Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Olimpiki ilikuwa ya wanaume, Helene akaibadili

Hellennn Olimpiki ilikuwa ya wanaume, Helene akaibadili

Thu, 1 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 128 ya michezo ya Olimpiki ambayo hivi sasa inafanyika Paris, Ufaransa, pamekuwepo usawa wa kijinsi uliokuwa ukipigiwa kelele kwa miaka mingi, hasa na wanawake.

Katika michezo hii wapo washiriki 5,630 wanaume na wanawake ni 5,416. Haikuwa kazi rahisi kwa kiwango hiki kufikiwa kutokana na michezo ilianza kwa kuwa ni ya wanaume tu na kila wanawake walipotaka kushiriki waliambiwa kaeni pembeni na kuwa watazamaji na washangiliaji.

Wapo wahafidhina waliokuja na kauli za kejeli za kuwaambia wanawake wapeni waume zenu mazoezi magumu nyumbani ili waibuke washindi.

Mafanikio ya wanawake kuweza kushiriki michezo hii yametokana na ujasiri mkubwa na kujiamini kwa mwanamke mmoja wa Uswisi kuuvunja mwiko mwaka 1900 wa kushiriki na mwanaume katika mbio za mashua. Mwanamama huyu ni Helene de Porurtales.

Tukio hili lilionekana kama la ajabu na habari zake zilitawala vyombo vya habari kuliko tukio jengine lile la michezo ya Olimpiki ya 1900 ambayo pia ilifanyika Paris ambako sasa tunaona usawa wa uwakilishi miongoni mwa wana michezo wanaume na wanawake na viongozi waliojumuka hapo.

Kinachofurahisha pia ni kwamba hata idadi ya watangazaji na wachambuzi wanawake wa michezo hii pia imeongezeka. Katika michezo inayoendelea Paris wapo watangazaji wanawake 35 kati ya 92 waliochaguliwa rasmi na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).

Hii ni asilimia 40 na ambayo ni karibu mara mbili ya idadi ya wanawake waliofanya hivyo katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020 iliyofanyika Tokyo, Japan.

Katika michezo hiyo mwanamama huyu wa Uswisi aliacha alama nyingi, kwanza ni kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushiriki michezo hii, lakini yeye na mwenzake waliibuka kuwa washindi na kuchukua medali ya dhahabu.

Namna ambavyo huyu mwanamama ambaye ni mzuri wa umbo na sura alikuwa na misuli kama ya mwanaume na alipiga makasia kwa mwendo wa haraka kuliko karibu wanaume wote walioshiriki mashindano yale, pamoja na aliyekuwa na aliyekuwa mshirika wake katika mashindano yale.

Kushiriki kwa mwanamama huyu na zaidi kwa mashua yao kufika ulingoni mwanzo kuliko nyingine uliwafungua macho viongozi wa IOC na wengine waliokuwa wamewajengea ngome wanawake ya kuwazuia kushiriki katika michezo ya Olimpiki ambayo siku zote ilikuwa ya wanaume na wanawake kuwa watazamaji.

Baada ya ushindi wa huyu mama wa Uswisi ndio vuguvugu la wanawake kuhimiza waruhusiwe kuwa washiriki wa michezo ya Olimpiki lilipopamba moto.

Wanawake hao wakaja na wazo wa kuanzisha michezo ya Olimpiki ya Wanawake kwa kueleza kwa kuwa iliyokuwepo ni ya wanaume tu basi ni vizuri na wanawake kuwa na michezo yao ya Olimpiki.

Kilichowauma vingozi wa IOC na wengine waliowakataa wanawake katika michezo ya Olimpiki ni pale kinamama waliposema michezo yao haitakuwa na ubaguzi na itawafungulia mlango wanaume kushiriki.

Hapo ndipo IOC ikaona safari yake ya kuwabana kinamama imegonga mwamba na katika michezo iliyofuata ya 1904 ikawaruhusu wanawawake kushiriki katika mchezo wa upigaji mishale.

Baada ya hapo kila ilipofanyika michezo ya Olimpiki milango ikazidi kufunguliwa kwa wanawake na idadi yao kuongezeka polepole hadi hii leo tunaona upo usawa wa kijinsi katika michezo inayoendelea Ufaransa.

Mwanamama huyu wa Uswisi aliyewafungulia mlango wanawake kushiriki katika michezo ya Olimpiki akiwa na miaka 22 alizaliwa New York, Marekani, Aprili 28, 1868 na kuiaga dunia akiwa Geneva, Uswisi Novemba 2, 1945.

Habari za maisha yake na zaidi katika mchezo wa kupiga makasia ndani ya mashua zimekuwa sehemu muhimu ya historia ya miaka 128 ya michezo ya Olimpiki na harakati za mwanzo za wanawake kupigania haki walizokuwa wakinyimwa katika jamii miaka ya nyuma.

Ujasiri wa mwanamama huyu wa Uswisi umechangia pakubwa harakati za wanawake katika nchi nyingi kupigania haki za wanawake za ajira, kupiga kura, kumiliki ardhi, katika michezo na mambo mbalimbali.

Hivi sasa IOC inamuhesabu mwanamama huyu wa Uswisi kama mmoja wa mashujaa wa michezo ya Olimpiki na wajukuu zake hualikwa kila inapofanyika michezo hii katika nchi mbalimbali na hata kupewa heshima ya kuvishwa medali washindi wa michezo mbalimbali.

Aliyoyafanya katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 1900 iliyofanyika Ufaransa ni mfano mzuri wa kuigwa na wanawake na wanaume wanaofanya harakati za kudai haki kutokata tamaa kupata yale ambayo wengine waliyapignia na kutofanikiwa.

Chanzo: Mwanaspoti