Mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon ni mmoja kati ya makipa wa Manchester United kwa matumaini na matarajio makubwa baada ya David de Gea kuondoka Juni maka huu.
Onana alitakiwa kuwa suluhisho la muda mrefu lakini tangu alipotua kwa Pauni 47 milioni kutok Inter Milan amegeuka kuwa mmoja wa matatizo makubwa.
Kipa huyo amefungwa mabao 19 katika mechi 10 za kwanza alizocheza akiwa na uzi wa Mashetani Wekundu huku mashabiki wakiwa na hofu kuhusu kiwango chake.
Onana aliiongoza timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 3-0 mara mbili mfululizo katika Uwanja wa Old Trafford. Wikiendi iliopita alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuruhusu mabao matatu katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City. Pia, akachezea tena mabao 3-0 dhidi ya Newcastle katika Kombe la Carabao. Hiyo ni rekodi mbovu ya kufungwa zaidi ya mabao mawili Old Trafford kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1962. Sasa Mcameroon ametajwa kuingia katika orodha ya makipa wa hovyo waliowahi kupita Man United kwa mujibu wa Goal.Com.
7. BEN FOSTER
Foster alikuwa usajili wa muda mrefu wa Sir Alex Ferguson ambao haukufaulu. Hakuna mashaka hata kidogo ukilinganisha na makipa wengine kwenye orodha hii, lakini alipata nafasi ya kuwa kipa wa kwanza wa kimataifa wa England kuanza katika kikosi cha kwanza cha Man United. Foster alikuwa mbadala wa kipa, Edwin van der Sar kwa misimu miwili na alifanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la Ligi baada ya ushindi wa penalti dhidi ya Tottenham mwaka 2009.
6. MARK BOSNICH
Kipa huyo alikuwa mchezaji pekee ambaye Ferguson alimsajili mara mbili. Alicheza mechi mbili za Ligi Kuu England kabla ya kurejea baada visa yake kumalizika. Baada ya kuonyesha kiwango bora alipokipiga Aston Villa, Bosnich alirejea tena mwaka 1999 baada ya Peter Schmeichel kuondoka. Licha ya kuchukua nafasi ya kipa huyo mkongwe hakuweza kuvaa viatu vyake badala yake aliboronga. Aliichezea Man United kuanzia msimu wa 1989 hadi 1991 kabla ya kujiunga na Sydney United na kurejea tena mwaka 1999.
5. TIM HOWARD
Kipa huyo wa zamani wa Marekani hakujulikana sana England aliposajiliwa na Man United mwaka 2003, pia hakukabiliana na presha yoyote wakati anajiunga na timu hiyo, lakini mwanzo mzuri wa Howard ulianza kuibuka katika mechi ya hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Porto iliyonolewa na Jose Mourinho. Hata hivyo, Howard alishindwa kuiokoa Man United na kutolewa nje huku Mourinho akishangilia.
4. ROY CARROLL
Kipa huyo wa zamani wa Ireland Kaskazini alianza maisha akiwa Man United kama mwanafunzi wa chini wa Fabien Barthez kipa namba moja wa kikosi hicho. Kipa huyo hakuwa na maajabu kwani alishindwa kuokoa penalti katika ushindi wa mikwaju ya penalti dhidi ya Arsenal kwenye fainali ya Kombe la FA mwaka 2005. Kipa huyo alikuwa na makosa mengi na kuigharimu timu yake na kupigwa chini mwaka 2005.
3. FABIEN BARTHEZ
Bingwa wa Kombe la Dunia na EURO akiwa na uzi wa Timu ya Taifa ya Ufaransa. Iliaminika kwamba angekuwa mrithi sahihi wa Peter Schmeichel lakini alishindwa kutoboa kwani alijiamini sana kuanzia msimu wa 2000 hadi 2004. Miaka mitatu aliyokipiga Man United ilikuwa ya kukumbukwa zaidi alipoonyesha kiwango kibovu katika mechi ya Man United ambayo ilipokea kichapo cha mabao 3-1, pia alifanya makosa katika kichapo walichopata dhidi ya Deportivo La Coruna kwenye mechi ya Ligi Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, kipa huyo aliisaidia Man United kubeba ubingwa katika msimu wa tatu, lakini alikuwa dhaifu kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid kwani aliruhusu mabao matatu mechi zote mbili baada ya hapo hakucheza tena.
2. VICTOR VALDES
kipa huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Hispania aliwahi kuichezea Barcelona na kuisumbua Man United kwenye fainali mbili za Ligi Mabingwa Ulaya na baada ya miaka mitatu alijikuta anakipiga Old Trafford. Valdes hakuwa chaguo namba moja na alikubali kusajiliwa na Monaco baada ya kugoma kuongeza mkataba Barcelona. Baada ya kupata majeraha Man United ilikubali kumsaidia matibabu yake kabla ya kusajiliwa chini ya Kocha Louis van Gaal mwaka 2015. Hata hivyo alipitia wakati mgumu chini ya kocha huyo kwani alicheza mechi mbili tu.
1. MASSIMO TAIBI
Man United ilimsajili Mtaliano huyo mwaka 1999 kama msaidizi wa wa Mark Bosnich alipojeruhiwa, na kulipa Pauni 4.5 milioni kwa Venezia. Kipa huyo aliweka rekodi mbovu ya kuruhusu mabao 11 katika mechi nne za kwanza. Mechi yake ya kwanza dhidi ya Liverpool aliruhusu bao la kizembe na kumpa fursa Sami Hyppia kufunga bao. Mechi ambayo mashabiki wa United hawakuisahau kipindi hicho ilikuwa dhidi Chelsea kwani aliruhusu mabao na hiyo ikawa mechi yake ya mwisho.