Kikosi cha Simba tayari kipo jijini Casablanca, Morocco kwa ajili ya pambano la kukamilisha ratiba ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casabalanca litakalopigwa saa 7 usiku wa kuamkia jumamosi, huku mabosi wa klabu hiyo wakijipanga kupangua benchi la ufundi.
Simba itavaana na Raja kukamilisha ratiba ya kundi hilo, kwani timu zote zimeshafuzu robo fainali, huku zote zikiwa na kumbukumbu ya pambano la awali lililopigwa jijini Dar es Salaam kwa Raja kushinda mabao 3-0, hivyo Wekundu watakuwa na kazi ya kutaka kulipa kisasi kwa wenyeji wao.
Hata hivyo, wakati Simba ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo huo kabla ya kurejea nyumbani kwa mechi ya Kombe la ASFC itakapoumana na Ihefu siku ya Aprili 7 na siku chache kurudiana nao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa jijini Mbeya, mabosi wa Simba wameanza mipango ya chinichini ya kulipangua benchi la ufundi lililopo chini ya Kocha Roberto Oliveira 'Robertinho'.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, mabosi wa Simba wameanza kufumua benchi hilo kwa kumtoa aliyekuwa kocha msaidizi, Seleman Matola kwa kumpa kazi ya kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Soka la Vijana na Wanawake.
Baada ya hapo watahamia kwa Meneja, Patrick Rweyemamu ambaye anatarajiwa kuhamishiwa kwenye kikosi cha timu ya vijana (Simba B) kama alivyowahi kufanya kazi hiyo miaka 10 iliyopita na kuibua vipaji lukuki vinavyotamba kwa sasa nchini.
Taarifa hizo zinasema kuwa, nafasi ya Rweyemamu inatarajiwa kuzibwa na Mratibu wa sasa wa timu hiyo Abbas Ally Seleman, aliyekuwa akiishikilia nafasi hiyo kabla ya kubadilishana na meneja huyo wa sasa.
"Mbali na Rweyemamu kupelekwa timu ya vijana, lakini hata kocha wa viungo kutoka Afrika Kusini Kelvin Ndlomo kuna nafasi kubwa ya kupigwa chini ili kupisha mtaalamu mwingine mpya, ila kwa sasa jambo hili linafanywa kwa usiri mkubwa," kilisema chanzo hicho na kueleza sababu ya mabadiliko hayo ni kutaka kutengeneza benchi litakaloenda na mipango ya uongozi mpya wa klabu hiyo.
Rweyemamu ambaye ameambatana na timu hiyo nchini Morocco alipotafutwa kwa njia ya mtandao alisema bado hajapokea taarifa rasmi juu ya jambo hilo, japo alikiri amekuwa akisikia tu hewani suala hilo. Hata hivyo, Rweyemamu alisema, kama jambo hilo kweli lipo hana shida kwani alishawahi kuifanya kazi nzuri katika soka la vijana na matunda yameonekana hadi leo.
"Kama ulivyosikia wewe, ndivyo nami nimesikia tu hewani, lakini sijapewa taarifa rasmi, ila kama viongozi wakiona nafaa kwenda kwa vijana basi, nitakwenda. Siwezi kubisha, ila ukweli hadi sasa sina taarifa rasmi," alisema Rweyemamu na kuongeza;
“Nafahamu Matola (Seleman) ndiye aliyepewa dhamana ya kwenda kwa vijana, ila kwa upande wangu niko safarini na wachezaji tunaenda Morocco.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salum Abdallah ‘Try Again’ alipoulizwa juu ya taarifa hizo, alisema hawezi kulitolea ufafanuzi wowote kwa vile mwenye nafasi ya kufanya hivyo ni Mtendaji Mkuu, Imani Kajula. Kajula alipotafutwa na kuulizwa na Mwanaspoti alisema hajui lolote juu ya taarifa hizo na kama suala hilo litakuwepo, basi umma utajulishwa kupitia tovuti na akaunti za mitandao ya kijamii za klabu hiyo.
Rweyemamu, Seleman Matola pamoja na Amri Said anayeinoa kwa sasa KVZ ya Zanzibar ndio waliokuwa wapishi walioibua vipaji lukuki kupitia timu ya Simba B miaka ya 2010 na kuwaibua nyota kama Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, William Lucian 'Gallas', Edward Christopher na wengineo waliotapakaa kwa sasa katika klabu mbalimbali nchini.