Beki na winga wa Singida Fountain Gate FC, Nickson Kibabage anatarajia kuonekana na uzi wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, msimu ujao.
Kibabange, ambaye amefanya vizuri kwenye Ligi Kuu msimu uliopita, awali alikuwa akitajwa kuwa anaweza kujiunga na Simba, lakini jana ilifahamika kuwa amepewa mkataba wa miaka miwili na Yanga, ambao utasainiwa Julai 1.
Beki huyo wa kulia na kushoto imeelezwa kuwa akizunguka na mkataba huo kwenye gari lake kusubiri tarehe rasmi ili asaini na kuwa mali ya Yanga rasmi baada ya timu zote kuafikiana.
Ikiwa hilo litakamilika, Upande wa kushoto wa Yanga utakuwa na nguvu zaidi kutokana na uwepo wa Joyce Lomalisa, ambaye pia ni mzuri katika kushambulia.
"Alipewa mkataba wikiendi, akaenda kuusoma na wakakubaliana kuwa upo sawa na hata fedha nyingine ameshapewa anatamba nazo mjini, Yanga ilikuwa inataka kumsajili tangu dirisha dogo, lakini haikufanya hivyo," kilisema chanzo cha uhakika ndani ya Yanga.
Mwananchi lilimtafuta beki huyo mahiri, ambaye alifunga mabao manne na pasi tatu za mabao katika mechi 15 za msunguko wa pili wa Ligi Kuu, alisema bado usajili huo haujakamilika.
"Nimeziona taarifa hizo zinazosambaa, lakini ukweli hadi sasa bado sijui kitu chochote, labda Yanga wanitake siku mbili hizi, lakini bado nina mkataba na Singida na lazima waanzie kwao," alisema beki huyo.
Mbali na kucheza kama beki, Kibabage pia amekuwa akitumika kama winga kwenye baadhi ya michezo kuanzia akiwa Mtibwa Sugar, kabla hajatua Singida Big Stars iliyogeuka kuwa Fountain Gate.
Ni rasmi sasa ataungana na nyota wengine aliocheza nao kwa mafanikio ndani ya Mtibwa Sugar na timu ya Taifa ya vijana (U-17), kipa Abutwalib Mshery na mabeki Kibwana Shomari na Dickson Job.
Kabla ya kujiunga na Singida kwenye dirisha dogo, beki huyo aliwahi kuzichezea Mtibwa Sugar, KMC na Difaa Al Jadida ya Morocco.