Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nuksi wamechemka baada ya kusajiliwa dirisha dogo

Samatta Chama Nuksi wamechemka baada ya kusajiliwa dirisha dogo

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dirisha dogo la usajili la Januari limeshika kasi Ulaya na mabosi wanasikilizia kunasa saini za wachezaji watakaokwenda kuimarisha vikosi vyao kwenye kuwania mataji mwisho wa msimu.

Hata hivyo, dirisha hili limekuwa likichukuliwa kama la kujiokotea tu na hakuna wachezaji sahihi wa kuwanasa hadi lile la majira ya kiangazi.

Linatajwa pia kama ni dirisha nuksi kwa wachezaji wanaokwenda kwenye timu nyingine licha ya wanakotoka kuonyesha viwango vikubwa na kutamanisha vigogo kurusha ndoano zao na kuwanasa.

Mastaa wengi waliosajiliwa dirisha la Januari wameishia pabaya na wameshindwa kuonyesha kile kilichotarajiwa, ingawa wapo waliofanikiwa.

Hawa hapa mastaa ambao walionyesha moto walikotoka, lakini walikokwenda wakachemka mbaya.

MBWANA SAMATTA

Nyota wa Kitanzania ambaye alisimamisha nchi Watanzania wakishuhudia kwa mara ya kwanza Mtanzania akicheza Ligi Kuu England.

Aston Villa baada ya kuona mavitu yake akiwa na Genk ya Ubelgiji, fasta ikamfuatilia na kukatisha mkataba wake dirisha la Januari ili kwenda kutibu tatizo la ushambuliaji Villa Park.

Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi, Samatta alishindwa kuonyesha ubora wake aliokuwa nao Genk na kwenye mechi 16 za michuano yote aliyocheza akiwa na Villa, alifunga mabao mawili tu.

Moja ya mabao hayo alifunga kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Bournemouth, huku jingine akifunga kwenye fainali ya Carabao dhidi ya Manchester City.

Villa ilimtoa kwa mkopo mwisho wa msimu kwenda Fernebance kabla ya kuuzwa jumla kwa timu hiyo. Alikaa Villa kwa miezi isiyozidi minane.

ALEXIS SANCHEZ

Akiwa Arsenal, Sanchez alikuwa moto na kuzitamanisha Manchester United na City kuinasa saini yake.

Hata hivyo, mwishowe United ilishinda mbio hizo na kumpa mkataba wa miaka mitano na mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki huku akitarajiwa kuendeleza kile alichokuwa akikifanya The Gunners.

Kilichofuata ni kama ilivyokuwa kwa Samatta na staa huyu wa kimataifa wa Chile alishindwa kuonyesha mavitu yake Old Trafford na kwenye mechi 45 za michuano yote aliyocheza alifunga mabao matano, huku kwenye ligi akifunga matatu.

Man United iliamua kumtoa kwa mkopo kwenda Inter Milan ya Italia kabla ya kuamua kujiunga nao jumla mwaka 2019.

ANDY CARROL

Mwaka 2011, Liverpool ilivunja benki na kumsajili Andy Carroll kutoka Newcastle United kwa ada ya uhamisho ya Pauni 35 mlioni na ilimsainisha mkataba wa miaka mitano na nusu. Ada hiyo ya uhamisho ilivunja rekodi ya timu hiyo na kumfanya Carroll kuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kutokea kwa wakati huo.

Hata hivyo, wakati anasajiliwa tu alipata majeraha hivyo ilitakiwa asubiri kwa mwezi mmoja kabla ya kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza.

Alicheza mechi ya kwanza dhidi ya Manchester United. Baada ya hapo alikaa kwa miezi 18 tu, kwenye viunga hivyo vya Merseyside akacheza mechi 58 na kufunga mabao 11. Baada ya hapo alitolewa kwa mkopo kwenda West Ham na baadaye akauzwa kwenye timu hiyo kwa ada ya uhamisho ya Euro 17.5 milioni.

PHILIPPE COUTINHO

Alijiunga na Barcelona akitokea Liverpool mwaka 2018, kwa usajili wa pesa nyingi uliotikisa. Barca ililazimika kutoa Pauni 105 milioni, ambayo ilikuwa inaweza kuzidi kulingana na vipengele mbalimbali vilivyowekwa kwenye mkataba wake.

Katika miezi mitano ya mwanzo alionyesha kiwango bora kwa kufunga mabao tisa na kutoa asisti nane kwenye mechi 22 za michuano yote. Lakini msimu wa 2018-19 alizidi kushuka kiwango, akifunga mabao matano tu kwenye mechi 34 za msimu huo.

Aliachwa na akajiunga na Bayern katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2019 kwa mkataba wa mkopo wa msimu mmoja.

Alirudi tena Barca mwaka 2020, lakini mambo yakaendelea kuwa mabaya kutokana na majeraha ya paja yaliyokuwa yanamwandama.

Kijumla alicheza mechi 106 za michuano yote, akafunga mabao 25 na kutoa asisti 14, ilipofika Januari 7, akajiunga na Aston Villa kwa mkopo na akasaini nao mkataba wa kudumu, akiwa hapo pia akatolewa kwa mkopo kwenda Al Duhail ya Qatar.

JUAN CUADRADO

Chelsea ilimsajili staa huyu baada ya kuvutiwa na kiwango alichoonyesha kwenye mashindano ya Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Colombia.

Baada ya kufika na kuitumikia Chelsea kwa nusu msimu, Agosti mwaka 2015 alitolewa kwa mkopo kwenda Juventus kabla ya kuuzwa mazima.

Katika kipindi chake akiwa na matajiri hao wa Jiji la London alicheza mechi 15 na kutoa asisti moja.

WILFRIED BONY

Kabla ya Harry Kane, Bony alikuwa mmoja kati ya wachezaji walioonyesha kiwango bora sana kwenye Ligi Kuu England kwenye suala la ufungaji. Wakati huo alikuwa akiitumikia Swansea. Mwaka 2014 alimaliza kwa mabao 20. Man City ikashawishika kumsajili ikitoa Pauni 25 milioni.

Hata hivyo, baada ya Pep Guardiola kuchukua mikoba ya kuifundisha timu hii, hakushawishika na kiwango cha Bony ambaye alimkuta kwenye mechi 46 amefunga mabao 10 tu na kutaka atolewe kwa mkopo kabla ya kuuzwa jumla Swansea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live