Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyoni? Achaneni naye kabisa!

Nyoni (600 X 400) Erasto Nyoni

Fri, 24 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Hadithi ya kiraka wa Simba, Erasto Nyoni inawasisimua wadau wanaomtazama kama nembo inayosomwa na vijana wanaokuja nyuma yake kupata siri ya kudumu muda mrefu.

Simba ina mpango wa kuwatoa mastaa wake watano kwa mkopo na kati ya majina hayo lipo la Nyoni, jambo ambalo limewashtua wadau na kutoa neno kwa viongozi wa Azam na Simba alizozitumikia.

Azam FC aliitumikia miaka saba (2010-17) akitokea Vital’O ya Burundi kisha akajiunga na Simba 2017-2021 ambapo zinaenea tetesi kutoka ndani ya timu kwamba anatolewa kwa mkopo.

Straika wa zamani wa Azam FC, Philip Alando aliyewahi kucheza na Nyoni katika kikosi hicho kabla ya kuwa meneja wake, alishangazwa na habari za kutolewa kwa mkopo.

Alando alisema Nyoni licha ya umri wake kiwango chake ni kilekile kinachotokana na nidhamu anayoionyesha kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi.

“Ningekuwa kiongozi wa timu yoyote ningemsajili Nyoni kwanza ana faida tatu, kucheza nafasi zaidi ya moja, uzoefu na nidhamu. Nimecheza naye namjua namna anavyouheshimu mpira. Ndio maana wanakuja vijana wanapotea, wakongwe wenzake wanapotea, lakini yeye bado yupo,” alisema.

“Kama kweli watamuondoa siyo kwa kushuka kiwango chake, labda kocha ana mpango wa kuwa na wachezaji chipukizi ambao ningekuwa mimi ningemuacha ili waweze kujifunza kupitia yeye, kwa sababu ana masomo mengi iwe kwenye klabu alizozitumikia ama Stars (Taifa Stars),” alisema.

Alisema jambo lingine la tofauti alilonalo Nyoni siyo mchezaji mwenye majungu bali anapenda kuleta furaha mbele ya wenzake.

Kocha wa zamani wa Gwambina, Athuman Bilal ‘Bilo’ aliyesema bado anamuona Nyoni ana nafasi ya kuendelea kubaki Simba, kutokana na aina ya uchezaji wake. “Kuwa na mchezaji anayeweza kucheza nafasi zaidi ya moja ni faida kwa timu. Pia ana nidhamu ya kulinda kiwango na atakuwa kiongozi wa chipukizi kuwaelekeza zaidi majukumu uwanjani na kwa ulijendari wake anastahili aagwe kwa heshima,” alisema Bilo.

Kipa wa zamani wa Simba, Steven Nemes alisema: “Mchezaji anapaswa kuhukumiwa kwa anachoonyesha uwanjani na si nje ya hapo, ingawa siwezi kusema mengi ila Nyoni ni mchezaji wa mfano zaidi ya wengine ni nadra kuwa nao wa aina yake.”

Kocha wa Kagera B, George Kavila alisema bado anaamini uwezo wa Nyoni unatakiwa kuendelea kuihudumia Simba.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz