Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyota 10 wa Tembo Warriors walioula Ulaya

Tembo Warriors Ulayaaa Nyota 10 wa Tembo Warriors walioula Ulaya

Tue, 8 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Viwango bora kabisa vya wachezaji wa Kitanzania kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Uturuki mwaka huu kwa walemavu ndio siri ya mafanikio ya mastaa hao.

Viwango hivyo ndio vilivyotajwa kuzivutia klabu kubwa barani Ulaya kupigana vikumbo kuwania saini za nyota hao ambao walikuwa gumzo katika fainali za Kombe la Dunia wakiwa na Timu ya Taifa ‘Tembo Warriors’.

Kama ambavyo ilikuwa kwa Timu ya Wanawake Chini ya Umiri wa Miaka 17 ‘Serengeti Girls’ wiki chache zilizopita kule India, Tembo Warriors ilionyesha dunia kuwa Tanzania ni taifa la soka Afrika.

Timu hiyo ilipenya kutoka Kundi E mbele ya Hispania ambayo iliburuza mkia na kwenda hatua ya 16 bora hadi robo fainali.

Ilikuwa michezo mitano ya nguvu kwa Tembo Warriors kuanzia hatua ya makundi hadi robo fainali ambapo ilitolewa na Haiti kwa kufungwa mabao 4-1.

Hadi kufikia hatua hiyo ilitosha kuwafanya maskauti ambao walikuwa wakifutilia vipaji kwenye mashindano hayo kuulizia upatikanaji wa wachezaji 10 wa Kitanzania ambao viwango vyao viliwapagawisha.

Wachezaji hao ni Alfan Kyanga, Juma kidevu, Habibu Likoike, Shedrack Hebron na Abdulkarim Amiri.

Wengine ni Salimu Bakari, Ramadhan Chomelo, Frank Ngailo, Mudrick Azzan na Richard Swai ambao kwa sasa kila mmoja ameanza maisha mapya ya kuchezwa soka la kulipwa Ulaya baada ya usajili wao kukamilika katika klabu tano tofauti.

Hakuna mtu aliyetarajia kama mastaa hao watabadili maisha na kuweza kugombaniwa na timu za mchezo wa soka kama ilivyokuwa.

Lakini kwa sasa mastaa hao wamekuwa na maisha mengine kabisa kutokana na faida ya kucheza mchezo huo wa soka la walemavu.

Kikubwa ni kwamba hawakukata tamaa baada ya kupata ulemavu na kujishughulisha na soka na kuweza kuitumia vizuri fursa waliyoipata na sasa wameonekana na katika timu ambazo zitakuwa na maslahi mazuri kwa upande wao.

Mmoja wa wadau wetu wa Nje ya Bongo, Juma Nassoro ambaye yupo Uturuki kwa miaka sita sasa, anaeleza namna ambavyo wachezaji hao walivyofanya makubwa kwenye fainali hizo ambazo zilikuwa zikifanyika kwa mara 17 chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani kwa Walemavu (WAFF).

Mdau huyo anasema hakutarajia kile alichokiona kutoka kwa Watanzania hao. Nassoro ambaye aliishuhudia Tembo Warriors ikishiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza alisema hakutarajia kuwaona vijana hao wa Kitanzania wakionyesha ushindani wa kiwango kile, “Ilikuwa ni maajabu kwakweli, binafsi nilienda kwa ajili ya kukutana tu na watu wa nyumbani, sikuwa na imani kabisa kuwa tuna timu nzuri ya kushindana na mataifa mengine.

“Nilikuwa uwanjani tangu siku ya kwanza ambapo tulicheza dhidi ya Hispania, kwa kweli nilishangazwa sana na kiwango cha timu yetu, kitendo cha kutoka sare ya ya bila kufungana (0-0) na wababe hao wa soka la Ulaya niliona tuna kitu maana wachezaji wetu walicheza kwenye kiwango kizuri, tulicheza vizuri sana.

“Mchezo uliofuata tulifungwa na Poland (3-0), yalikuwa ni matokeo ambayo kila mmoja wetu yalimuumiza, lakini tulijipa moyo na kuamini kuwa tutafanya vizuri kwenye mchezo wetu wa mwisho maana ni timu tatu zilikuwa zikitakiwa kusonga mbele,” anasimulia Mtanzania huyo ambaye ni mzaliwa wa Morogoro.

Anaendelea kwa kusema, “Sapoti yetu mashabiki ilikuwa kubwa kwa timu na tukafanikiwa kuifunga Uzbekistan (2-0) na kuingia hatua ya 16 bora, kiukweli kila mchezaji alikuwa akifanya vizuri, wachezaji wetu walikuwa kivutio kwani wengi walikuwa vijana tofauti na wa mataifa mengine.”

Yapi malisho ya wachezaji hao ambao waliwatoa kimasomaso Watanzania kabla ya Serengeti Girls, hizi ndio klabu zao mpya na wachache kati yao waliongea na safu hii na kueleza vile ambavyo mapambano mapya yameanza huko Uturuki.

SISLI YEDITEPE

Hii ndio timu yenye wachezaji wengi wa Kitanzania, Sisli Yeditepe imewanasa wachezaji wanne ambao ni Alfan, Juma, Habibu na Shedrack.

Kwa niaba ya wenzake, Shedrack anasema, “Ni jambo zuri kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa Ulaya, ni nafasi adhimu ambayo tumepata.

“Tuna imani kuwa tutakuwa na wakati mzuri, kuna uzoefu ambao tuliupata kwenye Kombe la Dunia kwa hiyo unaweza kutusaidia kufanya vizuri kwenye ligi.”

KAYSERISPOR

Abdulkarim na Salimu wao ni mali ya klabu ya Kayserispor ambayo mbali na kuwa na timu ya walemavu wanayo ya kawaida kwa wanaume na wanawake.

Akizungumzia maisha ya Uturuki, Salimu anasema, “Unapotoka sehemu moja kwenda nyingine lazima kuwe na mabadiliko, huwa inahitaji muda kuendana nayo. Mpira ni uleule ila kila sehemu wana namna ya uchezaji wao, tumejiandaa kukabiliana na changamoto mpya naamini kuwa zitatuimarisha na kuwa bora zaidi.”

Kwa upande wake, Abdulkarim anashauku ya kuanza kukiwasha kwenye Ligi ya Uturuki, “Nilijipa muda wa kusoma mpira wao, nimeona kuwa ligi yao ni kubwa na ina ushindani, hivyo inahitaji nguvu na akili ya mpira.”

KONYA

Ni Ramadhan Chomelo aliyejiunga na klabu ya Konya naye anasema: “Najua kuwa kuna mechi ambazo zitakuwa zikinikutanisha na ndugu zangu ambao tumekuwa tukishirikiana kwenye timu yetu ya taifa, itapendeza kuonana nao na kuongea mawili matatu.

“Natamani kuwa mshindi siku zote, najua kuwa inahitaji muda kuthibitisha hilo, nimedhamiria kuonyesha kipaji changu katika hatua nyingine,” anasema.

IZMIR BBSK

Frank Ngailo ambaye yupo zake kwenye Klabu ya Izmir BBSK anasema: “Hii fursa kwetu, ni ndoto ambayo naamini kila mmoja wetu alikuwa akiiota, sidhani kama kuna mmoja wetu alikuwa na uhakika kuwa siku moja atacheza soka la kulipwa kwenye taifa kubwa kama Uturuki na ikizingatiwa mpira wetu sio maarufu nyumbani.

“Watu wengi wamekuwa wakiuzungumzia na kuupa uzito pamoja na kufuatilia mpira ila upande wa wenzetu, tulipambana ili kuonyesha kuwa na sisi tunaweza na hatimaye milango imefunguka zaidi na tumepata nafasi ya kuendelea kuonyesha zaidi vipaji vyetu,” anasema nyota huyo.

MERSIN

Mudrick Azzan na Richard Swai wamejiunga na Mersin na wapo tayari kukabiliana na changamoto mpya ya namba.

“Kabla ya kuja huku binafsi nilikuwa na programu za mazoezi kwa ajili ya kujiweka sawa, najua kuwa inahitaji kazi ya ziada ili kupata nafasi ya kucheza lakini hilo haliwezi kunitatiza kwani najua namna ya kumshawishi mwalimu kunipa nafasi ya kufanya vizuri mazoezini,” anasema Mudirck.

Kwa upande wake, Richard anasema:

“Sina presha na changamoto ya namba, cha kwanza ambacho nakiona ambacho nahitaji ni muda wa kuzoeana na wachezaji wenzangu baada ya hapo itakuwa rahisi kwangu kujua namna ya kucheza nao.”

Chanzo: Mwanaspoti