Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Old Trafford yenye Fei Toto na Bacca pekee sio poa

Bacca X Fei Beki wa Yanga, Ibrahim Bacca na Fei Toto

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Na kama kuna Rais anayejiamini katika anachokifanya basi yupo Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi ambaye kwa wengine ni kaka yetu kwa makamo. Ameipania Zanzibar. Anajenga kila anachoona kinafaa kujengwa kwa manufaa ya watu wake na vizazi vijavyo vya Wazanzibar.

Anajua mitaani anaitwa ‘Rais wa Ujenzi’. Watani zake wengine wanamuita ‘Rais wa Mabati’. Naona anataka kuifumua Zanzibar aitengeneze kwa namna anayotaka yeye na sio ile iliyozoeleka ambayo mwenyewe aliikuta. Nakukumbusha tu kwamba Rais Mwinyi ndiye Rais wa kwanza Zanzibar kuzaliwa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Jumatano jioni wakati anazindua Uwanja wa Amaan uliokarabatiwa pale Zanzibar alinifurahisha. Aliongea kwa kujiamini kwamba ifikapo mwaka 2027 wakati Tanzania itakapokuwa inaandaa michuano ya Afcon anataka moja kati ya viwanja vitakavyoandaa michuano hiyo pale Zanzibar kiwe kipya na kiwe kama Old Trafford. Nani ambishie Rais?

Nilikumbuka mbali kidogo. Rais Mwinyi anapambana, lakini kuna mahala anapaswa kupambana zaidi. Wachezaji wenyewe wa kucheza Old Trafford yake wako wapi? Old Trafford ya Zanzibar unaweza kuwa uwanja wa wageni. Ni kama ambavyo michuano ya Kombe la Mapinduzi imegeuka kuwa michuano ya wageni. Wazanzibar mara nyingi wanacheza hatua ya makundi kisha wanatolewa.

Baadaye wanabaki kushangilia Simba na Yanga. Tatizo liko wapi? Zanzibar ya vipaji ambayo tunaifahamu imekwenda wapi? Haipo tena. Duniani visiwa vina idadi ndogo ya watu na vimeshindwa kufanya vema katika soka. Lakini Zanzibar kama ingekuwa katika mwelekeo ule ule wa miaka ya 1970, kisha miaka ya 1980, halafu mwanzoni mwa miaka ya 1990 basi ingekuwa miongoni mwa visiwa vichache vinavyotamba katika soka.

Zanzibar ilikuwa na mastaa hasa wa soka. Licha ya idadi kubwa ya klabu za soka za Bara zikiongozwa na Simba na Yanga, lakini Zanzibar ingeweza kuleta idadi kubwa ya wachezaji katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars na wachezaji hao walikuwa wanaanza katika kikosi cha kwanza.

Wakati huo tulikuwa tunaimba majina makubwa ya wachezaji wa Tanzania Bara kina Hussein Marsha, Hamis Gaga, Method Mogella na wengineo lakini Zanzibar ilikuwa inatuletea wachezaji waliokuwa wanaingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza. Kina Juma Bakari ‘Kidishi’, Innocent Haule, Ally Sharrif ‘Adolph’, Ally Bushir, Amour Aziz, Eddy Abdalah na wengineo lukuki.

Walikuwa wanaitwa kwa ajili ya kucheza. Leo wachezaji wa Zanzibar wanaoitwa katika kikosi cha Taifa Stars wakitokea timu za Zanzibar wanaitwa kwa ajili ya kutengeneza taswira ya Muungano. Wenye ubavu wa kucheza kikosi cha Taifa Stars ni wale ambao wanachezea timu za bara. Nao ni Fei Toto na Ibrahim Bacca tu. Kuna mchezaji wa Zanzibar anayeweza kuanza katika kikosi cha Taifa Stars akitokea timu za Zanzibar?

Majuzi nilikuwa Zanzibar nikipiga stori na washkaji wa Zanzibar wote wakakiri kwamba hakuna upendeleo katika hili. Wanakiri kwamba mpira wa Zanzibar umeshuka katika kiwango kikubwa. Tatizo la kwanza lipo katika udhamini. Zanzibar haiamini katika udhamini wa kamari na pombe ambao kwa kiasi kikubwa ndio unatawala katika soka duniani kote.

Katika ile dunia ya zamani Zanzibar walishindana kwa sababu hata Tanzania hakukuwa na mambo haya. Matokeo yake hata wafadhili wa Zanzibar walikuwa na jeuri ya kuchukua wachezaji kutoka pande nyingine za dunia. Marehemu Naushad Mohamed katika kiburi chake cha hali ya juu cha pesa alikuwa Mtanzania wa kwanza kuleta wazungu kuja kuchezea timu yake.

Aliwaleta wazungu wawili kutoka Bulgaria ambao walikuwa wanajua soka kweli kweli. Akamleta Mordon Malitoli kutoka Zambia kisha akawatwaa Edibily Jonas Lunyamila na Nico Bambaga kutoka Yanga. Ile ilikuwa dunia ya usawa. Baada ya ufadhili kuondoka na kisha udhamini kushika hatamu basi Zanzibar ikaanza kudorora.

Matokeo yake Bara ndio imeonekana kuwa Ulaya ya wachezaji wa Zanzibar. Mchezaji mzuri wa Zanzibar sehemu anayoishia ni kutakiwa na timu za Bara. Huku ndio walau anaweza kupata maslahi mazuri. Zamani kutokana na kipato wachezaji wa Zanzibar walikuwa wanaishia kucheza Zanzibar. Hao wachezaji wengi niliowataja hapo juu waliishia kucheza Zanzibar kwa sababu waliridhika na walichokipata.

Waliovuka kuja kucheza Bara ni wachache tu kama marehemu Riffat Said. Mambo yalipoharibika ndipo wakaanza kuja kina Abdi Kassim ‘Babi’, Kassim Issa ‘Chim’ na baadaye kina Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Leo ndio tumefika hapa ilipo kwa kinda wa miaka 18 kutoka Zanzibar kukimbizwa na Simba na Yanga. Zamani angeishia huko huko mpaka akomae na kucheza timu kubwa za Zanzibar.

Kijana wa Zanzibar mwenyewe kipaji leo anaona bora azamie Ulaya kusaka maisha au atafute mtumbwi wa kwenda kuvua samaki maarufu kama chombo. Yote hayo yasingeshinda utajiri wa soka kama Zanzibar wangeendelea pale pale walipoishia. Hata Fei na Bacca naamini wamepata pesa nyingi miaka hii kuliko washkaji zao waliowaacha kijiweni wakijishughulisha na uvuvi.

Hili eneo ndilo ambalo Mheshimiwa Rais anapaswa kuliangalia kwa umakini mkubwa. Kwanini vipawa vya Zanzibar vimetoweka? Nini kilifanyika zamani ambacho sasa hivi hakifanyiki? Wazanzibar hawashindani tena na vipaji ni nadra kwa sasa. Majuzi ametokea kijana mmoja anaitwa Shekhan Ibrahim Khamis amefanya Simba na Yanga zikimbizane. Zamani wangekimbizana kwa wachezaji wangapi?

Sifahamu kuhusu michezo mingine ndani ya Zanzibar lakini kuhusu soka nina ushuhuda. Kuna mahali Zanzibar walifika na wangeweza kuwa moja kati ya kisiwa cha kutolea wachezaji kwa klabu za Ulaya na kwingineko. Hata sasa naamini kina Fei wanaweza kuzalishwa kwa wingi Zanzibar. Na pengine hili linaweza kuwa jambo muhimu kuliko uanzishwaji wa Old Trafford nyingine.

Tungeweza kuweka viwanja vya kisasa vya vijana kisha tukatafuta mkondo wa kuwapeleka nje. Inaonekana kuna tatizo la kuandaa vipaji na pia kuandaa mapokeo ya wachezaji wenyewe kwenda katika ngazi za juu. Wachezaji hawaandaliwi vema kiakili na ndio maana wengi wao wanaamua kwenda kwenye chombo kuvua.

Kuweka Old Trafford ambayo itatawaliwa na wageni halitakuwa jambo la busara sana. Old Trafford ya Zanzibar inapaswa iendane sambamba na kurudi kwa kina Juma Kidishi wapya. Itapendeza. Binafsi niliwahi kuwaona wachezaji hawa.

Leo wangeweza kuwa wanacheza katika klabu mbalimbali kubwa barani Afrika na Ulaya kwa ujumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live