Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyota Mutale, Mukwala watema cheche Simba

Mukwala Mutale 8 01 At 17.jpeg Nyota Mutale, Mukwala watema cheche Simba

Thu, 1 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati tiketi za jukwaa la mzunguko kwa ajili ya kuingia katika kilele cha tamasha la Simba Day Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa lililopewa kaulimbiu ya 'Ubaya Ubwela, wachezaji wapya Joshua Mutale na Steven Mukwala wamewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa wataishuhudia timu tofauti na ile waliyoiona msimu uliopita.

Nyota hao walisema msimu huu Simba ina wachezaji wanaocheza soka safi na la kuburudisha huku wakiwa na uwezo mkubwa, ari na nguvu, pamoja na benchi bora la ufundi lenye mbinu nzuri za ufundishaji chini ya Kocha Fadlu Davids. Wachezaji hao wamewataka mashabiki kwenda uwanjani kuona soka safi la burudani, pamoja na ushindi usiokuwa na shaka.

Kikosi hicho kimewasili jana jijini Dar es Salaam kutoka nchini Misri ambako kiliweka kambi kwa takriban wiki tatu kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano.

Mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Mukwala, alisema mechi yao ya mwisho ilieleza kila kitu, kwani walicheza jinsi ambavyo kocha wao siku zote alikuwa anataka wacheze na waliweza kufanikiwa kutokana na kuwa fiti tofauti na michezo miwili iliyopita.

"Mechi ya mwisho ilieleza kila kitu, ilikuwa ngumu kuliko zote tulizocheza, timu kutoka Saudi Arabia haikuwa rahisi, lakini tulipambana na kuweza kushinda, nawaahidi wanachama na mashabiki wa Simba wataona mchezo mzuri sana kila tutakapocheza, wataona kitu tofauti na walichokiona msimu uliopita, tunajua nini wanataka na tuwape hicho wanachohitaji," alisema mshambuliaji huyo raia wa Uganda aliyesajiliwa kutoka klabu ya Asante Kotoko ya Ghana.

Katika mechi ya mwisho, Jumatatu usiku, Simba ilicheza dhidi ya Al Adalah ya Saudi Arabia, Uwanja wa New Suez Canal nchini humo na kushinda mabao 2-1, ambao yalifungwa na Mukwala pamoja na Mutale.

Aidha, Mutale kwa upande wake alisema kwa sasa wapo katika utimamu wa miili kwa asilimia 90 na ndicho kilichofanya wapate ushindi katika mchezo wao wa mwisho huku akisema sasa wapo tayari kwa ajili ya Simba Day pamoja na msimu mpya wa mashindano, licha ya kwamba Kocha Fadlu bado anafanya marekebisho ya hapa na pale.

"Kwa sasa tupo kwenye asilimia 90 ya kiwango cha utimamu wa mwili, mazoezi yalikuwa mazuri na magumu, mchezo wetu wa tatu umeonyesha tayari tupo kamili, tulikuwa tunakaba wote, tunakimbia kwa kasi, kukaa kwenye maeneo sahihi kwa wakati sahihi na hata wakati mwingine tulikuwa tunapigiana pasi ndefu kila upande wa uwanja haraka haraka huku tukikimbilia eneo la adui kiasi cha kuwachanganya wapinzani na hata bao la pili nililofunga lilipatikana kwa mtindo huo.

Nadhani sasa tupo tayari kwa Simba Day na msimu mpya, najua mashabiki wetu watatupokea vizuri kutokana na hiki ambacho tunawapelekea uwanjani," alisema Mutale, winga mpya aliyesajiliwa kutoka Power Dynamos ya Zambia.

Wakati hayo yakiendelea kuelekea kwenye Tamasha la Simba Day ambapo timu hiyo itacheza na APR ya Rwanda, tiketi za mzunguko wa pili zimemalizika, huku zilizosalia ni za VIP B, VIP C na rangi ya machungwa ambazo nazo zimebaki chache.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amewataka mashabiki kununua tiketi kwenye majukwaa hayo, kwani mbali na mzunguko, tiketi za Platnum na VIP A, nazo zimemalizika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live