Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ofisa Habari Azam FC amefungiwa kwa kusema ukweli

Zaka Za Kazi Ban.jpeg Msemaji wa Azam FC, Thabit Zakaria

Tue, 11 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mwingine hii nchi ina mambo ya ajabu sana. Kuna watu wamejijengea ngome zao na hawataki kuguswa kabisa. Ni kama hawa watu wa mpira.

Hivi majuzi imetoka taarifa ya kushtua ya Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ kufungiwa miezi mitatu kwa kosa la kuwakashfu waamuzi wa mechi yao na Tanzania Prisons pale Mbeya. Ni adhabu ambayo imeanza mara moja.

Wakati Zaka akifungiwa, waamuzi wa mchezo huo wakiongozwa na Hance Mabena wamepelekwa kwenye Kamati ya Waamuzi kwa kushindwa kuumudu mchezo huo.

Hapa sasa ndio kituko chenyewe kinapoanzia. Kwa nini Zaka afungiwe kama tunakiri kweli waamuzi walikosea?

Ni ukweli uliokuwa wazi kuwa Mabena na jopo lake waliionea Azam pale Mbeya. Tena mchana kweupe. Walitaka wafanye madudu yao halafu msemaji wa timu akae kimya? Hapana. Haiwezekani sehemu yoyote duniani.

Uzuri ni Zaka alizungumza kwa mifano iliyokuwa hai kabisa. Alitoa ushahidi wa video kuonyesha namna Azam ilivyoonewa kwenye mchezo huo.

Kila mmoja aliona hilo na kazi ya Zaka ilikuwa kusema. Akatimiza majukumu yake vyema ya kusema. Kwa nini tunalazimisha kuwafunga watu midomo pale wanapozungumza mambo ambayo hatupendi kuyasikia?

Kwa nini tunafungia watu wanaosema ukweli? Hili la Zaka kufungiwa ni uonevu wa wazi wazi. Ni mara ngapi Azam inaonewa na mamlaka zimekaa kimya? Kila mtu anaona kwa miaka kadhaa waamuzi wamekuwa wakishindwa kutenda haki kwenye mechi za Azam. Mfano mzuri ni mechi ya Yanga hapo majuzi tu. Yanga ilifunga bao baada ya kunufaika na mpira uliokuwa umetoka, lakini mwamuzi hakujali.

Pengine Azam ingeshinda mchezo ule kama sio hilo bao la ‘Mchongo’. Lakini nani anajali? Hakuna. Zaka alisimama na kupaza sauti anafungiwa. Kwa nini tunapenda kutengeneza kizazi cha waoga? Ukweli ni msimu huu waamuzi wengi wako ovyo.

Waamuzi wengi wanachezesha mechi chini ya viwango. Hadi kuna wakati unajiuliza kama wamepata mafunzo kweli ama wanakurupuka? Kuna matukio yametokea na kuziumiza timu nyingi. Mfano Singida Big Stars ilipewa penalti ya mchongo dhidi ya Mbeya City pale Singida. Yalikuwa ni maamuzi ya ovyo na yakaiumiza Mbeya City. Lakini watu wanaogopa kusema wasije wakafungiwa.

Pale Mwanza mwamuzi aliizima Singida dhidi ya Geita Gold. Ilikuwa ni mechi ya ushindi kwa Singida lakini kutokana na makosa ya ‘kibinadamu’ ya mwamuzi mchezo ulimalizika kwa sare. Nani anajali? Hakuna.

Hakuna anayeshtushwa kama kilichowakuta Coastal Union kule Lindi katika mechi yao na Namungo. Akijitokeza mtu wa kusema ukweli anafungiwa!

Pale Mbeya, Tanzania Prisons waliminywa dhidi ya Simba. Bao la Simba kwenye mchezo ule limejaa utata, lakini ndio hivyo limeshapita na maisha yanaendelea.

Haya ni baadhi tu ya makosa ya waamuzi ambayo yamezigharimu timu nyingi msimu huu. Kama tunataka kuimarisha soka letu, tunahitaji watu kama kina Zaka. Watu ambao wanaweza kusimama na kusema ukweli pindi mambo yanapokwenda mrama.

Kuwafungia watu wanaosema ukweli ni kurudisha nyuma maendeleo ya soka letu. Mwishowe ni kutengeneza kizazi cha woga na kusifia tu. Tutaishia hapa hapa na maendeleo tutayasikia

Chanzo: Mwanaspoti