Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Okrah ndio basi tena

Okrah Kituu Augustine Okrah

Wed, 8 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Winga mahiri wa Simba aliye majeruhi, Mghana Augustine Okrah anahesabu siku tu kwa sasa akiwa amebakiza kama mechi saba za Ligi Kuu Bara kabla ya kusepa zake klabuni hapo kwa kile kinachoelezwa ni kutoridhishwa na namna mabosi wa klabu hiyo wanavyomtendea tangu ajiunge nayo.

Okrah aliyefunga bao la kuongoza la Simba kwenye Kariakoo Derby dhidi ya Yanga katika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, likiwa ni kati ya mabao manne anayoyamiliki katika Ligi Kuu Bara hadi sasa alitua Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea timu ya Bechem United ya Ghana na kupokewa na mashabiki wa soka kwa matumaini makubwa lakini hadi sasa hajaonyesha maajabu makubwa.

Mbali na kushindwa kufanya yake uwanjani na hasa baada ya kuwa majeruhi, lakini kuna jingine lililoibuka ambalo limemfanya mchezaji huyo kutaka kuachana na Si

Mwanaspoti limethibitisha winga huyo kupitia kwa wakala wake ambaye ni Mghana pia kuwa tayari wameandaa barua ya kuwapelekea mabosi wa Simba wakiwaomba wamuachie huru mchezaji huyo mwisho wa msimu ili akatafute changamoto sehemu nyingine.

Mmoja wa marafiki wa karibu wa Okrah amelipenyezea Mwanaspoti kuwa kiungo huyo yupo Dar es Salaam akiendelea kuuguza majeraha, lakini moyo wake haupo tena ndani ya Simba na sasa anahesabu mechi saba za ligi ziishe ili arudi kwao Ghana.

“Kwa sasa Okrah hana furaha na Simba. Kuna vitu kwa upande wake anaona sio sahihi kufanyiwa, lakini hajioni akiwa na mwendelezo mzuri ndani ya kikosi hicho, hivyo anasubiri msimu uishe ili aondoke,” alisema rafiki huyo wa karibu wa Okrah.

“Ni vitu vingi vimemzunguka sio suala la majeraha tu, bali ana baadhi ya tuhuma ambazo sio za kweli kutoka kwa baadhi ya watu wa Simba.”

Rafiki wa mchezaji huyo alidokeza kuwa baadhi ya tuhuma anazopewa Okrah nyingi ni za kinidhamu ikiwemo ugomvi na wachezaji wenzake mara kwa mara, kutoroka na kutoripoti kambini ndani ya muda unaotakiwa na kutopenda kusafiri jambo ambalo amekiri ni ugonjwa wake wa muda mrefu.

“Hayo mengine hayana ukweli, labda hilo la kushindwa kusafiri na timu masafa marefu. Okrah ana shida na usafiri wa ndege akisafiri safari ndefu akiwa angani inamhitaji muda usiopungua siku mbili kurejea kwenye hali yake (ya kawaida) sasa kwa ratiba za Simba hilo huwa linamchangaya sana,” alisema rafiki huyo.

“Sio yeye tu, kuna watu wengi duniani hawapandi ndege kutokana na tatizo hilo. Kuna wengine hawavuki maji na wengine hawapandi hata mabasi, hilo linatokea na kwa Okrah ndege ni changamoto.”

Jambo lingine ambalo Mwanaspoti limeambiwa juu ya mchezaji huyo ni kwamba Okrah hana maelewano mazuri baadhi ya watu katika benchi la ufundi la Simba chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na huenda asionekane tena uwanjani akiwatumikia wana Msimbazi hao hadi mwisho wa msimu huu.

Kutokana na hali hiyo, inaufanya uongozi wa Okrah kuanza kumtafutia timu nyingine winga huyo kwani unaamini licha ya kutaka kuondoka lakini pia hayupo kwenye mipango ya benchi la Simba kwa msimu ujao chini ya Robertinho.

Ulipotafutwa uongozi wa Simba kuzungumzia jambo hili haukupatikana hadi tunaingia mitamboni, lakini awali Ofisa Habari wa Ahmed Ally alilithibitishia Mwanaspoti kuwa Okrah ana majeraha na atakapopona atajiunga na wachezaji wenzake katika timu.

Mara ya mwisho Okrah kuonekana kwenye kikosi cha Simba, ilikuwa Februari 5, mwaka huu katika mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan na baada ya hapo hajaonekana tena mazoezini, safarini na hata kwenye mechi nyingine za Simba.

Licha ya kufunga mabao 14 msimu uliopita akiwa na Bechem ya nchini Ghana, tangu amejiunga na Simba amefunga mabao manne kwenye ligi likiwemo lile alilofunga dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga katika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Timu zingine alizowahi kuchezea Okrah ni Asante Kotoko, NorthEast Utd, Smouha, Al Hilal, Al Merrikh, Häcken, Liberty Prof. na RB Ghana.

Simba inatarajia kukutana na kushuka uwanjani leo katika Uwanja wa Mkapa kuikaribisha Vipers ya Uganda kwenye mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live