Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Okocha: Nigeria tuna nafasi kubwa AFCON 2023

Augustine Jay Jay Okocha Gwiji wa soka wa Nigeria, Austin ‘Jayjay’ Okocha

Thu, 18 Jan 2024 Chanzo: Dar24

Gwiji wa soka wa Nigeria, Austin ‘Jayjay’ Okocha, amesema fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka huu nchini Ivory Coast zinaonyesha hamna ‘underdogs’ na pia timu zinazoweza kutwaa ubingwa ni nyingi, huku akimsifu staa wa Super Eagles, Victor Osimhen kuwa ni mshambuliaji wa kiwango cha dunia anayeweza kuwapa ubingwa.

Nigeria inawavaa wenyeji Ivory Coast leo Alhamis katika mechi ya pili ya Kundi A na Okocha amesema ni mechi ambayo inasubiriwa na dunia nzima.

Super Eagles iliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Equatorial Guinea katika mechi yao ya ufunguzi, wakati Ivory Coast ilitoka na ushindi wa kibabe wa 2-0 dhidi ya Guinea-Bissau, huku Osimhen akitupia bao moja.

Kila mechi ni ngumu, lakini ukicheza dhidi ya nchi mwenyeji, inakuwa ngumu zaidi. Lakini, lakini utamu wa soka ni kwamba ili uwe bingwa ni lazima uwafunge mabingwa. Na kama tunavyojua, katika soka kila mechi ni ngumu.

Kama umejiandaa vyema unakuwa na nafasi ya kushinda mechi. Lakini, sisi Wanigeria, tunajua itakuwa mechi ngumu, lakini pia tunaamini tuna uwezo wa kushinda,” amesema Okocha.

Fundi huyo wa mpira ameongeza, “Tunajua Victor Osimhen ni mfungaji wa kiwango cha dunia na mchezaji mkubwa. Anahitaji huduma kutoka kwa wachezaji wenzake na naamini alipata katika mechi ya kwanza. Sio wakati wote ukipata nafasi utafunga. Lakini naamini ana njaa ya kurekebisha makosa ya mechi ya kwanza, tunamuamini kwa sababu anao uwezo wa kung’aa katika michuano hii.

“Naipa nafasi kubwa Nigeria ya kutwaa ubingwa msimu huu. Lakini kuna timu nyingi sana zinazoweza kutwaa ubingwa.

Senegal walianza vyema, Morocco, walitisha kwenye Kombe la Dunia. Lakini pia ukiziangalia timu kama Cape Verde, Equatorial Guinea, Angola, huwezi kuzipuuza.

Huwezi kuzichukulia tena kama ‘underdogs’. Nina uhakika wenyeji Ivory Coast wanaweza kutwaa kombe hili.

Chanzo: Dar24