KUKOSA KOMBE
Simba wameanza msimu huu vibaya baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga kwneye mchezo wa Ngao ya Hisani, Yanga wao wameanza msimu vizuri kwa kuchukua taji hilo la kwanza kushindaniwa.
Simba walilikosa kombe hilo la kwanza walilokuwa wakilitetea baada ya kulibeba msimu uliopita wakiwafunga Namungo na ilikuwa bahati mbaya kwao kwani walikuwa na malengo ya kulibeba.
Baada ya kushindwa kuchukua taji hilo malengo makubwa kwao yalihamia Ligi ya Mabingwa Afrika kufuzu hatua ya makundi ingawa nako walishinda na kujikuta wakiangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa bao 3-1 na Jwangen Galax ya Botswana.
USAJILI
Halikuwa jambo la kutegemewa na wengi msimu huu baada ya kusajili wachezaji 12, kutoka maeneo tofauti.
Kutokana na ubora wa kikosi chao msimu uliopita walitakiwa kufanya maingizo machache kwa kuangalia mapungufu machache ya kikosi kama beki wa kati, kiungo mshambuliaji (namba nane) na winga mmoja aliyekamilika.
Hata kuondoka kwa Clatous Chama na Luis Miquissone, hawakutakiwa kusajili idadi kubwa ya wachezaji kama sasa.
Mbali na usajili wa wachezaji hao, wachache ndio wamefanya vizuri ila wengi wao wameshindwa kupenya hata kikosi cha kwanza jambo ambalo limechangia kushindwa kuanza vizuri kwa haraka na kucheza kwa maelewano.
MO KUJIUZULU
Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kwenye uongozi wa Simba, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji alijiondoa katika nafasi hiyo na kumteua Salim Abdallah ‘Try Again’ kushika nafasi hiyo nyeti.
Wakati anatangaza kujitoa kwenye nafasi hiyo alisea atabaki kuwa mwanahisa ingawa mchakato huo wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji haujakamilika.
Tangu kujiondoa kwake kumekuwa na baadhi ya dalili kwenye maeneo tofauti kuwa pesa aliyokuwa anaitoa ni tofauti na ilivyo wakati huu.
MECHI ZA LIGI
Chungu nyingine ambayo Simba wanapitia sasa kutokuwa na maendeleo mazuri katika mechi zao tano walizocheza nyumbani na ugenini, wameshinda mechi tatu na kutoka sare mbili huku wakikusanya pointi 11 wakishika nafasi ya pili kwenye msimamo huo.
Pamoja na matokeo hayo, kiwango chao si bora kama ilivyokuwa msimu uliopita kwani hawachezi vizuri, wamekuwa na makosa mengi kwenye maeneo mbalimbali, wanakosa nafasi nyingi za kufunga mabao jambo ambalo hata mashabiki wao wamekuwa hawalifurahii.
LIGI YA MABIMGWA
Simba walianzia hatua ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika huku wengi wakiamini watakwenda hatua ya makundi kutokana na aina ya wapinzani ambao walikutana nao.
Kama haitoshi mbali ya kucheza na Jwaneng Galaxy ambayo haikuwa timu tishio kutokana na rekodi zao walianza vizuri mechi ya ugenini kwa kupata ushindi wa mabao 2-0.
Jambo la kushangaza kwenye mechi ya marudiano ambayo Simba walikuwa nyumbani huku wakiwa na uhakika mkubwa wa kushinda kutokana na walivyocheza mechi ya kwanza walipoteza mabao 3-1.
Baada ya kichapo hicho cha nyumbani Simba waliondolewa katika mashindano hayo kwa ngazi kubwa ya klabu huku wakiwa wamecheza soka si la kuvutia.
BENCHI LA UFUNDI
Baada ya kuondolewa kwenye mashindano hayo ikiwemo kufungwa na Yanga, uongozi uliamua kuachana na makocha wao akiwemo kocha mkuu Didier Gomes na wasaidizi wake Milton Nienov na Adel Zrane, hadi sasa wamecheza mechi mbili za kimashindano bila ya kocha mkuu huku timu ikisimamiwa na kocha msaidizi Thierry Hitimana.
Huenda kuvunja benchi la ufundi kumechangia pia kuwepo ugumu wa kufanya vizuri mechi yao ya Coastal Union ambao walitoka nao sare tasa na kupata ushindi dakika za mwisho dhidi ya Polisi Tanzania wa bao 1-0.
WAMEINGIA LAWAMA
Kuondolewa kwao Ligi ya Mabingwa kuliibuka baadhi ya maneno na kuna wachezaji waliingia lawamani akiwemo beki wa kati, Pascal Wawa.
Wawa tangu mechi na Galaxy amekutana na presha kubwa mno hadi kushindwa kuwepo hata benchi katika mechi mbili za ligi dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union.
UBORA WA YANGA
Chungu nyingine ambayo Simba wanapitia ni ubora ambao wameonyesha wapinzani wao Yanga ambao haukutarajiwa na wengi.
Kama shabiki wa Simba anatoka kuangalia mechi za Yanga ubora ambao wanaonyesha akienda kufananisha na kile ambacho wanaonyesha Simba hadi wakati huu lazima atakuwa na mengi kuongea moyoni mwake.
Simba mbali ya kushindwa kupata ushindi mfululizo kikosi chao kimekuwa hakichezi soka la kuvutia pengine kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita.
WASIKIE WADAU
Mchambuzi wa soka nchini, Jemedary Said alisema kuna wakati Simba walifikia mafanikio ya juu katika maisha ya soka hasa nchini ila sasa inaonekana ni tofauti.
“Binafsi Simba wanatakiwa kupata kocha mzuri, viongozi wote kuwa na muelekeo mmoja, wachezaji kutambua majukumu yao pamoja na mengine ya msingi naamini bado wapo imara”.
Kwa upande wa kocha wa timu ya taifa ya wanawake, Edna Lema alisema; “Simba inahitaji muda kidogo kuimarisha maeneo ya msingi ambayo wameonyesha kuwa na mapungufu msimu huu ili kurudi katika ubora wao.”