Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Okocha aipa mbinu mpya Stars

Gfht Okocha Okocha aipa mbinu mpya Stars

Sat, 14 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Unapolitaja jina Jay Jay Okocha, unawakumbusha wadau wa soka namna alivyokuwa miongoni mwa mastaa walioiwezesha Nigeria kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 1994.

Alicheza kwa dakika 73 katika mechi ya fainali waliyoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zambia kisha kumpisha Nduka Ugbade.

Miaka miwili baadaye, Okocha akawa miongoni mwa wachezaji walioiongoza Timu ya Nigeria chini ya umri wa miaka 23, kuibuka mshindi wa medali ya dhahabu ya michezo ya Olimpiki upande wa soka iliyofanyika Marekani wakiichapa Argentina kwa 3-2 katika fainali.

Katika ngazi ya klabu, Okocha ameshinda mataji tofauti katika timu za Borussia Neunkirchen,  Fenerbahçe, PSG,  Bolton Wanderers na Hull City.

Kiwango chake bora na cha kuvutia uwanjani, hakijamfanya Okocha apate mafanikio katika klabu tu alizochezea bali pia na idadi kubwa ya tuzo binafsi ambazo ni zaidi ya 15, jambo linalomfanya awe miongoni mwa wachezaji bora wa muda wote katika Taifa la Nigeria na Bara la Afrika kwaujumla.

Mwanzoni mwa wiki hii, Jay Jay Okocha alitua Dar es Salaam, Tanzania kushiriki uzinduzi rasmi wa mashindano ya dunia ya soka ya maveterani ambayo kwa mara ya kwanza yatafanyika Kigali, Rwanda, Septemba mwakani na akapata fursa ya kuzungumzia masuala tofauti yanayohusu soka na maisha yake binafsi.

Aipa mbinu Taifa Stars

Nyota huyo ametoa ushauri kwa Tanzania kuhakikisha inakuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa katika ligi kubwa na zenye ushindani Ulaya ili timu za taifa zifanye vizuri.

Kwa mujibu wa Okocha, wachezaji wa Kiafrika wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi na kulifanya soka la bara hili kupigia hatua kwa kuhamishia ubora na ushindani wanaopata huko hadi katika mashindanonya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) na Kombe la Dunia.

“Tanzania ina vipaji vingi vya soka. Kuunganisha vipaji hivi na kupandisha timu ya taifa kwenda ngazi za juu tunahitaji kuona wachezaji wengi wa Tanzania wanashindana katika ligi kubwa za Ulaya.

“Uwezo wa kushindana, uzoefu wa kimataifa na mazingira ya ushindani ya ligi za Ulaya vinaweza kuendeleza ujuzi wao wa mpira wa miguu,” alisema Okocha.

Alisema wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kufikiria kucheza Ulaya sio kwa sababu ya mafanikio yao binafsi tu bali pia manufaa kwa timu ya taifa.

“Kwa wachezaji wengi kuwa kwenye ushindani katika ligi kubwa Ulaya, kikosi cha Tanzania kitanufaika kwa kuongezeka ushindani, ngazi ya juu ya uelewa wa mbinu na uzoefu wa kimataifa wa staili tofauti za uchezaji,” alisema Okocha.

Asili ya jina Jay Jay

Jina lililozoeleka la nyota huyo ni Jay Jay Okocha lakini lile halisi ambalo wengi hawalifahamu ni Augustine Azuka Okocha na ni wazi kwamba wengi hawafahamu ni wapi jina Jay Jay limetokea hadi kuwa maarufu kwa mamilioni ya wapenzi wa soka duniani.

Okocha anafichua kuwa jina hilo lilikuwa linatumiwa na kaka yake ambalo watu walianza kumuita yeye kutokana na urahisi wa kulitaja.

“Kiasili ni jina la kaka yangu ambaye alikuwa anaitwa James Junior. Kunitambulisha mimi kama mdogo wake nilipoanza kucheza wakawa wananiita Augustine mdogo wa Jay Jay.na baadaye ikawa rahisi kuniita Augustine Jay Jay,” anasema Okocha.

Kupenda jezi namba 10

Okocha anasema kupenda kwake kutumia jezi namba 10 katika timu mbalimbali alizowahi kuzichezea kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na majukumu ya nafasi husika uwanjani.

“Kiasili namba 10 ni kiungo mchezeshaji nami ndio nafasi ambayo ninapenda kuicheza. Namba 10 ndio ubongo wa kila timu. Kwa mahitaji ya soka la sasa majukumu yake yamebadilishwa,” anasema Okocha.

Maisha ya wanasoka wa zamani

Maisha ya baadhi ya wachezaji wa zamani kwa sasa sio mazuri na baadhi wamekumbwa na kadhia mbalimbali hasa hali mbaya ya kiuchumi jambo linalofanya baadhi yao kuonekana kituko katika jamii.

Okocha anafichua kushindwa kujipanga na maisha baada ya soka ni sababu kubwa inayochangia maisha ya mastaa wengi waliostaafu soka kuwa magumu.

“Watu wa mpira wanasahau kuwa na sisi ni binadamu pia na sio rahisi kudhibiti umaarufu kwa sababu ya matarajio. Nadhani Siwezi kusema sana kuhusu kila gwiji kwa sababu siko karibu na wengi wao wale ambao niko karibu nao tumekuwa tukibadilishana mawazo tunajaribu kuendana na wakati uliopo jambo ninaloamini ni muhimu katika kutufanya tuwe na jambo la kufanya.

“Na hilo kwangu linasaidia kuiweka vizuri afya ya akili na kama nilivyosema mwanzo kwamba ni muhimu kuwa na mpango mbadala ukizingatia mpira wa miguu unahitajika kukupa msingi wa kujijenga kwa sababu ni kazi ya muda mfupi,” alisema Okocha.

Hata hivyo, Okocha anaamini angalau kwa sasa kundi kubwa la wanasoka waliostaafu katika miaka ya hivi karibuni halina hali ngumu kiuchumi kulinganisha na miaka mingi ya nyuma.

Ladha ya soka kupungua

Okocha anasema kwa sasa mchezo wa soka umekuwa wa matokeo zaidi jambo ambalo anahisi linachangia kupunguza ladha.

“Nadhani ni muhimu kutochukua furaha ya kucheza mpira wa miguu kwa watoto. Tuwafanye watoto wapende kucheza mpira badala ya kuangalia zaidi zao la mwisho kwa sababu watoto wengi sasa hivi wanawaza kwanza ndege binafsi, magari ya kifahari, majumba. Wanachosahau ni kwamba unapokuwa na mafanikio unatakiwa uwe na haki ya kufurahi,” alisema Okocha

Watoto wa mastaa

Kiungo huyo wa zamani wa PSG, anafichua siri ya kinachochangia wachezaji wengi wa soka maarufu kutopenda watoto wao kucheza soka.

“Nadhani presha inakuwa kubwa na watu wanatamani kuona wanafikia pale ambapo wazazi wao wamefikia jambo ambalo linasababisha kutotimiza matarajio hivyo ndio maana wengi hawapendi kuona watoto wao wakicheza soka,” alisema nyota huyo.

Anajikita na biashara, ubalozi

Tofauti na wanasoka wenzake wengi ambao huwa wanasiasa au viongozi wa vyama vya soka pindi wanapostaafu, Okocha anasema ameamua kujikita na biashara tofauti pamoja na kufanya shughuli za kibalozi za taasisi na kampuni tofauti akiamini haziwezi kumbana kufanya mambo mengine binafsi.

Alichosema Okocha kuhusu Stars kina ukweli?

Chanzo: www.tanzaniaweb.live