Siku moja Makamu wa Rais, Philip Mpango alikuwa akiondoka nchini. Pale uwanja wa ndege alikuwa akiagwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Makamu wa Rais akaegesha mkono wake wa kulia katika mkono wa kushoto kama vile anataka kutetema. Staili ya Fiston Mayele apokufunga bao.
Makamu wa Rais ni Yanga wa kutupwa wakati Waziri Mkuu ni Simba wa kulia. Hapo walikuwa wakitambiana. Mayele angepata wapi heshima hii? Nimewaza tu kwa namna ambavyo Wacongo wanapenda sifa, zitahitajika pesa nyingi kumng’oa Mayele Yanga wakati huu dirisha la uhamisho likiwa wazi.
Nasikia tu kwamba kuna ofa za Mayele mkononi mwake. Huwa najaribu kuitazama filamu hii ya Mayele. Jinsi ambavyo anatetemekewa kila mahala nchi hii najaribu kuifikiria filamu ya kuondoka kwake itakavyokuwa. Hasa kwa muda huu.
Ni kweli ana mkataba wa mwaka mmoja na Yanga ambao Waarabu wanaweza kupita nayo kama upepo. Pesa sio kila kitu katika maisha ya mwanadamu. Mayele yupo katikati ya ubora wake wa kuitetemesha nchi.
Sasa hivi Yanga wapo likizo lakini Mayele anazurura hapa na pale hapa hapa nchini. Ana pesa mfukoni lakini hajakwenda mbali na Tanzania. Nadhani anasikia raha namna anavyoishi nchini. Nani asingesikia raha. Katika likizo yake hii ameamua kucheza bonanza nchini.
Anasikia raha kuwa nchini. Majuzi alikuwa Zanzibar katika mechi ya hisani ya Fei Toto. Akaondolewa na Polisi kutokana na umati wa watu kutamani kumgusa. Majuzi tena akaenda Morogoro kucheza pambano la hisani lililoandaliwa na wachezaji wenzake wa Yanga, Dickson Job na Shomari Kibwana.
Kwa sasa kila mtu anataka kumuona Mayele, kila mtu anamkubali Mayele, hata mashabiki wa timu pinzani wanamkubali Mayele. Nchi inatetema. Ipo ile siku ambayo nilimkuta Mlimani City huku maelfu ya mashabiki wakileta fujo kujaribu kumtazama. Korido za Mlimani City zilikuwa hazipitiki. Kisa Mayele?
Hiki ni kipimo kikubwa cha kupima weledi wa mchezaji katika maamuzi yake. Ni wakati ambapo mchezaji anajikuta amekwama kuchagua kati ya maisha yake au upendo dhidi ya watu wake. kuchagua kati ya pesa dhidi ya upendo anaopewa.
Hapa nchini tumewahi kuwa na wachezaji wa aina ya Mayele. Hawakuwahi kucheza nje ya nchi kwa sababu walikuwa wanafikiria namna ya kuziacha sifa kama hizi na kwenda kujaribu maisha nje ya nchi. Haishangazi kuona kwamba wengi waliharibu maisha yao hapa hapa licha ya kutakiwa na klabu mbalimbali za nje.
Halafu kuna wachezaji wetu ambao waliwahi kuondoka nchini wakiwa katika ubora kama wa Mayele na wakiimbwa kama Mayele. Hawa walipoenda nje ya nchi akili zao zote waliziacha Dar es salaam. walikuwa wanatamani huko wanakoenda washindwe ili warudi nchini.
Na kweli, mchezaji alikuwa anaondoka kwa mbwembwe anajiunga na timu fulani au anakwenda kufanya majaribio na timu fulani lakini ndani ya miezi michache unakutana naye mitaa ya Posta Mpya akiwa amezungukwa na kundi la mashabiki. Baadaye unasikia yupo hapa hapa ameanza mazoezi na timu yake ya zamani akisubiri msimu mpya.
Tusiwalaumu sana wachezaji wetu pekee. Najaribu kupima pia akili ya Mayele. Jinsi anavyopendwa nchini. Atakubali kuingia katika mkumbo wa wachezaji wetu. Sitaki kubashiri sana lakini hapo hapo nakumbuka kwamba hata hapa alipo tayari Mayele yupo nje ya nchi yake.
Anaweza kuamua kuamua kubakia au kuondoka. Akili ya kwanza inaniambia kwamba Mayele atabakia kwa sababu ya sifa anazopewa. Ufalme ambao anatembea nao kila kona ya nchi hii unaweza kumshawishi abakie hasa ukizingatia kwamba yeye ni Mcongo.
Wacongo ni watu wanaopenda kuabudiwa. Wanaopendwa kupendwa. Kuanzia kwa matajiri wao, Wanamuziki wao, wachezaji wao, na hata Wanasiasa wao. Wanapendwa kupendwa na kuabudiwa. Mayele hawezi kuwa tofauti sana ingawa kitu kikubwa kinachomtofautisha na Wacongo wengine ni kwamba hana maringo wala majivuno.
Achilia mbali pale alipopandwa na hasira na kujaribu kugombana na kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin katika pambano la watani wa jadi, Mayele hajawahi kuhusika katika matatizo mengine ya kikorofi ndani na nje ya uwanja.
Kitu ambacho nakifahamu ni kwamba hata kama Mayele ataamua kubakia hapa nchini basi atatumia nafasi ya umaarufu wake kutengeneza pesa kwa kigezo cha mkataba wenye ubora. Hapa ndipo wachezaji wetu wa zamani na wa sasa walikosea
Wachezaji wengi wa zamani wazawa ambao walipendwa na klabu hizi walikuwa hawatingishi kwa ajili ya kusaka maslahi zaidi. waligeuzwa kuwa kama mashabiki wa timu hizi na wakasahau weledi wao. Kila mchezaji mkubwa mzawa ilikuwa inajulikana kwamba alikuwa klabuni kwa ajili ya kutetea maslahi ya klabu.
Kwa mfano, Edibily Lunyamila aliichezea Yanga kama shabiki zaidi. Hakukuwa na nyakati ambazo alionekana kama vile angeweza kusaka maslahi zaidi katika klabu nyingine kubwa nchini kama Simba. Labda pale alipokwenda kuibukia Malindi ya Zanzibar.
Hata hivyo hawa akina Mayele ni wageni. Anaweza kuamua kunogewa na sifa za nchini, akaamua kubakia kwa mshahara wa shilingi milioni 20 huku akikataa mshahara wa shilingi milioni 30 za Waarabu. Lakini hawezi kubakia nchini kwa mshahara wa shilingi milioni 10.
Hawa wachezaji wamekuja kutuamsha katika suala la maslahi. Walianza akina Emmanuel Okwi wakaja akina Clatous Chota Chama. Muda wowote walionekana wangeweza kuvuka boda kwenda kwa mtani kama wangeshawishiwa na pesa nyingi.
Nasubiri kujua Mayele anaweza kuamua nini kwa sasa. Sawa Yanga wana mkataba naye lakini mkataba ni kitu kinachoweza kuvunjika kama mchezaji akiamua kuondoka. Lakini pia ni kitu ambacho kinaweza kuongezwa kama akiamua kubaki.