Baada ya mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele kushinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu ya mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na mabao saba, kiungo wa AS Real Bamako, Ibrahim Sidibe amesifu uwezo wa Mkongomani huyo.
Mayele aliifunga Bamako nje ndani wakati timu hizo zilipokutana katika Kundi D la Shirikisho, ambako kule Mali alifunga moja katika sare ya 1-1, na kisha akaja kuwafunga jingine moja Dar es Salaam wakati Yanga ikishinda 2-0. Bao jingine la Yanga lilifungwa na Jesus Moloko, huku Yanick Bangala akikosa penalti katika dakika ya 68.
Sidibe, ambaye timu yake ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi tano Kundi D huku Yanga ikimaliza kinara kwa pointi 13, amesema Mayele sio mtu wa mchezo.
"Wachezaji wote wa Yanga wamefanya vizuri msimu huu lakini katika mafanikio yao huwezi kuacha jina la mtu kama Mayele kwa sababu katika michezo mingi na migumu aliiamua yeye hivyo kwangu nampa pongezi," alisema.
Aidha, Sidibe aliongeza kwa alichofanya Mayele ni dhahiri timu nyingi kubwa zitamuhitaji hivyo ni jukumu la viongozi wao kuhakikisha wanamboreshea mkataba wake ili aendelee kusalia kwenye timu.
"Unapofanya vizuri hasa michezo hii ya kimataifa ni wazi unazidi kuuza jina lako na kwake ndicho ambacho pia nakiona, amefanya kazi kubwa hivyo jukumu litabaki kwake kuamua kama atabaki au atatafuta changamoto sehemu nyingine."
Mayele pia yuko kwenye nafasi nzuri ya kuchukua tuzo ya ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwani anaongoza akiwa na mabao 16.