MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi sasa imeingia hatua ya nusu fainali, ambapo timu nne zote kutoka Tanzania Bara zimefanikiwa kufuzu hatua hiyo ambazo ni Yanga, Simba, Azam na Namungo.
Katika hatua hii mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga wanatarajiwa kuvaana na Azam, huku watani zao wa jadi Simba wao wakivaana na Namungo.
Nusu fainali hizi ni marudio ya nusu fainali za mwaka jana za mashindano haya ambapo Simba iliwaondosha Namungo kwa kuwafunga mabao 2-1, huku Yanga wakiwa na kumbukumbu ya kuiondoa Azam kwa changamoto ya mikwaju ya Penalti 5-4 baada ya sare ya bao 1-1 kwenye dakika 90.
Ninakuletea baadhi ya dondoo muhimu kuhusu nusu fainali hizo mbili zitakazopigwa leo Jumatatu kama ifuatavyo;
MICHEZO YA KISASI
Michezo hii unaweza kuipa thamani ya kuwa ya kisasi, achana na matokeo ya mwaka jana lakini moto zaidi unakolea kutokana na matokeo ya timu hizi mbili katika michezo yao ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Simba wao katika mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Namungo walibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa dakika za mwisho na mshambuliaji raia wa Rwanda, Meddie Kagere, mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, hivyo hii ni nafasi kwa Namungo kulipa kisasi mbele ya Simba.
Yanga wao wataingia katika mchezo dhidi ya Azam wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga wapinzani wao hao mabao 2-0, hivyo hii ni nafasi kwa Azam pia kujiuliza mbele ya Yanga.
AZAM YAWAFUNIKA WOTE
Miongoni mwa timu zote nne zilizoingia hatua ya nusu fainali, Azam ndiyo wamekuwa na matokeo mazuri zaidi kulinganisha na timu zote tatu zilizosalia.
Azam imetinga hatua hiyo baada ya kukusanya pointi zote tisa baada ya kushinda michezo yao mitatu ya hatua ya makundi dhidi ya Yosso Boys, Meli 4 City na Namungo ambao walikuwa nao ndani ya kundi A.
Namungo ni timu ya pili iliyotinga kwenye hatua ya nusu fainali wakiwa na pointi nyingi, hii ni baada ya kukusanya pointi sita wakishinda mechi mbili dhidi ya Yosso Boys na Meli 4 City, huku wakipoteza mbele ya Azam.
Simba na Yanga ndizo zimetinga hatua hii wakiwa na pointi chache zaidi ambapo kila moja imekusanya pointi nne tu, kila timu ilishida mechi moja na kutoa sare mechi moja kwenye makundi B na C waliyoyaongoza.
CHANGAMOTO MPYA KWA PABLO, KAZE
Kocha Pablo Franco wa Simba na Cedric Kaze wa Yanga wanatarajia kukutana na changamoto ya tofauti katika michezo hii kulinganisha na michezo ya mkondo wa kwanza ya ligi kuu, hii ni kutokana na mabadiliko ya mabenchi ya ufundi yaliyofanywa na wapinzani wao Azam na Namungo.
Ikumbukwe kuwa wakati Simba inaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo kikosi hicho kilikuwa chini ya aliyekuwa kocha msaidizi Mnyarwanda, Thierry Hitimana hivyo kocha Pablo anatarajiwa kukutana na changamoto mpya kutoka kwa benchi jipya la Namungo chini ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Kwa upande wa Kaze yeye alikuwa sehemu ya benchi la ufundi la Yanga lililoibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam ambayo ilikuwa chini ya Mzambia, George Lwandamina lakini sasa atakutana na kihunzi cha Mmarekani, Abdihamid Moallin ambaye anaonekana kuisuka Azam mpya.
WADHAMINI WACHOCHEA MOTO
Katika michezo yote ya hatua ya makundi ya mashindano haya mchezaji bora wa mechi alikuwa akichukua mzigo wa fedha kiasi cha Shilingi 500,000, lakini kwa michezo yote miwili ya nusu fainali dau hilo limeongezwa na kuwa 1,000,000.
Hali ambayo ni wazi itaongeza ari ya ushindani kwa wachezaji, katika majukumu yao ya kuzisaidia klabu wanazo tumikia.