Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Novatus mbele kwa mbele tu

Novatus Dismas Nidhamu Novatus Dismas

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ukizungumzia wachezaji wenye umri mdogo ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars hutaacha kumzungumzia Novatus Dismas.

Novatus aliyezichezea baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara ambazo ni Biashara United na Azam FC, anacheza soka la kulipwa Ubelgiji ambako amejizolea umaarufu kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja.

Novatus alitangazwa msimu wa 2020/21 kuwa kwenye mipango ya Azam FC na walimuongeza mkataba wa miaka mitatu, lakini nafasi aliyopata ya kwenda Israel ndio ilikuwa tiketi yake ya kuanza soka la kimataifa.

Kwani licha ya kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya kwenda kujifunza, akajikuta akipata nafasi ya kuonyesha kipaji chake na hapo ndipo Maccabi Tel Aviv ilipovutiwa naye na kumsajili na alitumika kwa kipindi cha misimu miwili.

Novatus Dismas amejiunga msimu wa 2022/23 na klabu ya SV Zulte Waregem inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Maccabi Tel Aviv ya Israel.

MAISHA NJE NA BONGO

Novatus anasema maisha ya Bongo na kule hayako sawa, kwani namna wanavyoishi Ubelgiji ni tofauti kubwa na hapa nchini kutokana na mifumo yao ya upatikanaji wa vitu na maisha kwa ujumla.

Anasema kwa mtu yeyote aliyebadilishiwa mazingira lazima aone utofauti kuanzia hali ya hewa ma mengine.

"Maisha ya wenzetu yanaweza kuwa mazuri zaidi kutokana na technolojia yao kuwa kubwa zaidi lakini nyumbani ni bado pana upekee wake na raha yake pia."

MSIMU WA KWANZA ULAYA

Novatus anasema msimu uliopita ndio ulikuwa wa kwanza kwake katika mambo mengi, anaeleza kuwa kipindi hicho alicheza michezo mingi zaidi tangu aanze safari yake ya soka.

Anasema ukiachana na michezo mingi pia hata kucheza soka la kulipwa hili kwake ni mafanikio makubwa ambayo vijana wengi kama yeye wanatamani kuyafikia lakini kwa sababu mbalimbali hawajaweza kufikia.

"Mpira wa Nje kwangu umekuwa wa mafanikio makubwa kwani naweza kusema ni kipindi ambacho nimecheza michezo mingi zaidi ambayo imeniwezesha kuwa bora zaidi," anasema Novatus.

WAZAWA WANAKWAMA HAPA

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 kwa sasa anasema kupata bahati ya kucheza nje inakuwa ngumu kwa wachezaji wazawa kuipata kwani hakuna uwekezaji uliofanyika wa kuzalisha vipaji vitakavyoweza kukuzwa na kuonekana mbali.

Anasema kuwa wenzetu wamefaulu sana kuwa na wachezaji nje ya nchi kwani walipeleka watoto wenye vipaji katika Academy za kujifunzia mpira ndio maana wachezaji wao wengi wanacheza huko.

"Uwepo wa vijana wanaopata mafunzo ya mpira huku na wametokea nchi zingine ndio uliowapa fursa wachezaji wengi wa nchi zisizo za bara hili kuja kucheza Ulaya."

"Tukifanya uwekezaji mzuri tutapata mawakala wengi watakaotaka kupeleka wachezaji wetu kutumika kwenye timu nje na Tanzania," alisema Novatus.

KITU ROHO INAPENDA

Mchezaji huyo anasema kwa sasa hawezi akasema kuwa anatamani kucheza soka la nyumbani kwani tayari analifahamu hivyo ndoto zake ni kuendelea kubaki Ulaya.

Anasema kuwa kucheza kwake huko kumemfanya abadilike na kujihisi kama amekuwa mchezaji mpya kwani huku alikuwa anacheza nafasi ya kiungo na sasa ni beki hivyo kwake ni mafanikio.

"Akili yangu ya mpira kwa sasa imebadilika sana kwani nacheza na wachezaji wenye ubora zaidi hivyo inanibidi nipambane kuhakikisha nakuwa na uwezo wa kushindana nao."

"Sasa kucheza nyumbani sio kipaombele kwani nafikiria mbali zaidi hasa katika eneeo la kufanikiwa kupitia soka hivyo shauku yangu ni kuendelea kusalia Ulaya," anasema Novatus

SITASAHAU

Novatusi anasema hatasahau kushuka daraja kwa timu yake kwani ni jambo lililomuumiza zaidi katika maisha yake ya soka aliyopitia kutoka alipoanza hadi sasa.

Anasema haikuwa rahisi kwake msimu huu kwani ushindani ulikuwa mkubwa na wachezaji wamekuwa bora ila anaeleza kuwa pamoja na yote alijiandaa kiakili kupokea lolote ambalo lingetokea mwisho wa msimu.

"Tulikuwa na timu nzuri ambayo haikuwa inafungwa lakini mchezo wa mwisho ndio ulioamua sisi kushuka daraja pamoja na yote bado najiandaa kufanya vizuri msimu ujao."

"Msimu wote nilijifunza kutumia nafasi zote niolizopata vizuri hivyo tuluivyoshuka niliona ni mipango ya Mungu kwani tulifanya juhudi zote kuhakikisha tunabaki," anasema Beki huyo.

MSIMU UJAO

Beki huyo anaehusishwa na timu mbalimbali Ulaya anasema mpaka sasa hana taarifa rasmi ya kuhitajika msimu ujao na timu yoyote kwani bado ana mkataba na kikosi chake hicho ambacho bado ni kipya.

Anasema kuwa kama kuna timu inamuhitaji lazima iende kwa viongozi wangu na timu pia wapewe utaratibu na kufikia makubaliano.

"Sijapokea ofa yoyote ile hivyo msimu ujao nitaendelea kutumikia timu yangu ambayo bado nina mkataba nayo ila hata ikitokea imekuja nafasi ya kuondoka bai lazima iwe ya Ulaya kwani huko ndiko natamani kucheza."

LIGI YA BONGO NA ULAYA

Beki huyo ambae ndio mara yake ya kwanza kucheza Ulaya anasema utofauti wa Ligi yetu na kule ni mkubwa sana hata aina ya wachezaji na kasi ya mechi.

Anaeleza kuwa wachezaji wengi wa Ligi Kuu Ulaya wanakuwa wazuri, hivyo wakiletwa huku wanaweza kuwa Mastaa kwani wanauzoefu mkubwa mpira kwani wakua wakicheza tangu utotoni.

"Ulaya wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuwa na wachezaji wazuri kutokana na mafunzo wanayoyapata tangu utotoni hivyo tunaona kuwa Ligi yao ni nzuri zaidi kuliko yetu kwa sasa."

"Uwekezaji wa muda mrefu unaweza kutufanya tuwe na viwango hivyo kwani hakuna kinachoshindikana kwenye hii dunia ila ni swala la muda ili kuweza kufikia malengo hayo makubwa," anasema Novatus.

SOKA LETU LIMEKUA

Novatus anasema sasahivi tumeongezeka na ubora wa wachezaji ni mkubwa ukilinganisha na miaka miwili hapo nyuma hii inatupa picha kuwa tunakoenda kunaweza kuwa kuzuri zaidi ya tuliko toka.

Anaendelea kusema kwaka anaona fahari anapoona nchi yetu inashiriki mashindano na kufika mbali hii inamaana kuwa tunauwezo wa kukabiliana na timu kubwa na bado tukashinda.

"Sasa mpira umekua na ni kazi ya kuheshimika hivyo mabadiliko lazima yaendelee ili kuhakikisha kuwa tunawakilisha nchi mbali zaidi kwani uwezo na nguvu tunazo."

Chanzo: Mwanaspoti