Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyeye akacha safari kisa ndege

Nyeye Akacha Safari Kisa Ndege.jpeg Nyeye akacha safari kisa ndege

Sun, 10 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Usafiri wa anga unapendwa na wengi kutokana na urahisi wake wa kufika maeneo ya mbali kwa muda mfupi. Kitoka nchi moja kwenda nyingine, au mkoa mmoja au mwingine kwa njia ya basi utatumia muda mrefu tofauti na ndege.

Hata hivyo, sio kila mtu anaupenda usafiri huo, Dennis Bergkamp, nyota wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Uholanzi, ni mmoja wa wachezaji waliokuwa hawapandi ndege.

Hata kama kuna mechi muhimu vipi, atatangulia na usafiri mwingine lakini sio kupanda ndege, au asiende kabisa kwenye mchezo huo.

Hapa nchini nyota wa mkongwe wa Namungo FC, Hamis Nyenye ni kati ya wachezaji waliopitia tatizo hilo la woga wa kupanda ndege.

Wapo wanaopanda lakini hawazoei mazingira ya kuwa angani, watatua salama lakini wakikumbuka hawana hamu, ila kwa Nyenye anamtaja mama yake ndiye aliyesababisha kupanda ndege baada ya kuwa na woga na hadi kufikia kuikacha timu yake ilipokuwa ikisafiri kwenda kucheza mchezo wa kimataifa nje ya nchi akihofia kupanda ndege.

Akifanyiwa mahojiano na Mwanaspoti, kiungo huyo mkabaji wa Namungo FC anasema, “Katika tukio ambalo sitoweza kulisahau kwenye maisha yangu ni kitendo cha kushindwa kusafiri na timu kwenda kushiriki mashindano ya kimataifa nikihofia kupanda ndege.

“Msimu wa 2021 nikiwa na Namungo, nilibaki Dar es Salaam kutokana na kukosa ujasiri wa kupanda ndege. Timu ilikuwa ikienda Angola kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CD de Agosto.”

Nyenye anasema hata hivyo, anashukuru Mungu mchezo huo uliopangwa ufanyike Februari 14, 2021, haukufanyika kutokana na sababu za Uviko 19 na wachezaji wengi walikutwa na maambukizi.

Hata hivyo, anasema anamshukuru mama yake mzazi kwa kumjengea imani na ujasiri na sasa anapanda ngege kama kawaida ingawa bado hajawa na ujasiri mkubwa kama wengine.

ALIANZIA SOKA MTAANI

Mastaa wengi wa soka, wamepambana sana hadi kufikia kucheza soka la daraja la juu (ligi kuu). Hata hivyo, kwake mambo hayakuwa magumu kwani alitokea kitaani hadi ligi kuu kama anavyothibitisha mwenyewe.

“Nimeanza kucheza mtaani kabla sijatua Namungo, njia yangu haikuwa ngumu sana kwani nimeanza kucheza ligi ya ushindani baada ya kutoka mtaani;

“Namungo ndiyo timu yangu ya kwanza kubwa kuchezea na ndiyo iliyonipa jina kubwa hadi sasa kwani nimeanza kucheza tangu ikiwa daraja la chini hadi sasa inashiriki Ligi Kuu Bara.”

KUMBE ALIKUWA KIPA

Sio kila mchezaji anayecheza nafasi aliyopo sasa alianza kucheza hapo kuna wengine walianza kukaa langoni kama kipa na sasa wamekuwa washambuliaji na wengine viungo kama ilivyo kwa Nyeye.

“Wakati naanza kucheza nilianza nafasi ya kipa, lakini kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda nikajikuta nabadili nafasi na kujikuta natamani kucheza eneo lingine tofauti na kocha niliyekuwa chini yake kipindi hicho alikubali na kunipanga nafasi tofauti;

“Sikumbuki jina la kocha nilikuwa na umri mdogo ninachokumbuka ni maneno yake tu akiniambia kutokana na kimo changu sipaswi kucheza langoni (Kipa) akiniambia nina kimo kifupi na kunipanga katikati (kiungo) nafasi ambayo naicheza hadi sasa,” anasema.

Nyenye ambaye amekiri kuupa kipaumbele mpira kuliko shule anasema anafurahia kucheza nafasi ya kiungo kwani anakuwa anafanya mambo mengi uwanjani tofauti na angekuwa kipa.

MIAKA SABA BILA TAJI

Wakati kuna mastaa wanaocheza ligi kuu wametwaa mataji zaidi ya matano kama ilivyo kwa Jonas Mkude unaambiwa kwa upande wa kiungo wa Namungo, Nyenye ndani ya misimu saba ndani ya timu hiyo hajawahi kunyanyua kwapa.

“Ndani ya miaka saba ambayo nimedumu ndani ya kikosi cha Namungo mafanikio makubwa ambayo nimeyapata ni kushiriki mashindano ya kimataifa baada ya kumaliza nafasi ya nne msimu wa 2021;

“Ndoto yangu ni kupata nafasi ya kunyanyua kwapa nikiwa ndani ya timu hii ambayo nimeichezea kwa misimu saba nikiwa na nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kwenye kila kocha aliyepita kikosini hapa,” anasema Nyenye.

AUCHO VIATU, CHENGA

Ukitaja kiungo fundi wa ukabaji ndani ya Yanga huwezi kusita kutaja jina la Khalid Aucho ambaye ni panga pangua kikosi cha kwanza ndani ya timu hiyo tangu amesajiliwa hilo pia limethibitishwa na kiungo wa Namungo ambaye amemtaja mchezaji huyo kuwa ni bora eneo hilo.

“Viungo wanaocheza eneo la ukabaji navutiwa nao wengi kwa upande wa wazawa namkubali Jonas Mkude (Yanga) na Yusuf Kagoma ambaye anakipiga Singida Big Stars ni wachezaji wazuri wanajua kucheza na ni bora wakiwa na mpira hata timu ikipoteza unaona wakiangaika uwanjani;

“Lakini kwa upande wa wachezaji wageni namkubali Aucho anayecheza Yanga ni kiungo ambaye ana mambo mengi uwanjani anacheza kwa akili ni ngumu kumwonyesha mwamuzi madhambi yake;

“Aucho anakupiga chenga anaipa timu yake matokeo na viatu anakupiga vilevile ni mchezaji ambaye anacheza rafu kwa akili tofauti na wachezaji wengine,” anasema Nyenye.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live