Kiungo mshambuliaji mpya wa Yanga, Augustine Okrah tayari ameshatambulishwa ndani ya klabu hiyo jana wakati timu yake ikiwa uwanjani kwenye pambano la michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, lakini mabosi wake wakapiga akili ndefu juu ya Mghana huyo aliyewahi kukinukisha Simba kwa msimu mmoja tu.
Okrah ametua Yanga akitokea Benchem United ya Ghana aliyojiunga nayo tena akitokea Simba mwishoni mwa msimu uliopita, akiwa ni mchezaji wa pili mpya wa Yanga baada ya kiungo Shekhan Ibrahim Khamis aliyesajiliwa kutoka JKU ya Zanzibar.
Mghana huyo aliyeondoka Simba akiwa ameifungia mabao manne na kuasisti moja kwenye mechi za Ligi Kuu anatua Yanga ili kuchukua nafasi ya beki wa kati kutoka Uganda, Gift Fred anayetarajiwa kupewa mkono wa kwa heri baada ya kushindwa kufanya maajabu tangu aliposajiliwa katika dirisha kubwa.
Katika kuhakikisha nyota huyo aliyefunga mabao tisa katika mechi 15 za Ligi Kuu ya Ghana akiwa na Benchem kwa msimu huu, anaitumikia kwa ufanisi, imeamua kumpa mkataba wa miaka miwili wenye masharti magumu ukimtaka wakati wote anatakiwa kuwa ndani ya mstari sahihi wa nidhamu.
Mabosi wa Yanga wameamua kumpata mkataba huo mgumu Mghana huyo, baada ya kusikilia kelele nyingi za mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo wakidai hatofautiani nidhamu na winga wa zamani anayetokea pia Ghana aliyewika Simba na Yanga, Bernard Morrison aliyepo kwa sasa FAR Rabat ya Morocco.
Yanga imewashusha presha mashabiki wake ikisema mkataba ambao Okrah amepewa umezingatia vipengele vigumu vya nidhamu ambao kama atatoka nje ya mstari tu itakula kwake.
Hatua hiyo ya inakuja kufutai uwepo wa madai mbalimbali kuwa Okrah kabla ya kuondoka Simba alikuwa akikabiliwa na makosa mbalimbali ya kinidhamu ya nje ya uwanja.
“Tunajua hilo ingawa hatuna uthibitisho nalo kwa kuwa linasemwa sasa lakini hapa kwetu tumelizingatia haitakuwa rahisi kwake kufanya makosa ya ajabu kama haya ambayo yanasemwa,” alisema bosi huyo wa juu na kuongeza;
“Wapo wachezaji ambao tuliwachukua walisemwa kama ambavyo alisemwa Okrah na walipokuja kwetu hata kama walifanya makosa hayo waliipata fresh tulirudi kwenye mikataba yao na kutoa hukumu.
“Tunaamini atazingatia mkataba wake na anajua kwamba kama ikitokea akafanya makosa hayabasi mkataba huu utamhukumu mara moja ili klabu ilinde hadhi yake.”