Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyota wa kumrithi Sure Boy pale Azam

Mrithi Pic Data Said Ndemla, Kiungo wa Simba aliyepo kwa mkopo Mtibwa

Sat, 25 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mwisho wa enzi moja ni mwanzo wa nyingine, kile kizazi cha Azam FC ambacho kilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2013/14 ndio kimeishia hivyo kwenye kikosi hicho chenye maskani yake Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Achana na kina Shaaban Chilunda ambao kwa wakati huo ndio waliokuwa wakichipukia hapa, tunazungumzia wale ambao waliipigania jezi ya Azam FC na kufanya makubwa mbele ya vigogo wa soka la Tanzania, Simba na Yanga.

Miongoni mwa wachezaji hao ni pamoja na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye Azam imekubali kumwachia mara baada ya kuwasilisha maombi ya kutaka kuvunjwa kwa mkataba wake na klabu hiyo ambayo amaichezea kwa miaka 14.

Sure Boy ndiye mchezaji pekee ambaye alikuwa amesalia kwenye kikosi hicho kati ya wale ambao waliipandisha timu hiyo huku wakipigana kutwaa ubingwa wao wa kwanza na mwisho Ligi Kuu Bara, walishasepa kitambo tu kama aliyekuwa nahodha wao, John Bocco na Aishi Manula ambao wapo Simba huku wengine waliosajiliwa baadaye na kuipa mafanikio timu hiyo kama Kipre Tchetche, Kipre Balou nao wakiondoka.

Kuondoka kwa Sure Boy ambaye anatajwa kutimkia Yanga sio mwisho wa maisha kwa Azam ni mwanzo wa maisha mengine bila ya fundi huyo, Mwanaspoti inakuletea nyota ambao wanaweza kuvaa viatu vya fundi huyo kama macho ya benchi la ufundi la timu hiyo yatatua kwao kulingana na mahitaji ya kikosi chao.

CLEOPHACE MKANDALA

Ni miongoni mwa injini za Dodoma Jiji, amekuwa kwenye kiwango bora kwa kipindi kirefu tangu akiwa na Tanzania Prisons.

Mkandala sio kiungo mwenye mambo mengi lakini ni mzuri kutekeleza majukumu yake ya msingi, anauwezo mkubwa wa kuutafuta mpira, kuunganisha timu na hata kutengeneza nafasi hilo amelithibitisha akiwa na Dodoma Jiji.

KENNY ALLY

Ni kiungo mzoefu ambaye anaweza kuingia moja kwa moja kwenye timu kama benchi la ufundi la Azam litaona kuwa anaweza kuongeza nguvu kwenye kikosi chao.

Huyu ni fundi tofauti na Mkandala, anauwezo wa kuunganisha timu na kusukuma mashambulizi, mbali na kiungo, Kenny anauwezo wa kucheza nyuma ya mshambuliaji na akawa msaada, tumeonaa mara kadhaa akitumika kwenye maeneo yote akiwa na timu tofauti ambazo amezichezea ikiwemo, Singida United.

DEUSDEDITY COSMAS

Uwezo wake wa kumiliki eneo la kiungo ni mkubwa. Huyu ni aina ya wachezaji ambao huhitaji muda kuonyesha makeke yake.

Kama Azam inatazama mchezaji ambaye anaweza kuvaa viatu vya Sure Boy kwa miaka michache ijayo ikiwa wataona kwenye akademi yao hakuna basi Cosmas ambaye anaichezea Polisi Tanzania anaweza kulibeba hilo.

SAID NDEMLA

Simba ni kama hawana mpango na kiungo wao, Said Ndemla ambaye anaichezea kwa mkopo Mtibwa Sugar, nafasi kwa fundi huyo ni finyu kwenye kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi hivyo anaweza kuwa lulu, Azam FC.

Hakuna asiyeujua uwezo wa Ndemla, amekuwa hodari kwenye kusukuma mashambulizi na kusaidia kukaba pale ambapo timu inakuwa inashambuliwa, akiaminiwa na kupewa nafasi anaweza kutushangaza kutokana na uzoefu alionao.

RAPHAEL DAUD

Alizima kama mshumaa lakini ni miongoni mwa viungo ambao walitikisa akiwa na Mbeya City na hata Yanga kabla ya mambo kumwendea kombo.

Upopo mchafu ulipita kwa Daud kiasi cha kupotea kabisa lakini kwa sasa ameanza kuchomoza upya akiwa na Ihefu FC ya inayoshiriki Ligi ya Championship kama ataaminiwa anaweza kuonyesha kuwa kuteleza sio kuanguka.

Daud ni aina ya kiungo mwenye uwezo kuchezesha timu kwa pasi zake za mbele zenye mlengo wa kushambulia zaidi, Kocha wa timu hiyo Zubeir Katwila ameonyesha imani kubwa kwa fundi huyo na huenda akarejea tena midomoni mwa watu.

WASIKIE WADAU

Kipa wa zamani wa Yanga, Juma Mpongo anaamini kuwa Ndemla na Raphael bado damu zao ni changa na wanauzoefu mkubwa wa kucheza soka la ushindani hivyo mmoja wao akaionekana anafaa anaweza kuziba pengo mna Sure Boy.

“Wenye maamuzi ya mwisho ni benchi la ufundi ambalo huwa na uchanganuzi wao kulingana na vigezo ambavyo wanavitazama lakini kwangu hapo ni wachezaji wenye ubora mkubwa ni vile tu wamepitia vipindi vigumu,” alisema.

Upande wake, Ulimboka Mwakingwe alisema; “Ndemla ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, anakitu miguuni mwake, anaweza kuzipa pengo la Sure Boy na kwa uzoefu anaona wa kutosha na hata presha anaweza kuhimili.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz