Baada ya kusota Dar es Salaam kwa takribani wiki mbili, hatimaye Majimaji inatarajia kusafiri kurejea nyumbani mjini Songea kesho Februari 28 alfajiri baada ya beki wa Simba, Erasto Nyoni kutoa nauli na kumaliza deni lililokuwa limebaki hotelini.
Majimaji ilikuwa imekwama jijini humo tangu ilipomaliza mechi yake dhidi ya African Lyon kabla ya kucheza tena mchezo wa juzi dhidi ya Dar City kutokana na kukosa pesa ya nauli na deni katika nyumba ya kulala wageni.
Kwa muda mrefu timu hiyo iliyowahi kucheza Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja na kushiriki first league kwa sasa, ilikuwa ikitembeza bakuli kuweza kupata fedha za kulipa deni na nauli.
Mapema wadau na mashabiki wa timu hiyo wa kabila la wangoni waishio Dar es Salaam walianza kuichangia Sh 180,000 kabla ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuchangia Sh 500,000 lakini haikutosha na kuifanya timu hiyo kuendelea kubaki jijini humo.
Leo jioni Nyoni alifika kambini ilipo timu hiyo na kulipa takribani Sh1 milioni ikiwa ni malipo ya deni lililokuwa linadaiwa pamoja na nauli kwa wachezaji na viongozi 10 waliokuwa wamebaki Dar es Salaam.
"Katika pesa ambayo tulipokea awali tulisafirisha baadhi ya wachezaji sita hivyo na matumizi mengine tukabaki wengine 10 hapa Dar es Salaam, lakini tunashukuru sana Nyoni amekuja na kulipa kila kitu na kesho tunasafiri kurudi nyumbani" amesema Catherine Masasi ambaye ni kiongozi wa timu hiyo.