Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nusu fainali AFCON hakuna mnyonge

Congo DR AFCON Nusu fainali AFCON hakuna mnyonge

Tue, 6 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), inafanyika kesho katika miji ya Bouake na Abidjan ikizihusisha timu nne za taifa ambazo ni Nigeria, Afrika Kusini, Ivory Coast na DR Congo.

Katika Uwanja wa La Paix, Bouake, Afrika Kusini itakabiliana na Nigeria kuanzia saa 2:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki wakati kuanzia saa 5:00 usiku, wenyeji Ivory Coast watakabiliana na DR Congo jijini Abidjan katika Uwanja wa Alassane Ouattara.

Ni nusu fainali isiyo ya unyonge kwani inakutanisha timu nne za taifa ambazo kila moja imewahi kuonja ladha ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo katika nyakati tofauti lakini pia mbali na hilo, kila moja imekuwa na historia ya kufika hatua za juu za mashindano hayo mara nyingi.

NIGERIA

Nigeria ni bingwa mara tatu wa mashindano hayo ikiondoka na taji mwaka 1980, 1994 na 2013.

Imetinga hatua ya fainali baada ya kuichapa Angola bao 1-0 katika hatua iliyopita, shukrani kwa bao la nyota wa Atalanta, Ademola Lookman.

Silaha kubwa ya Nigeria katika fainali za Afcon mwaka huu ni safu yake ya ulinzi ambayo hadi sasa ikiwa kwenye nusu fainali, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu katika mashindano hayo mwaka huu.

Ukiondoa Lookman mwenye mabao matatu, tegemeo lingine la Nigeria katika mechi hiyo ya nusu fainali ni mshambuliaji wa Napoli, Victor Osimhen.

AFRIKA KUSINI

Wakati mashindano hayo yanaanza, Afrika Kusini haikutegemewa kama ingeweza kufika hatua iliyopo na imani hiyo iliongezeka baada ya kuanza kwa kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mali.

Lakini baadaye Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana ilibadilika na kuonyesha kiwango bora, ikivuna pointi nne katika mechi mbili zilizofuata za hatua ya makundi dhidi ya Namibia na Tunisia kisha ikashtua wengi kwa kuichapa Morocco mabao 2-0 kwenye hatua ya 16 bora.

Mabingwa hao wa Afcon mwaka 1996, wametinga hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 2-1 dhidi ya Cape Verde baada ya timu hizo kutoka suluhu katika dakika 120 za mchezo.

Kipa na nahodha wa timu hiyo, Ronwen Williams amekuwa tegemeo lao kubwa kwa sasa kutokana na uwezo mkubwa ambao amekuwa akiuonyesha katika kulinda lango lake.

IVORY COAST

Wenyeji Ivory Coast ni mabingwa mara mbili wa Afcon wakichukua taji hilo mwaka 1992 na 2015, mara zote wakiifunga Ghana kwenye mechi za fainali.

Ni timu ambayo inaonekana imeingia hatua ya nusu fainali kimaajabu kutokana na mwenendo mbaya iliokuwa nao kwenye hatua ya makundi, ikishinda mechi moja tu na kupoteza mbili na iliingia hatua ya 16 bora kwa kutegemea nafasi nne za timu shindwa zenye matokeo bora (best losers).

Katika raundi ya 16 bora ilishtua wengi kwa kuitupa nje, Senegal kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida wa mchezo na kwenye robo fainali ikaichapa Mali kwa mabao 2-1.

Inaingia katika mechi ya nusu fainali ikimkosa nyota wake tegemeo, Omar Diakhite ambaye anatumikia adhabu ya kukosa mechi moja kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.

DR CONGO

Sare tatu ilizopata katika hatua ya makundi, zilitosha kuipeleka DR Congo katika hatua ya 16 bora ambayo iliweza kuvuka na sasa ni miongoni mwa miamba minne iliyopo katika hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Afcon.

DR Congo hii itakuwa ni mara yao ya sita kucheza hatua ya nusu fainali ya Afcon ambapo kati ya mara tano zilizopita, walifanikiwa kuondoka na medali tofauti katika mara nne tofauti.

Mara mbili walichukua ubingwa ambazo ni mwaka 1968 na 1974, wakimaliza katika nafasi ya tatu mara mbili ambazo ni 1998 na 2015 na mwaka 1972 walimaliza katika nafasi ya nne.

Kumbukumbu nzuri kwa DR Congo ni kwamba mara zote mbili walizowahi kutwaa ubingwa, walipata ushindi dhidi ya timu mwenyeji kwenye nusu fainali na sasa wanakwenda tena kuvaana naye.

Chanzo: Mwanaspoti