Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Onana kupangua kikosi Simba

Onana Goal Mkwakwani.jpeg Onana kupangua kikosi Simba

Thu, 21 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati viongozi na mashabiki wa Simba wakiendelea kujipanga kwaajili ya mchezo wa Ahly, kocha mkuu wa chama hilo, Abdelhak Benchikha ameanza kuangalia uwezekano wa kumtumia winga Willy Onana kuwamaliza Al Ahly kama alivyofanya kwa Wydad akiwafunga mabao 2-0 yaliyoipeleka Simba robo fainali.

Simba na Wydad zililingana pointi 9 kila moja lakini kwa kuwa Simba iliwafunga waarabu hao mabao mengi zaidi ya 1-0 walilofungwa wao kule Algeria, Wekundu wa Msimbazi wakatinga robo fainali.

Onana alirejea hivi karibuni kwenye kikosi cha Simba baada ya majeraha aliyoyapata Desemba mwaka jana na kumfanya akose mechi nane za Mnyama ila amerudi akiwa moto na kuanzia alipoishia jambo lililomkosha Benchikha na kueleza anawaza kutafuta namna kumtumia.

“Ni jambo jema kumuona (Onana) akijumuika na timu tena, ni mchezaji muhimu kwetu na tunatafuta namna ya kumtumia kwenye mechi zijazo,” alisema Benchikha alipoulizwa kuhusu Onana.

Onana aliumia Desemba 23 mwaka jana kwenye mechi ya ligi dhidi ya KMC iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2, na kumfanya kukosa mechi nane za Simba, sita za ligi dhidi ya Mashujaa, Tabora United, Azam FC, Geita Gold, JKT Tanzania na Tanzania Prisons sambamba na mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas (0-0), na Jwaneng Galaxy ambayo Simba ilishinda 6-0 kibabe.

Kabla ya kuumia Onana alikuwa ameanza kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba lakini aliporejea ameendelea alipoishia licha ya kwamba amekuwa akianzia benchini.

Tangu amerejea amecheza mechi tatu zote akiingia kipindi cha pili kwa muda tofauti ikiwa jumla ame-cheza dakika 97 tu lakini amehusika kwenye mabao mawili ndani ya muda huo.

Onana alirejea uwanjani kwenye mechi dhidi ya Coastal Union ugenini dakika ya 71 akichukua nafasi ya Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ na dakika ya 73 aliifungia Simba bao la pili na la ushindi mechi ikimalizika kwa mabao 2-1.

Mchezo uliofuata ulikuwa dhidi ya Singida Fountain Gate alipoingia dakika ya 77 akichukua nafasi ya Kibu Denis na mechi kumalizika kwa Mnyama kushinda 3-1 huku mechi ya mwisho dhidi ya Mashujaa akiingia dakika ya 46 kuchukua nafasi ya Freddy Michael alitoa pasi ya bao la kwanza kwa Clatous Cha-ma alilofunga dakika ya 57 kabla ya Mzambia huyo kufunga tena bao la pili dk72.

Akizungumzia kurejea kwake kikosini Onana amesema asingeweza kuingia moja kwa moja kikosini ila sasa ni zamu yake.

“Ni ngumu kutoka kuwa majeruhi na kuingia moja kwa moja kikosini. Mwalimu anakuwa anakupa mu-da kuangalia utimamu wako na baada ya hapo ndipo ataamua kukupa muda mwingi zaidi kucheza kutokana na ulichokionyesha,” alisema Onana na kuongeza;

“Nashukuru nimerudi salama sasa ni zamu ya kupambana kuhakikisha napata muda wa kutosha kuitu-mikia timu. Kipindi hiki cha kambi fupi naamini nitaimarika na kurejea kwenye ubora wangu.” alisema winga huyo Mcameroon.

KUPANGUA KIKOSI

Kati ya maeneo magumu kupanga kwenye kikosi cha Simba ni lile la safu ya ushambuliaji kuanzia kwa viungo wa juu hadi mshambuliaji wa kati na Onana huenda akapangua watu eneo hilo.

Kwa hivi karibuni kutokana na mfumo wa 4-2-3-1 Benchikha amekuwa akiwatumia zaidi Chama, Saido na Kibu wanaocheza nyuma ya mshambuliaji mmoja Freddy Michael.

Lakini katika mechi iliyopita dhidi ya Mashujaa Benchikha alibadilika na kumtoa mshambuliaji wa kati, Freddy na kuingia Onana ambaye alienda pembeni kisha Saido akacheza kama namba tisa huku Chama akiwa nyuma yake (namba 10), na Kibu akacheza winga jambo lililoipa timu hiyo ushindi.

Aidha, mara kadhaa ambazo Onana amekuwa akipata nafasi basi mmoja kati ya Chama, Saido na Kibu hukaa nje kwani ndio wapinzani wa karibu katika nafasi.

Hata hivyo, maeneo hayo kuna wachezaji wengine wanaowania nafasi kama Luis Miquissone, Ladack Chasambi, Salehe Karabaka na Edwin Balua lakini hawaonyeshi ushindani wa kutosha kwa Chama, Kibu, Saido na Onana.

Wakati huu ni nafasi ya Onana kujitafuta na kuingia kikosini kwani wapinzani wake wote wa karibu, Chama, Saido na Kibu hawapo kwenye kambi ya Simba pale Zanzibar kutokana na kuwa kwenye vikosi vya timu zao za taifa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: