Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyota walionusurika kujiunga klabu ndogo England  

23c228f357be611c3f9a9afb76bcb65d Straika wa Bayern Munich, Rober Lewandowski

Wed, 15 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mchezaji akishakuwa nyota ni kawaida kujiunga na klabu kubwa, na hata sasa tunaona chipukizi waliotokea kuwa imara ghafla wakitafutwa na klabu kubwa kwa ajili ya kujiunga nazo.

Klabu kubwa zinajulikana, baadhi zikiwa ni Bayern Munich, Barcelona, Real Madrid, Manchester City, Chelsea, Arsenal, Manchester United, Porto, Liverpool, Juventus, Inter Milan, AC Milan na nyinginezo.

Wapo lakini, wachezaji nyota kutoka nchi mbalimbali ambao ilikuwa nusura watue kwenye klabu ndogo za England na hapa tunawatazama.

Roberto Carlos – Aston Villa

Mwenyekiti wa Aston Villa, Doug Elis, mnamo 1995 alivutiwa sana na uchezaji wa Roberto Carlos, beki kisiki wa Brazil na ilikuwa kwenye mechi baina ya Brazil na Sweden, ikiwa ni ya kirafiki iliyochezwa Villa Park.

Villa walikwenda mbali zaidi na kufanya mazungumzo na mchezaji huyo aliyekuwa akikipiga Palmeiras, lakini ikawa kwamba hatimaye kocha Brian Little hakumpenda Carlos, badala yake akamsajiliSouthgate kutoka Crystal Palace. Kwa hiyo leo ingekuwa historia kwamba Carlos alipata kucheza Villa, timu ndogo ya England.

Carlos, badala yake, alijiunga na Inter Milan wa Italia 1996 – ambako Roy Hodgson, alijaribu kumtumia kama mshambuliaji na mchezaji huyo kulalamika akisema; “Sikupenda mfumo wala eneo ambalo Hodgson alinitaka nicheze.”

Robert Lewandowski – Blackburn Rovers

Mwaka 2010 Kocha wa Blackburn, Sam Allardyce alifikia makubaliano ya dili la pauni milioni 4.2 kumsajili Robert Lewandowski ambapo klabu yake ya Lech Poznan ilishakubali kila kitu. Hata hivyo, dili hilo lilibumburuka baada ya kutokea volcano huko Iceland na majivu yakazuka kwa wingi kiasi kwamba ilibidi ndege zisiruke, hivyo mchezaji huyo kushindwa kuingia England.

Ama kwa hakika Allerdyce, au kama anavyojulikana ‘Big Sam’ hawezi kusahau wala kuisamehe dunia kwa hilo. Badala Lewandowski, alimsajili Nikola Kalinic na baadaye Lewandowski akajiunga na Borussia Dortmund alikoshinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani – Bundesliga mara mbili.

Andriy Shevchenko – West Ham

Harry Redknapp aliyepata kuwa kocha wa Timu ya Taifa ya England – Three Lions, alipata kumpa ofa Shevchenko ya kujiunga na West Ham kwa pauni milioni moja tu miaka ya mwisho ya 90.

Anaiweka hivi Redknapp: “Tulijiwa na rafiki wetu wawili na washabiki wa Villa waliosema kwamba walikuwa wakifanya biashara Ukraine, tukashituka lakini tukafurahi kwamba tungeweza kuwa na dili kwa ajili ya kutazama vijana hawa.

“Mmoja wao, Shevchenko, tulipata kucheza dhidi ya timu yake na alifunga bao la ushindi. Wakasema wanataka pauni milioni moja nikakubaliana nao kabisa lakini wakuu wa klabu wakakataa wakisema eti ni nyingi mno. Mpaka leo nawalaumu kwa hilo kwa sababu tulimwacha akaondoka hivi hivi.”

Gabriel Batistuta – Ipswich Town

Mwanzoni mwa msimu wa 1994/95, Ipswich waliibuka kwa ushangao wakimtaka Batistuta kwa pauni milioni 2.9 baada ya raia huyu wa Argentina akiripotiwa kwamba hakuwa na raha katika klabu yake iliyokuwa imepanda daraja ya Fiorentina.

Kocha John Lyall alielezwa kwamba alikuwa na mawasiliano ya karibu na wawakilishi wa mchezaji huyo, lakini dili hilo likavunjika baada ya La Viola kutoa ofa kubwa zaidi.

Edinson Cavani – West Ham

West Ham walionekana kumtaka sana Edinson Cavani wakati huo akiwa Palermo na inaonekana kana kwamba mwenyewe alifurahi akiona kwamba ilikuwa makubaliano mazuri.

Kocha wa zamani wa raia huyo wa Uruguay, Stefano Colantuono, alieleza kwamba mshambuliaji huyu maarufu alitaka kuingia Upton Park 2008, lengo kubwa kwake likiwa kujaribu changamoto na bahati katika Ligi Kuu ya England (EPL).

Didier Drogba – Portsmouth

Tunarudi tena kwa Redknapp, na safari hii inasema kwamba akiwa Portsmouth aliamua kumsajili mshambuliaji wa Ivory Coast, Didie Drogba ili awe pacha wa mshambuliaji mwingine, Yakubu Ayegbeni wakati klabu hiyo ilipopanda EPL.

Drogba alikuwa mtamu sana akiwa na klabu ya Guingamp na alipata kufunga mara mbili dhidi ya Lyon wakati Redknapp akiwa jukwaani akitazama mechi hiyo.

Hata hivyo, kutokana na uhaba wa fedha klabuni Portsmouth, wakuu wa Pompey walishindwa, wakisema kwamba kima cha pauni milioni 3.5 kilikuwa kikubwa mno na badala yake wakamsajili Teddy Sheringham.

Radamel Falcao - Aston Villa

Mwaka 2008, Kocha wa Aston Villa, Martin O’Neill alipewa fursa ya kumsajili mshambuliaji wa Colombia aliyekuwa ameibukia kwa makali, Falcao, akiwa na klabu ya River Plate nchini Argentina.

Falcao alikuwa tayari kuuzwa kwa pauni milioni tano, lakini O’Neill akafikiria vinginevyo, akaamua kumsajili mpiga mabao mzuri wa Wigan, Emile Heskey.

Zinedine Zidane – Blackburn Rovers

Mwenyekiti wa Blackburn, Jack Walker anaeweza kuwa amewezesha klabu yake kuwa na mafanikio makubwa 1995 lakini hakupatia inavyotakiwa.

Kocha Kenny Dalglish alipendekeza kwamba mchezaji Zidane wa Bordeaux asajiliwe kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kitwae ubingwa. Hata hivyo, Walker alikuwa na majibu ya kukatisha tamaa kwa sababu alimwambia Dalglish; “kulikoni tumsajili Zidane wakati tunaye Tim Sherwood?” Likaishia hapo.

Pierre-Emerick Aubameyang – West Bromwich

Skauti wa zamani wa West Brom, Stuart White, anabainisha kwamba Baggies hao walikuwa na fursa ya kumsajili Aubameyang ambaye sasa yupo Arsenal kwa pauni milioni mbili tu mwaka 2011.

Baada ya kumtazama raia huyu wa Gabon akichezea Saint-Etienne dhidi ya Auxerre, White alipata mawasiliano kutoka kwa wakala wake aliyemwambia kwamba Auba angepatikana kwa bei rahisi tu. Licha ya hayo, taarifa nyingine za kiskauti zilimshawishi vinginevyo. Auba akasonga na kufunga mabao 41 kwenye mechi 97 kabla ya kutwaliwa na Borussia Dortmund kwa pauni 13m kiangazi cha 2013.

Luka Modric – Newcastle United

Ipo simulizi ya aina yake juu ya Kevin Keegan, Newcastle na Luka Modric ambaye awamu yake ya pili Newcastle haikuwa nzuri. Mwaka 2008, bosi alipokea simu kutoka kwa wakala wa Modric aliyekuwa na tamaa ya kumchukua mchezaji huyo kutoka Dinamo Zagreb hadi Newcastle akakipige kwenye Uwanja wa St James’ Park.

Keegan akawa amekubali lakini ndoto yake haikuwa kweli, kwani Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Tony Jimenez, alidai kwamba Modric alikuwa mwembamba, mwenye uzito wa chini na dhaifu mno. Wakamkosa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz