Meneja wa Manchester United, Ole Gunner Solskjaer amepewa mechi tatu kuhakikisha anafanya vyema kama anataka kuendelea kukinoa kikosi hicho cha Mashetani wekundu.
Viongozi kutoka katika klabu ya Manchester United, wanataka kumpa muda kuonesha thamani yake na asisite kufanya mabadiliko ya haraka yenye manufaa ili yasijirudie yaliyotokea mwishoni mwa wiki dhidi ya Liverpool, walipopoteza kwa magoli 5-0.
Sio jambo rahisi pia, kwa sababu ratiba yao katika hiyo michezo mitatu ni watasafiri kuwafuata Tottenham, kisha Atalanta katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa, kisha watarudi nyumbani kupambana na wapinzani wao wa jadi Manchester City.
United hawajashinda mechi ya Ligi tangu kati kati ya mwezi Septemba na kelele za mashabiki zinasikika kila upande wakihitaji mabadiliko ili kuweza kupambania ubingwa.
Bodi ya wajumbe ilikutana siku ya Jumatatu, kujadili hatma ya klabu na wengi walikubaliana kumuacha Ole kuendelea na majukumu yake ila hawakuacha kuweka wazi kuwa matokeo ya timu hayakua ya kuridhisha na hawatashindwa kumbadilisha mwalimu pale itakapohitajika.
Taarifa zinasema kuwa United wanaficha maamuzi yao juu ya hatma ya Solskjaer kwa kuwa hawana uhakika kama kuna mtu kutoka ndani ya klabu anayeweza kuchukua majukumu kwa kipindi cha mpito wakati wanamtafuta Mwalimu rasmi.
Itakua jambo jema pia kama Manchester United watasubiri mpaka mapumziko ya timu za taifa ambayo yatafuata baada ya mpambano wa watani hao wa jadi dhidi ya Man City, ambapo watakua na takribani siku 14 za kumtafuta Mwalimu kabla ya mchezo wao dhidi ya Watford.