Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Onana, Kocha wana jambo lao

Onana Goal Vs Wydad.jpeg Onana, Kocha wana jambo lao

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kipyenga kimelia Msimbazi na mastaa wote wa Simba ambao hawako kwenye Afcon wanatakiwa kufika kesho Jumatano wawe tayari kambini kwaajili ya kuanza mazoezi ya kujiandaa na mechi zijazo huku wenyewe wakitamba kwa kusema “Raundi hii tutaelewana.”

Hiyo ni baada ya kumalizika kwa siku 10 za mapumziko mafupi ambayo benchi la ufundi chini ya kocha Mualgeria Abdelhak Benchikha lilitoa kwa mastaa hao ili kupoza miili kutokana na mashindano ya Afrika kusimama kupisha fainali za Afcon.

Hata hivyo, Simba haikutaka wachezaji wake wakae kizembe kwenye mapumziko hayo ndipo ikampa kila mmoja programu maalumu ya mazoezi atakayokuwa anafanya akiwa nyumbani kwake na pale atakaporejea kambini atakaguliwa kuwa aliitimiza kiufasaha.

Staa wa Simba, Willy Onana anayemalizia mapumziko nchini kwao Cameroon alisema mapumziko waliyoyapata yamewasaidia kwenye kujitafakari na kujua nini wanatakiwa kufanya watakaporejea uwanjani.

“Tumetumia muda huu kujitafakari wapi tulikosea na wapi tunatakiwa kuongeza nguvu pia kuweka mipango mipya, muda si mrefu tutarudi uwanjani, najua tutakuwa na ari mpya ya kupambana zaidi lengo ikiwa ni kuipa timu mafanikio,” alisema Onana ambaye gari limewaka tangu kocha Benchikha amechukua timu.

Kocha wa makipa wa Simba, Dani Cadena anayemalizia mapumziko nchini kwao Hispania aliliambia Mwanaspoti kuwa, “Raundi hii tutaelewana. Kuna wachezaji wameongezwa na waliokuwepo wamepata muda wa kupumzika nadhani tukirejea kwa pamoja tutakuwa na nguvu kubwa na mashabiki wataifurahia timu yao,” alisema Cadena mwenye leseni ya ukocha ya UEFA pro.

Simba ina wachezaji 13 wa kigeni ambapo ukiwatoa Henock Inonga (DR Congo), na Clatous Chama (Zambia), walio katika fainali za Afcon, wengine wote walirejea makwao na sasa ni muda wa kurudi nchini tayari kuitumikia klabu hiyo.

Ayoub Lakred (Morocco), Che Malone Fondoh na Onana (Cameroon), Fabrice Ngoma (DR Congo), Sadio Kanoute (Mali), Saidi Ntibanzokiza (Burundi) na Aubin Kramo (Ivory Coast), wengi wao walienda kwao mapumziko na kuanzia jana wameanza kurejea nchini sambamba na wale mastaa wapya watatu wa kigeni, Babacar Sarr anayetokea Senegal, Freddy Michael Kouablan kutoka Ivory Coast na Mgambia Pa Omar Jobe wote kufika kesho jioni watakuwa kwenye kambi za Simba tayari kwa kuanza mazoezi Alhamis.

Sio hao tu, pia maofisa wa benchi la ufundi wakiongozwa na Benchikha na msaidizi wake Farid Zemiti pamoja na kocha wa viungo Kamal Boujdjenane waliokuwa kwao Algeria, Cadena kutoka Hispania, Mtathimini michezo kwa njia ya Video ‘Video Analyst’ Mzimbabwe Kelvin Mavunga, na wengine wote waliokuwa makwao na sasa wanarejea.

ALICHOSEMA BENCHIKA

Kabla ya kutoa mapumziko hayo, kocha Benchikha aliwasisitiza wachezaji kila mmoja kufanya tafakuri binafsi na kutumia muda huo kupumzika na kufanya mazoezi kiasi huku akijipanga kwa mapinduzi yatakayofanyikia pindi watakaporejea.

“Wakati tunaahirisha kambi kocha alisisitiza tukapumzike huku tukijitafakari, aliongea hilo kwa lugha ya ukali na kusisitiza kuna mapinduzi na mabadiliko makubwa atayafanya tutakaporejea hivyo tujiandae kukabiliana nayo.

Inaonekana hakuridhishwa na tulichokifanya kwenye kombe la Mapinduzi, anataka kazi zaidi ndiyo maana akatupa mapumziko ili tukirudi tusiwe na la kusingizia kwani itakuwa kila mmoja amepata anachokitaka,” alisema mchezaji mmoja wa Simba aliyeomba kutotajwa gazetini.

Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Kikosi kimepata muda wa kupumzika na sasa tupo tayari kurejea uwanjani kuipambani timu yetu ili ifikie malengo.”

Simba baada ya mapumziko hayo, itatupa karata yake ya kwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, Februari 17, mwaka huu dhidi ya Dodoma Jiji, kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo.

Chanzo: Mwanaspoti