Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyota Simba, Yanga huumizwa makusudi

Moloko Gh Nyota wa Yanga, Jesus Moloko alifanyiwa upasuaji wiki chache zilizopita

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: Ippmedia

Hivi karibuni alisikika Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi akionesha kusikitishwa na wingi wa majeruhi katika kikosi chake huku akiwataka waamuzi wanaochezesha michezo ya Ligii Kuu Tanzania Bara kulinda wachezaji

Ilikuwa ni baada ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Geita Gold Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Nabi alisema waamuzi wa Tanzania wanatakiwa wawe na mamlaka ya kuwalinda wachezaji, si wa Yanga tu, bali wa timu zote ili zisizalishe majeruhi bila sababu yoyote.

Akasema mfano Yanga ina idadi kubwa ya wachezaji majeruhi ambao mara nyingi wanapatikana wakati wa kugongana na wachezaji wa timu pinzani.

"Tunajua ligi ni ngumu na kila timu inahitaji pointi tatu, lakini waamuzi wanatakiwa wawalinde wachezaji na siyo wa Yanga tu, bali hata wa timu nyingine ili zisizalishe majeruhi wengi bila sababu.

Hii si kwa Yanga tu, bali hata Pablo Franco naye amekuwa akilia na tatizo hilo la wachezaji wake kupaniwa na kufanyiwa rafu zisizo za kistaarabu na kimpira.

Ni kweli ukiangalia mpaka sasa klabu kubwa za Simba na Yanga ndizo zina majeruhi wengi kuliko timu zote kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara. Kuna wakati zilifikisha mpaka majeruhi 10.

Nafikiri kama idadi hiyo ingekua kwa timu zingine ukiondoa hizo, zingekuwa na hali mbaya zaidi kwa sababu huwa hazina vikosi vipana.

Kwa uchunguzi wangu mdogo na mfupi tu, nimegundua timu yoyote ikicheza na Simba na Yanga zinachofanya si kwenda kupambana soka, ufundi na mifumo, bali kwa asilimia kubwa ni matumizi ya nguvu.

Nadhani wamekariri ukicheza na timu hizi ili kuzidhibiti, basi matumizi ya nguvu yanahitajika zaidi. Na wakafanya rafu nyingi ambazo asilimia kubwa ni za kadi nyekundu. Mara nyingi rafu zile kwa sisi tunaotazama soka Ulaya, ni moja kwa moja kadi nyekundu hakuna mjadala.

Kule watu wametoa fedha zao za viingilio na makampuni yamewekeza kwa ajili ya kuona burudani, vipaji vya wachezaji na uwezo, siyo rafu za kipuuzi. Ulaya ukiruka miguu miwili na hata ukimkosa mlengwa unaweza kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa sababu dhamira yako ilikuwa ni kumvunja mwenzako, lakini huku itaangaliwa kama miguu ilimpata au ilimkosa.

Wachezaji wengi wa timu zinazoitwa au kujiita ndogo ukiangalia kwa makini wamekuwa na rafu nyingi za ajabu, si za kistaarabu, za kihusda na kutaka hata kumaliza muda wa wachezaji hao kwa kuwaumiza au kuwavunja.

Hawajali na hawana ile kauli mbiu ya kumlinda mwenzako na wengine wao wanavyocheza ni kama wana visasi nao, au kama wanaowaonea donge kwa sababu wanachezea timu kubwa, hivyo wanataka kuwakomoa.

Wanakuwa na bahati kwa sababu hata wakicheza rafu zao za kupuuzi, si mara nyingi zinarekodiwa na kurudiwarudiwa kwenye mitandao ya kijamii, kama zile ambazo wanacheza wachezaji wa Simba au Yanga.

Bahati mbaya walionayo wachezaji wa Simba au Yanga ambao wanachezewa sana rafu, wao wakirudishia tu video zao zinakuwa zinaonyeshwa sana kwenye mitandao ya kijamii kwa utamaduni ule ule wa U-Simba na U-Yanga kushinikiza wafungiwe, lakini kwa wachezaji wa timu nyingine wanaweza kucheza rafu mbaya sana, lakini isiwe habari ya mjini.

Bahati mbaya zaidi waamuzi nao wametekwa na hilo. Sijui kwa kuwaonea huruma au vipi, wamekuwa wakiwaachia kucheza rafu nyingi bila kuchukua hatua stahiki.

Mchezaji mmoja anaweza kucheza rafu mbaya za kadi nyekundu hata nne, halafu akapata njano moja tu. Na ukiangalia wale wanaopata kadi nyekundu ni wale ambao wana kadi za njano, halafu wanacheza rafu nyingine mbaya. Nadhani waamuzi wanaogopa kuonekana wanazionea timu hizo zinazoitwa ndogo.

Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kuwa Simba na Yanga zina majeruhi wengi kwa sababu ya kutokuwa na mazoezi mazuri ya utimamu wa mwili. Nilichogundua ni kuchezewa sana rafu mbaya ambazo waamuzi wamekuwa hawachukui hatua stahiki.

Chanzo: Ippmedia