Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nzegeli mabao 10, Aziz KI 10, Musonda 10, Yanga tamu

Maxi Nzengeli X Congo Winga mpya wa Yanga Maxi Nzengeli

Thu, 27 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mara ya tano sasa mfululizo, Tamasha la Siku ya Wananchi limefanyika wiki iliyopita pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ni kama kufungua Rasmi msimu mpya wa mashindano. Ni Siku maalumu ya kutambulisha wachezaji na benchi la ufundi.

Ni mwaka mpya wa Kisoka kwa wapenzi na mashabiki wa Yanga. Baada ya mambo yote nje ya Uwanja, kulikuwa na mechi ya Wananchi dhidi ya Kaizer Chiefs kutoka Bondeni pale nchini Afrika Kusini. Ulimuona Skudu? Mwaka jana alikuwa ni Stephen Aziz KI.

Mwaka huu, ilikuwa ni Mahlatsi Skudu Makudubela. Hawa ndiyo wachezaji waliotikisa kwenye usajili wa misimu miwili mfululizo. Aziz KI, hakuna na msimu mzuri licha ya usajili wake kutikisa nchi lakini bado ni mchezaji mzuri. Skudi hana rekodi nzuri za msimu uliopita pale Afrika Kusini lakini anaonekana ni waziri wa raha. Ni fundi wa mpira haswa.

Ni mzee wa Udambwiudambwi. Ni mtu wa kuupanda mpira mwingine amepatikana. Alikuwa kwenye kiwango kizuri dhidi ya Kaizer Chiefs? Jibu langu ni hapana. Hakuwa kwenye kiwango kizuri. Krosi zake nyingi hazikuwa na faida kwa timu. Madoido yake mengi hayakuwa na faida yoyote. Anaoonekana ni fundi wa mpira? Jibu ni ndiyo.

Bado tunahitaji kumuona zaidi na huenda mechi za Ngao ya Jamii kama Yanga atafika Fainali zitaanza kuonyesha uwezo wake halisi. Mchezaji anapopewa promo kubwa, huo ni mtego. Aziz KI msimu uliopita, alitambulishwa kwa makeke mengi matokeo yake hakuna kubwa aliloonyesha baada ya ligi kuanza.

Skudu msimu huu ameletwa kwa manjonjo na jezi namba sita. Matarajio kwake ni makubwa mno. Kumbuka pia jezi namba sita ilikuwa kwa Feisal Salum msimu uliopita aliyetimkia Azam FC. Umeonaje kiwango chake dhidi ya Kaizer Chiefs?.

Kuna mtu anaitwa Nungunungu. Ni Jonas Mkude ndani ya Kijani na Njano. Kama ndiyo kwanza unafika nchini na kumuona dhidi ya Kaizer Chiefs, ungedhani ni mchezaji aliyekuwa na Yanga kwa misimu yote 13 aliyocheza soka. Ni Jonas alikuwa anapiga pasi popote anapotaka. Ni mchezaji aliyemudu hasa Dimba la chini. Ni Jonas yule yule wa Juzi na Jana. Kama atabadilika kwa kiasi kikubwa kwenye maisha yake ya nje ya Uwanja, Yanga wamelamba Dume.

Alifanya kazi ya Mudathir na Maxi Nzengeli kuwa rahisi sana uwanjani. Zile pasi za Mita 20, zote zilitoka mguuni mwake. Kwa kile alichoonyesha dhidi ya Kaizer Chiefs kama kitakuwa na muendelezo, usishangae kumuona anarudi kwenye kikosi cha Taifa Stars. Jonas hajawahi kushuka kiwango, sema tu hakuwa chaguo la kwanza kwa Makocha wa Simba kwa msimu miwili mfululizo. Kutokucheza sana misimu miwili mfululizo ni faida kwa Yanga.

Anaonekana mpya kabisa kutoka kwenye makaratasi. Anaonekana amepumzika vya kutosha. Anaonekana ana mtihani wa kuthibitisha kuwa bado yumo. Kuachwa na Simba ni kama Kengele kwenye kichwa chake kwamba hizi timu kubwa muda wowote anaweza kupishana nazo. Nadhani kuna kitu atabadilika na kuwa msaada. Nadhani atapunguza mambo mengi ya nje ya uwanja.

Maana ukiachwa na Yanga, unaanza taratibu kupotea kwenye ramani ya mpira wetu. Ndoto ya kila mchezaji wa Tanzania na hasa wa zama hizi, ni kucheza ama Simba au Yanga. Kwingine ni daraja tu. Sina nia ya kuvikosea heshima klabu nyingine, lakini mpira wa Tanzania ni Simba na Yanga tu. Hata Azam FC na Singida Fountain Gate pamoja na uwekezaji mkubwa unaoendelea, bado wako chini kwa Simba na Yanga.

Maxi Nzengeli. Maxi Nzengeli. Maxi Nzengeli. Nimemuita mara tatu sio kwa bahati mbaya. Pengine huyu ndiyo alitakiwa kupigiwa Promo ya jezi namba sita. Pengine huu ndiyo usajili Bora wa Yanga msimu huu. Ni aina ya mchezaji mwenye kila kitu uwanjani. Ni mchezaji mwenye nguvu. Ni mchezaji mwenye kasi. Ni kijana mwenye maarifa mengi uwanjani.

Alianza mechi kama mchezaji wa kawaida. Alimaliza mechi kama star mpya wa Yanga. Yanga imekuwa timu ambayo mastaa wake wakubwa sio washambuliaji kiasili. Mawinga pale Jangwani na washambuliaji namba mbili, wengi ndiyo wamekuwa wabeba maono kwa timu tangu enzi na enzi. Ni mara chache sana watu kama kina Fiston Mayele wamekuwa wabeba timu pale Yanga.

Namuona Nzengeli akiirudisha Yanga Asili. Namuona akiwa Star mkubwa sana pale Jangwani. Kama wadada wa Sinza na Magomeni Mapipa hawatomshika masikio mapema, ni bonge moja la mchezaji. Ulimtazama vizuri Nzengeli?.

Muda mwingi wa mchezo wa Kaizer Chiefs, Nzengeli alishambulia kupitia katikati lakini huyu fundi pia wa kutokea pembeni kama winga. Ni mtu na Nusu. Ana nguvu. Ana piga. Kama atazoea Mazingira kwa hataka, Wananchi wameokota Dodo.

Mitihani mkubwa upo Kwa Kennedy Musonda. Hongera kwake kwa kufunga bao dhidi ya Kaizer Chiefs. Lile ni Goli la mechi ya Kimataifa ya Kirafiki, lakini kwa Musonda lilikuwa na maana kubwa. Bado anacheza chini ya mzimu wa Fiston Mayele. Kila timu itakapokosa mabao, hisia za Mayele zitaibuka. Musonda ni mchezaji mzuri na mwenye uzoefu mkubwa, hawezi kuwa Mayele mpya kakini atawabeba Wananchi kuelekea msimu ujao.

Yanga wakiwa na Mayele hawajawahi kushinda mechi ya Siku ya Wananchi hata moja lakini bila Mayele wameshinda. Bila Mayele Musonda amewapa goli la ushindi. Yanga wanahitaji kupata walau mabao 10 kwa Wachezaji watatu tofauti. Nzengeli anapaswa kuwapa magoli 10 kwa msimu, Aziz KI magoli 10 na Musonda Magoli 10. Wakifika kwenye wastani huo, watamsahau Mayele mapema sana. Wananchi ni lazima wafahamu kuwa Musonda sio Mayele.

Ni mchezaji mzuri sana kama atafunga mechi nyingi za mwanzo wa msimu, itampa kujiamini. Umewaonaje Wananchi dhidi ya Kaizer Chiefs? Naomba maoni yako kwa njia ya Ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: