.

Onyango ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwashinda Luis Miquissone na mlinda mlango Aishi Manula kutokana na kura nyingi zilizopigwa na mashabiki kupitia tovuti ya klabu yao.

Raia huyo wa Kenya amekabidhiwa tuzo hiyo katika Uwanja wa Mo Simba Arena baada ya kumalizika kwa mazoezi ya jana.

Ofisa Uhusiano na Masoko wa Emirate Aluminium, Issa Maeda alisema ana amini ushirikiano huo utaendelea kwa muda mrefu kutokana na mahusiano yaliyopo.

“Leo tumemkabidhi Onyango tuzo hii na hundi ikiwa ni zawadi ya kuchaguliwa mchezaji bora wa Machi kwa mujibu wa mkataba wetu na Simba,” alisema Maeda.

Naye Onyango aliwashukuru mashabiki kwa kumpigia kura nyingi na wadhamini Emirate Aluminium kumpa tuzo hiyo ambayo inamuongezea ari ya kupambana zaidi.

“Nawashukuru mashabiki wetu kwa kunipigia kura nyingi pamoja na wadhamini Emirate Aluminium kwa kunipa tuzo hii. Nawahakikishia nitaendelea kupambana kuhakikisha naisaidia timu kufanya vizuri zaidi,” alisema Onyango.

Katika kinyang’anyiro hicho, kura zilizopigwa ni 25,719 ambapo Onyango alipata kura 20,288 sawa na asilimia 79, Manula kura 4,673 sawa na asilimia 18 na Miquissone kura 758 sawa na asillimia 2.

Chanzo: www.habarileo.co.tz