Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nusu fainali ASFC heshima inasakwa

Simba SC Players Nusu fainali ASFC heshima inasakwa

Tue, 2 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba na Yanga zimemaliza wikiendi kwa jasho kubwa katika michezo ya kimataifa, Simba Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga jana ilicheza na Rivers Uwanja wa Mkapa katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Wiki hii timu hizo zinashuka tena uwanjani katika michezo ya hatua ya robo fainali Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) Simba ikiwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara dhidi ya Azam huku Yanga ikiwa Liti dhidi ya Singida Big Stars.

Yanga ndiyo bingwa mtetezi baada ya kuivua ubingwa Simba msimu uliopita huku Azam nayo iliwahi kuubeba ubingwa huo msimu wa mwaka 2018/19 kwa kuichapa bao 1-0 Lipuli katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Ilulu, Lindi.

Rekodi tamu

Tangu kurejeshwa kwa mashindano haya msimu wa mwaka 2015/16 Yanga imetinga hatua ya fainali mara tatu kama ilivyo kwa Simba, mwaka 2015/16, 2020/21 na msimu uliopita na katika fainali hizo imebeba ubingwa mara mbili, 2015/16 ikiifunga Azam 3-1 na msimu uliopita ikiifunga Coastal Union kwa penalti 4-1.

Simba ndio timu ambayo imewahi kutetea ubingwa kwa misimu saba ya mwisho kwani ikifika fainali imekuwa ikibeba ubingwa, msimu wa mwaka 2016/17 ikiifunga Mbao FC mabao 2-1, 2019/20 ikiichapa 2-1 Namungo Uwanja wa Nelson Mandela na 2020/21 ikiichapa Yanga bao 1-0.

Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 1967 Yanga imebeba mara nyingi zaidi sita (6) msimu wa mwaka 1967, 1974, 1998, 2001, 2015-16 na 2021/22.

Mchezo wa fainali msimu uliopita kati ya Yanga na Coastal Union uliozaa mabao mengi (6) tangu msimu wa mwaka 2015/16 yaliporejeshwa na ndio fainali iliyoamuriwa kwa penalti (Yanga 4-1 Coastal Union).

Wafungaji Bora

Hadi sasa Andew Simchimba wa Ihefu ndio anaongoza kwa mabao mengi (7) na katika misimu hii saba, Abdul Suleiman 'Sopu' akiwa Coastal Union ndiye mchezaji aliyefunga ‘hat trick’ kwenye fainali na ndiye mchezaji hadi sasa aliyemfunga mabao mengi (5) kipa wa Yanga, Djigui Diarra matatu kwenye ASFC na mawili kwenye Ligi Kuu.

Tangu msimu wa mwaka 2015/16 hakuna mfungaji bora aliyewahi kufikisha mabao 10 kwani msimu huo Hamis Kiiza (Yanga) alifikisha mabao sita japo tuzo ya mfungaji bora alipewa kimakosa Atupere Green aliyekuwa na mabao matano.

Msimu wa 2016/17 mfungaji bora alikuwa Obray Chirwa (Yanga) kwa mabao yake matano, 2017/18 Habib Kyombo (Mbao FC) akitwaa tuzo kwa mabao sita, 2018/19 Seif Karie akimaliza michuano kwa mabao manne.

Msimu wa 2019/20, Omari Yassin (Panama FC) akiwa na mabao tisa, Reliants Lusaji (Namungo) msimu wa 2020/21, akimaliza na mabao manne na msimu uliopita, Abdul Suleiman ‘Sopu’ akitwaa tuzo kwa mabao tisa.

Wametisha sana

Panama FC iliyokuwa inashiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL)Dar es Salaam ndiyo timu ya mwisho kutoka daraja la chini kufika hatua ya robo fainali (2019/20) baada ya kuchapwa na Sahare All Stars iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship) ambayo ilikwenda nusu fainali na kufungwa 1-0 na Namungo.

Lakini kabla ya hapo Baker Rangers ya Magomeni iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Nne ndio timu ya daraja la chini zaidi kufika hatua ya fainali mwaka 2002 kwa kuichapa Simba lakini ikapoteza fainali dhidi ya JKT Ruvu Stars.

Waamuzi hawa hapa

Tangu msimu wa mwaka 2015/16 hakuna mwamuzi aliyechezesha fainali mara mbili, msimu wa mwaka 2016/17 alichezesha, Ahmed Kikumbo, Emmanuel Mwandembwa (2017/18), Hans Mabena (2018/19), Abdalah Mwinyimkuu (2019/20), Ahmed Arajiga (2021/22) na Ramadhan Kayoko ((2021/22).

Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha ndio uwanja uliochezwa fainali mbili katika misimu hii saba ya nyuma, ilichezwa mwaka 2017/18 Mtibwa ikiichapa Singida United 3-2 na msimu uliopita.

Viwanja vingine vilivyochezwa fainali ni Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa) msimu wa 2015/16 Yanga ikiwa bingwa, Jamhuri, Dodoma (2016/17), Ilulu, Lindi (2018/19) Azam ikiifunga Lipuli 1-0 na Nelson Mandela (2020/21).

Simba, Yanga walimopita

Tangu mwaka 2015, Simba imebeba ubingwa mara tatu, 2016/17, 2019/20 na msimu wa 2020/21 wakati Yanga ikibeba mara mbili 2015/16, na 2021/22, Mtibwa 2017/18 na Azam msimu wa mwaka 2018/19.

Katika misimu saba, Yanga 2015/16 ndiyo ilikuwa bingwa kwa kuichapa Azam mabao 3-1 wakati Simba iliishia hatua ya robo fainali ilipofungwa na Coastal Union 2-1 ambayo nayo ilifungwa na Yanga nusu fainali.

Msimu wa 2016/17, Simba ikitwaa ubingwa kwa kuichapa Mbao FC, Yanga iliishia hatua ya nusu fainali ikifungwa na Mbao FC bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, bao lililofungwa na Pius Bustwita.

Simba mambo yakawaendea ovyo msimu wa 2017/18 ilipoondolewa na Green Warriors kwa penalti hatua ya 32 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Yanga nao hawakufika mbali kwani ilichapwa na Singida United kwa penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuifanya Singida kwenda hadi fainali na kupoteza kwa mabao 3-2 mbele ya Mtibwa Sugar.

Simba ikaendelea kufanya vibaya msimu uliofuata (2018/19) ilipoondolewa hatua ya 32 kwa kuchapwa na Mashujaa FC mabao 3-2, wakati Yanga ilichapwa nusu fainali mabao 2-0 na Lipuli iliyotinga fainali na Azam ilitwaa ubingwa.

Msimu wa 2019/20 Simba ikitwaa ubingwa kwa kuichapa Namungo 2-1, Yanga iliishia hatua ya nusu fainali ikifungwa 4-1 na Simba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live