Klabu ya KMC imepata pesa za kuanzia Ligi vizuri baada ya kumuuza Mlinda Lango wao Hussein Abel kwenda katika kikosi cha Simba SC kwa ajili ya msimu ujao.
Simba SC ilikuwa na ulazima wa kusaka Mlinda Lango baada ya aliyekuwa kipa wao mpya, Jefferson Luis kuumia na kuamua kuachana naye.
Baada ya hapo, Simba SC ilihaha huku na kule kusaka Mlinda Lango kwa haraka na baada ya kuona hawawezi kuchukua kipa wa kigeni wakaangukia kwa Hussein Abel wa KMC.
Kuchomoka kwa Abel katika kikosi hicho haikuwa rahisi, kwani bado alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na miezi sita na tayari alishaitumikia timu hiyo miezi sita msimu uliopita.
Habari kutoka ndani ya KMC na mchezaji huyo zimedokeza kwamba mazungumzo ya Simba SC na waaajiri wa Abel waliafikiana kulipa kiasi cha Sh 120 milioni.
“Simba SC walikuwa na uhitaji zaidi kwa Abel kwahiyo walitoa kiasi hicho cha fedha, Abel alikuwa na mkataba wa muda mrefu kwetu,” kimesema chanzo hicho.
Abel alijiunga na KMC katika dirisha dogo la Januari msimu uliopita na akitokea Tanzania Prison na aliitumikia timu hiyo kwa miezi sita tu.
Kipa huyo alitambulishwa rasmi Jumapili (Agosti 06) katika kilele cha Simba Day na ndipo mashabiki wengi wa soka wakawa wanajiuliza juu ya usajili wake ilihali bado alikuwa na mkataba na KMC.
Ujio wa Abel kwenye kikosi cha Simba ni wazi unakwenda kuongeza kitu, kwani kipa huyo atakutana na wenzake, Aishi Manula, Ally Salim na Ally Ferooz.