Eneo la kiungo ni moja kati ya maeneo muhimu zaidi ndani ya timu, na mara nyingi timu inapokuwa na viungo imara hufanya vizuri pia.Viungo huamua timu icheze vipi, ikabeje na kushambulia vipi.
Kuna aina nyingi ya viungo wengi wanaweza kucheza aina tofauti tofauti ya kiungo. Mchezaji anayecheza kama kiungo mshambuliaji, anaweza kutumika pia kama mchezaji anayeweza kuchezesha timu, beki wa kati au kiungo mkabaji.
Kuna viungo wengi washambuliaji wanaocheza namba nane katika timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.Wapo ambao wamekuwa wakifanya vizuri, wenye viwango vya wastani na pia kuna wanaoshindwa kutoa mchango mkubwa kwa timu zao.
Mwanaspoti lifanya mahojiano na kiungo fundi wa Geita Gold, Deusdedity Okoyo amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na tukio ambalo hataweza kusahau kwenye maisha yake lililomfanya aingie lumande.
ATUPWA JELA KWA KUSINGIZIWA
"Kwenye maisha yangu nimekutana na matukio mengi lakini hili la kuingia lumande ni tukio baya zaidi kwangu na sitokaa nikalisahau kwasababu ni tukio la kusingiziwa."
"Nilikuwa na rafiki yangu tulikuwa kwenye mihangaiko yetu ya hapa na pale ukatokea ugomvi ambapo mwenzangu niliyekuwa nimeongozana naye alikuwa anagombana bahati mbaya akafariki;
"Kwakuwa mimi ndiye niliyekuwa nimeongozana naye nikapakaziwa kesi iliyonifanya niingie gerezani sitaki kuzungumzia kwa upana zaidi hili tukio ila nimeshaingia Segerea bila kutarajia." anasema.
KUNA CHAMA HALAFU BALAMA
Kila mchezaji kwa nafasi anayocheza anakuwa na mchezaji ambaye anamfuatilia na kujifunza kitu kutoka kwake iwe kwenye ligi moja wanayocheza au nje ya ligi.
"Nimekuwa nikivutiwa na wachezaji wawili namna wanavyocheza kwa upande wa wazawa namkubali Mapinduzi Balama (Mtibwa Sugar) nafurahishwa na aina ya uchezaji wake anaweza kukaa na mpira na anajua kutengeneza mashambulizi pia anafunga;
"Kwa upande wa nyota wa kigeni wanaocheza nafasi yangu namkubali sana kiungo wa Simba, Clatous Chama ni mchezaji ambaye anaufanya mpira kuwa mchezo rahisi anajua sana sitaki kumelezea kwa upana zaidi ila kwa wanaofuatilia mpila wanamfaamu vizuri." anasema.
FEDHA ILIVYOMKOSESHA MKE
Kwenye mahusiano kuna changamoto za aina nyingi unaweza ukaachwa kwa sababu za kuchelewesha kujibu meseji, kupokea simu au kushindwa kuelewana.
Okoyo anathibitisha kuwa ameumizwa sana kwenye mahusiano huku akiweka wazi kuwa amekuwa akikutana na changamoto hiyo kutokana na kukosa fedha.
"Kwenye mahusiano nimeumizwa sana si unajua wanawake unaweza ukampenda sana lakini yeye yupo kwako kwaajili ya maslahi binafsi anakuomba kitu unamwambia huna anavumilia akirudi tena ukamwambia huna anaona hakuna umuhimu wa kuwa na wewe hilo limenikuta nimempoteza mwanamke niliyekuwa nampenda kisa fedha."
PADRI HADI KIUNGO
Kila mwanadamu kwenye maisha yake ana ndoto yake na hata mashuleni waalimu wamekuwa wakiuliza kila mwanafunzi anasoma ili awe nani, kwa upande wa Okoyo amethibitisha kuwa ndoto yake ilikuwa ni kuwa padri na sio mpira.
"Mimi malengo yangu yalikuwa ni kuwa Padri na sio kucheza mpira hata jina langu la Deusdedity nilipewa na Askofu mkuu wa Shinyanga ambaye pia aliona kitu kwangu lakini maisha na hali ya uchumi vimenibadilisha;
"Uchumi wa familia na mimi kuhama kutoka Shinyanga na kwenda mkoa mwingine kutokana na majukumu ya wazazi wangu hicho ndicho kilififisha ndoto zangu na kujikuta naangukia kwenye soka," anasema Okoyo
NDONDO HADI LIGI KUU
"Nilikuwa napenda kucheza ndondo sana kutokana na kushindwa kukaa mbali na familia yangu kitendo cha kusajiliwa na timu na kwenda kukaa kambini kilikuwa ni changamoto kwangu;
"Mechi za mitaani maarufu kama ndondo ndio nilikuwa napenda sana nakumbuka siku timu yetu iliomba mechi ya kirafiki na Geita Gild kipaji nilichokionyeha kwenye mchezo huo kiliwashawishi na kuniomba nijiunge nao;
"Dirisha la usajili lilikuwa limefungwa wakaniomba niendelee kujifua nao nikiwa kambini kwao hadi dirisha dogo lakini kabla ya dirisha kocha aliyenipa nafasi alifukuzwa aliyekuja hakunielewa nikaendelea kufanya mazoezi hadi msimu ulipoisha bila kusajiliwa." anasema.
Okoyo anasema baada ya kukaa msimu mzima bila kusajiliwa aliamua kutimkia Zanzibar ambapo alisajilia timu ya BQ inayoshiriki ligi daraja la kwanza alicheza nusu msimu.
"Nilipotoka Zanzibar nilienda Mererani iliyopo Manyala nikacheza Nyanza huko ndipo nilipoonwa na Marehemu kocha Hassan Banyai sasa nikajiunga na Geita Gold, baada ya hapo nikaenda Alliance nilicheza msimu mmoja nikaenda Polisi Tanzani chini ya Malale Hamsini nilicheza misimu miwili sasa nipo Geita Gold tena." anasema Okoyo