Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyuma ya mafanikio ya Rashford kuna Lucia

Marcus With Girl Nyuma ya mafanikio ya Rashford kuna Lucia

Tue, 5 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna msemo maarufu duniani katika lugha mbalimbali, kikiwemo Kiswahili, kwamba ‘Nyuma ya mafanikio ya kila mwanaume, kuna mwanamke.’

Kwa wanaume ambao bahati mbaya hawakukutana na wanawake sahihi, na badala ya mafanikio kwao ikawa maanguko, hawatauelewa msemo huu...lakini maisha ndiyo yako hivyo, hakuna kila kitu kwa kila mtu. Ila kwa wale ambao mafanikio yao yalijengwa na uimara au nyota ya mwanamke nyuma yao, ni mashuhuda wa msemo huu.

Moja ya watu hao ni mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford.

Dogo huyu mzaliwa wa jiji la Manchester, alijiunga na akademi ya Manchester United akiwa na miaka 7.

Maskauti wa United walimuona kwenye mashindano ya timu za watoto wa umri huo, akiichezea timu ya akademi ya Fletcher Moss Rangers aliyojiunga nayo akiwa na miaka mitano.

Akademi hii ilianzishwa mwaka 1986, ambao Sir Alex Ferguson pia alijiunga na Manchester United.

United ilikuwa na mazoea ya kuchukua vipaji kutoka Fletcher Moss Rangers, akiwemo Danny Drinkwater, Jesse Lingard, Danny Welbeck na hata Johnny Evans.

Kwa hiyo walipomuona Rashford, ikawa rahisi kwao. Lakini wakati huo alikuwa golikipa.

Katika nafasi yake ya golikipa, Rashford alimfuatilia sana kipa wa United wakati huo, Tim Howard, kutoka Marekani. Baada ya majaribio ya wiki moja, Rashford akajiunga na akademi ya United, akizitosa Everton na Liverpool zilizomtaka pia.

Akabadilishwa nafasi na kuwa mshambuliaji na akiwa na miaka 11, akahamia kwenye hosteli za akademi baada ya mama yake kuiomba Manchester United kumchukua moja kwa moja ili kumpunguzia majukumu.

Mama huyo masikini alielemewa na familia aliyokuwa akiilea peke yake baada ya baba kuikimbia.

United ikakubali na kumchukua, japo ilikuwa kinyume cha sheria zao ambazo zilitaka watoto wa kuanzia miaka 12 kukaa hosteli.

Alipomaliza shule ya msingi, Manchester United wakampeleka shule ya sekondari ya Ashton -on-Mersey. Shule hiyo ilikuwa kitengo chake kinachoitwa Sports College ambapo Rashford alijiunga nacho na kusomea Biashara na Elimu ya Teknolojia (Business and Technology Education Council - BTEC) na pia kupata Diploma ya Taifa kwenye michezo.

Akiwa bado mwanafunzi wa shule hii wa miaka 15 tu, Rashford akakutana na msichana aliyeitwa Lucia Loi.

Msichana huyu ndiyo kisa cha andiko hili...ndiyo mwanamke aliye nyuma ya mafanikio na maanguko ya Marcus Rashford.

MAFANIKIO

Akiwa na miaka 17 alisaini mkataba wake wa kwanza chini ya kocha David Moyes.

Alipofikisha miaka 18 akapandishwa na kocha Louis van Gaal na hatimaye kucheza mechi yake ya kwanza ambayo alifunga mabao mawili na kumfanya kuwa staa ghafla. Rashford akawa tegemeo la Manchester United na hatimaye kubadilisha namba ya jezi kutoka 19 aliyoanza nayo kwenye timu kubwa hadi 10.

Rashford akapanda hadi kuwa staa wa timu ya taifa na mwaka 2018 yeye na wenzake wakafanya kilichoshindikana kwa miaka mingi kwenye Kombe la Dunia kule Urusi. Wakati Rashford akifanya makubwa uwanjani, Lucia alikuwa akifanya makubwa jukwaani kumshangilia mpenzi wake.

Rashford akanunua jumba la zaidi ya Sh3 bilioni na kuhamia na mpenzi wake huyo.

Kadiri penzi lao lilivyoshamiri ndivyo Rashford alivyong’ara uwanjani. Msimu wa 2019/20, Rashford alifanya vizuri sana uwanjani akihusika na mabao 31 (kufunga na pasi za mabao).

Msimu uliofuata, 2020/21 ndiyo ulikuwa balaa zaidi kwani Rashford alikuwa wa moto akihusika kwenye mabao 34 (kufunga na kutoa pasi za mabao).

ANGUKO

Baada ya miaka 8 ya kuishi sayari nyingine, mwaka 2021 penzi lao likaingia kidudu mtu na kutengana kwa mara ya kwanza.

Hapo hapo kiwango chake kikashuka na msimu uliofuata, 2021/22, alihusika na mabao 7 tu (kufunga na kutoa pasi za mabao)

MAFANIKIO

Mwaka 2022 Rashford na Lucia wakarudiana, na kiwango chake likarudi pia.

Msimu uliofuata wa 2022/23 Rashford akauwasha hatari, akihusika kwenye mabao 39 (kufunga na kutoa pasi).

ANGUKO

Mwaka huu 2023 wakatengana tena na kiwango cha Rashford kimeporomoka ghafla.

Msimu huu hadi sasa Rashford amehusika na mabao manne tu.

MAFANIKIO TENA?

Sasa wamerudiana tena, je kiwango cha Rashford kitarudi?

Tusubiri na tuone!

Chanzo: Mwanaspoti