Yanga inachimba biti, Simba ndio kabisaaa hadi jana wamekula biriani la dabi Mbagala, Dar es Salaam. Kila mmoja akimwambia mwenzake ole wenu kesho.
Kuna wachezaji wanane wanawapa viburi mashabiki. Simba wanasema yule Baleke lazima atupie, huyo Chama atakichafua sana, Che Malone pale nyuma hatakatiza mtu na Ngoma atapiga pasi za hatari. Yanga sasa. Wanakwambia Aziz KI ana mbili, Pacome atawavuruga, Max atazunguka uwanja mzima na Yao Yao atamimina majalo ya kutosha.
Tukirudi kitaalamu sasa mifumo ya makocha wa Simba, Oliveira Roberto ‘Robertinho’ na wa Yanga, Miguel Gamondi ni kama inaendana, mara kadha kwenye mechi zao za Ligi Kuu Bara, wameonekana wakitumia 4-2-3-1, jambo linaloweza likaibua bato kali kwenye dabi yao, itakayopigwa kesho Jumapili.
Kama mfumo huo utatumika ina maana kuwa makocha wote watakuwa makini sana kuhakikisha timu zao zinapanda juu na kushambulia kwa kasi, huku wakiwa na watu wengi pia kwenye eneo lao la ulinzi.
Mara nyingi kwenye ligi imekuwa rahisi kumtabiri Robertinho lakini ni vigumu kwa Gamondi ambaye wakati mwingine amekuwa akibadilika na kucheza 3-5-2, yaani mabeki watatu, viungo watano na washambuliaji wawili kama alivyofanya kwenye mchezo dhidi ya Singida na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kama Gamond atakwenda na mabeki wanne ina maana timu yake itakuwa kwenye shepu ambayo imezoeleka msimu huu, Djigui Diarra atakaa langoni, mabeki wanaweza wakawa Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca au Dickson Job, mabeki wa pembeni wanaweza wakawa Joyce Lomalisa, Kouassi Yao kati anaweza akawa Khalid Aucho kama kiungo mkabaji ambaye atasaidiana na Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua, juu ni Aziz Ki na Maxi Nzengeli kwenye eneo la ushambuliaji atakuwa na Clement Mzize.
Kwa upande wa Simba mwenyeji wa mchezo huo, Kocha Robertinho akianza kwa mfumo huo (4-2-3-1), kipa anaweza akaanza Salim Ally, mabeki wa pembeni ni Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, wa kati Che Malone, Henock Inonga, viungo wakabaji Sadio kanoute, Fabrice Ngoma, ambapo mawinga Said Ntibanzokiza ‘Saido’, Kibu Denis na mbele yao ni Jean Baleke.
BATO ITAKAVYOKUWA
Diarra, Mwamnyeto na Bacca dhidi ya Baleke na Moses Phiri
Diarra ndiye aliyedaka dakika 540 sawa na mechi sita, ana Clean sheet nne alizopata dhidi ya JKT Tanzania, Namungo, Geita na Singida Big Stars, alifungwa na Ihefu mabao 2-1 aliruhusu mabao mawili dhidi ya Azam FC, licha ya timu yake kushinda mchezo huo, katika dabi hiyo atakabiliana na straika wa Simba mwenye uchu wa mabao Baleke ambaye hadi sasa ana mabao sita kwenye Ligi Kuu.
Kama si Baleke, kocha wa Simba akimpanga Phiri ambaye ana mabao matatu, pia atawapa kazi mabeki wa Yanga Mwamnyeto, Job au Ibrahim Bacca kukumbana na mashuti ya mshambuliaji huyo, licha ya kupewa dakika chache za kucheza lakini anafunga.
Mudathir na Aucho dhidi ya Kanoute na Ngoma
Kuna wakati kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya anacheza kama kiungo anayekaba na kushambulia, anamiliki mabao mawili akifunga dhidi ya Namungo na KMC,akikaba atasaidiana na Khalid Aucho ambapo watatengeneza bato kali kwa mastaa wa Simba, ambao Kanoute ambaye amerudi kwenye ubora kipindi cha hivi karibuni na Fabrice Ngoma ambaye ameonyesha makali sana kwenye michezo mikubwa aliyocheza anayemiliki bao moja alilofunga dhidi ya Mtibwa Sugar, nafasi zao zinaweza zikafanya mchezo wao utumie nguvu na hakika hapa ndiyo kwenye mechi yenyewe kesho kwani atakayelegalega hapa ataiua timu yake.
Lomalisa naYao dhidi ya Kibu na Saido
Mabeki wa pembeni wa Yanga, Joyce Lomalisa ana uwezo wa kupanda na kupiga mashuti, wakati Kouassi Yao ni fundi wa kukaba, lakini atakutana na mawinga wenye maarifa makubwa kama Ntibanzokiza ‘Saido’ ambaye hadi sasa ana mabao mawili akifunga dhidi ya Tanzania Prisons na alitoa asisiti na bao lingine dhidi ya Singida Big Stars, wakati Kibu Denis ni mchezaji mzuri nyakati zote timu ikiwa haina mpira na ikimiliki mpira, ana kasi na nguvu na alifunga dhidi ya SBS, hilo ndilo linamfanya kocha kumpa nafasi kubwa kikosini.
Aziz Ki na Maxi dhidi ya Inonga na Che Malone
Hadi sasa Aziz Ki ndiye mwenye mabao sita kwenye ligi ndani ya kikosi cha Yanga, akifunga dhidi ya KMC (bao moja), JKT (bao moja), Geita (bao moja) na hat -trick dhidi ya Azam FC, huku Maxi Nzengeli akiwa na mabao matano aliyofunga dhidi ya JKT Tanzania (mabao mawili), Geita (bao moja) na SBS (mabao mawili), lakini watakutana na wazee wa kazi ambao hawapendi kupitwa na wamekuwa mebeki panga pangua wa Simba ambao ni Henock Inonga na Che Malone, nafikiri hapa ni sehemu nyingine ambayo itakuwa na bato la aina yake.
Kwenye mchezo huo, Tshabalala na Kapombe wanaweza wakakabana na Maxi, Aziz Ki na Mzize, kutokana na aina ya uchezaji wao wa kunyumbulika ndani ya uwanja, hivyo watakutana nao kwa nyakati tofauti.
Lakini kwa Salim atakutana na washambuliaji wa Yanga ambao hawakumfunga ndani ya dakika 90 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, ingawa Mzize ndiye aliyemfunga kwenye mikwaju ya penalti.
Mafundi wa mpira watoa neno
Beki wa zamani wa Simba na Stars, Boniface Pawasa alisema hashangazwi kuona Robertinho akimpa nafasi kubwa Kibu, kwani ana manufaa kusaidia kunyang’anya mipira kutoka kwa wapinzani, huku akiiona dabi hiyo itahitaji maarifa ili timu kupata matokeo. “Ukiangalia ubora wa mchezaji mmoja mmoja timu zote zina wachezaji hao, ninachokiona timu itakayoshinda itahitaji iwe vizuri kimbinu na wachezaji kujiongeza kwenye maarifa ya kuchanganyua mabadiliko ya mchezo husika wawapo uwanjani,” alisema.
Aliyekuwa straika wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliizungumzia dabi hiyo: “Naiona Yanga itakuwa na nafasi ya kushinda mchezo huo, kwani timu yao ipo kwenye kiwango, sina maana kwamba Simba ina wachezaji wabaya ila unaona ubora wa mchezaji mmoja mmoja na maeneo ninayoona yatakuwa na bato kali ni viungo.”
Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba, Nassor Masoud ‘Chollo’, alisema dabi hiyo inahitaji utulivu bila kujali timu gani, inaonekana ipo vizuri kwa wakati huo. “Nimecheza dabi nyingi sana, kwani nilikuwa nahodha wa Simba najua na naelewa ugumu wake, ndio maana nasisitiza umakini ni kitu kikubwa kwenye mchezo huo, lakini pia kila kikosi kina wachezaji wazuri wanaoweza kuamua mchezo huo kama hawataingia kwa presha ya kuangalia upepo wa