Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ongala na kismati cha mechi kubwa

Kally Ongala Big Match Kally Ongala

Wed, 26 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Kally Ongala ni kama ana ‘Kismati’ cha kukutana na timu kubwa za Ligi Kuu Bara, Simba na Yanga akibahatika kuiongoza Azam FC dhidi ya vigogo hao wa Kariakoo akiwa kaimu kocha mkuu.

Kally aliyewahi kuzichezea Azam na Yanga miaka ya nyuma kwa nyakati tofauti, msimu huu alirejea Azam akiwa kama kocha wa washambuliaji lakini mwenendo mbaya wa makocha wakuu umemfanya kujikuta akiiongoza timu kwenye mechi zote mbili dhidi ya Yanga na Simba.

Baada ya Kocha Abdihimid Moallin aliyeanza msimu na Azam kufungashiwa virago baada ya mechi mbili tu za ligi akishinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na kutoa sare ya 1-1 mbele ya Geita Gold, Kally alikabidhiwa kukaimu nafasi ya kocha mkuu na mechi iliyofuata ilikuwa dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi, Yanga.

Kally aliinoa Azam na kuingia kwenye mechi hiyo kimkakati huku vijana wake wakipiga soka safi na mchezo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 mabao ya Azam yakifungwa na mabeki Daniel Amoah na Malickou Ndoye huku yale ya Yanga yote yakifungwa na kiungo Feisal Salum ‘Feitoto’, mechi iliyopigwa Septemba 6, 2022 uwanja wa Mkapa.

Siku moja baadaye, Azam ilimtambulisha Mfaransa Denis Lavagne kama kocha mkuu akichukua nafasi ya Moallin na Kally kurejea kwenye majukumu yake.

Lavagne aliiongoza Azam katika mechi sita, nne za ligi na kushinda mbili, 1-0 dhidi ya Mbeya City, 1-0 mbele ya Singida Big Stars, na kupoteza mbili kwa kuchapwa 1-0 na Tanzania Prisons kisha kufungwa 2-1 na KMC huku akiondoshwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na Al Akhdar ya Libya kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya kuchapwa 3-0 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani matokeo yaliyomfanya kutimuliwa.

Baada ya kutimuliwa kwa Lavagne, Kally amekabidhiwa tena timu akiwa kaimu kocha mkuu, akisaidiwa na nahodha wa kikosi hicho, Aggrey Morris atakayekuwa kocha msaidizi mchezaji na tayari wameanza matizi. Mechi ya kwanza atakayoanza nayo ni ile ya Simba itakayochezwa keshokutwa Uwanja wa Mkapa badala ya Azam Complex, Chamazi kama ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kally alisema; “Mchezo ujao tunacheza na Simba nyumbani, ni mechi tunayohitaji kufanya vizuri na tumeendelea vyema na maandalizi kwa ujumla.”

Chanzo: Mwanaspoti