Meneja wa Yanga Princess, Kibwana Matokeo ametolea ufafanuzi wa kutoonekana kwa nyota wawili wa kikosi hicho, Richanel Kiteko na Lidya Maximillan ambao hawajacheza wakiwa na timu hiyo tangu waliposajiliwa kuichezea katika dirisha kubwa.
Kibwana alisema Mzambia, Richanel ameshindwa kucheza kwa sababu ya kukwama kupata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) huku kwa Lidya alikuwa kwenye mkataba na kituo cha kukuza vipaji cha THT ambacho muda wowote kikimuhitaji wanamchukua.
“Kituo kiliongea na sisi wakasema kama tunataka kuendelea nae basi tuwape Sh20 milioni za usajili, tukaona ni pesa ndefu na ukiangalia ni mchezaji wa ndani, wakasema tayari wamepata timu ndio wakampeleka JKT lakini hatukuwa na mkataba nae,” alisema.
Tayari Yanga imesajili wachezaji 12, watano kutoka Tanzania na saba wa kimataifa akiwemo Mzambia, Richanel Kiteko ambaye hajaonekana kwa wananchi hao tangu atambulishwe dirisha kubwa na Lidya Maximillan anayekipiga kikosi cha JKT Queens.
Msimu huu kikosi hicho kimeanza vibaya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kwa kupoteza pointi tisa, ikianza dhidi ya watani zao Simba Queens kwa kufungwa mabao 3-1, Ceasiaa Queens 1-0 kisha JKT kwa mabao 3-1, yote ikichezwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi.