Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Onana katika rekodi ya Samatta iliyoanzia Cameroon

Andre Onana Sad Andre Onana

Tue, 9 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Michuano ya 34 ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2023, inatarajiwa kuanza kutimua Januari 13 na kudumu hadi Februari 11, 2024 huko Ivory Coast.

Kama ilivyo desturi kwa kila wakati michuano hii inapofanyika Januari, mizozo kati ya timu za Ulaya na mataifa ya Afrika huibuka na kugonga vichwa vya habari.

Migogoro hii husababishwa na mgongano wa maslahi baina ya pande hizo mbili kwa kugombania wachezaji.

Mataifa ya Afrika huwahitaji wachezaji wao wanaocheza Ulaya waje kuwakilisha mataifa yao huku timu za Ulaya zikitaka kuwabakisha huko waendelee kucheza ligi.

Safari hii kama ilivyo kawaida hali hiyo imeibuka tena kiasi cha kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp kuombea Mo Salah wa Misri timu yake itolewe mapema.

Lakini katika hao wote wa mwaka huu, mkasa wa kipa wa Cameroon na Manchester United, Andre Onana, ni wa kipekee.

Nyota huyo wa zamani wa Inter Milan ya Italia na Ajax ya Uholanzi, alisababisha kikao kizito kati ya klabu yake ya Manchester United na taifa lake la Cameroon, zote zilitaka huduma yake katika siku zinazofuatana.

Januari 14 timu yake ya Manchester United itakuwa na mchezo mgumu wa Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham Hotspur na Onana anatakiwa acheze, halafu Januari 15 taifa lake linacheza AFCON dhidi ya Guinea.

Onana amechagua kucheza mechi zote mbili katika simu hizo zinazofuata.

Huu ni sawa mkasa wa Mbwana Samatta na timu za taifa za Tanzania.

Mwaka 2011, akiwa na miaka 17, Samatta alikuwa mchezaji tegemeo wa timu mbili za taifa za Tanzania; Taifa Stars (timu kubwa ya taifa ) na Manyara Stars (vijana chini ya miaka 23).

Mechi hizo zilifanyika siku zinazofuatana na Samatta alichagua kucheza zote.

Mechi ya kwanza ilikuwa Dar es Salaam kwenye uwanja ambao sasa unaitwa Benjamin Mkapa.

Ilikuwa Machi 26, 2011 katika mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2012, Taifa Stars wakiwa wenyeji wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Siku iliyofuata, yaani Machi 27, 2011, timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 (wakati huo ikiitwa Manyara Stars) ilikuwa ugenini huko Cameroon kwa Onana kuwania kufuzu olimpiki ya 2012 London.

Makocha wa timu zote mbili; Jean Poulsen wa Taifa Stars na Jamhuri Kiwelo wa Manyara Stars walimhitaji Samatta kwenye timu zao.

Baada ya vuta nikuvute ikaamriwa kwamba Samatta acheze mechi zote mbili.

Hivyo basi, aliichezea Taifa Stars dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati pale kwa Mkapa, kisha akatoka uwanjani moja kwa moja kuelekea kiwanja cha ndege kuwahi usafiri aende Cameroon kwa jaili ya mchezo wa Manyara Stars.

Kwa Mkapa akafunga bao dakika ya 90 na kuipa Stars ushindi wa 2-1 baada ya kuwa Shaaban Nditi alifunga bao la kwanza ambalo lilikuwa la kusawasisha, dakika ya 70.

Na katika mchezo wa Manyara Stars, japo hakufunga na vijana wetu walipoteza 2-1, lakini alitoa mchango mkubwa uliosaidia kuifanya mechi ya marudiano kutokuwa ya mlima mrefu.

Manyara Stars wakashinda 2-1 Dar Es Salaam na kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3 hivyo mchezo kuingia hatua ya penalti.

Manyara Stars wakashinda kwa penati 4-3 na kusonga hatua iliyofuata.

Wakati Samatta aliweka rekodi nchini Cameroon, miaka zaidi ya 10 baadaye anatokea raia wa Cameroon anataka kuirudia.

Hata hivyo, kwa Samatta ilikuwa kizalendo zaidi kwa sababu zote zilikuwa timu za taifa.

MARK HUGHES NI KIBOKO YAO

Nyota wa zamani wa Wales na klabu ya Bayern Munich, Mark Hughes ndiyo kiboko ya wote.

Mwaka 1987 alicheza mechi mbili, moja ya klabu yake ya Bayern Munich na nyingine ya timu yake ya taifa ya Wales ndani ya siku moja.

Ilikuwa Novemba 11, 1987 ambapo Hughes aliandika rekodi ya aina yake kwa kucheza mechi mbili katika nchi mbili tofauti.

Akiwa na Wales, Hughes alicheza ugenini dhidi ya Czechoslovakia, kufuzu Euro 1988.

Baada ya mechi, akatoka moja kwa moja kuelekea Ujerumani kucheza mechi ya Kombe la Ujerumani, sawa na Kombe la Shirikisho la Azam Sports hapa kwetu, dhidi ya Borussia Monchengladbach.

Mechi hizo zilipishana saa chache, na zote alicheza huku ya pili akiingia kutokea benchini.

JOMO SONO HANA MFANOWE

Nyota wa zamani wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Jomo Sono, yeye aliweka rekodi ya aina yake kwa kucheza ‘mechi mbili’ za michezo tofauti ndani ya siku moja.

Ilikuwa Februari 10, 1979, katika siku muhimu katika maisha yake.

Sono alikuwa akifunga ndoa na mkewe, Gail, kwenye kanisa la Evangelical Presbyterian Church la Orlando Soweto huko Afrika Kusini.

Siku hiyo timu yake ya Orlando Pirates ilikuwa uwanjani kucheza na Higland Park.

Akiwa kanisani baba mkwe wake akaja na habari iliyowashtua wageni waalikwa alipotangaza kwamba Orlando Pirates ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 hadi mapumziko na Jomo Sono anatakiwa aende akaokoe jahazi.

Baba mkwe mwenyewe akampakiza kwenye gari lake na kumuwahisha uwanjani, dimba la Rand Stadium.

Jomo Sono akafika uwanjani kabla kipindi cha pili hakijaanza, akavua suti ya ndoa na kuvaa jezi, akaingia uwanjani.

Akatengeneza mabao matatu na yeye kufunga moja, dakika 90 Orlando Pirates 4-2 Highland Park.

Sono akavua jezi na kurudi harusini.

Chanzo: Mwanaspoti