Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Novatus anabebeshwa majukumu mazito kuzidi uwezo

Novatus Dismas UEFA Novatus anabebeshwa majukumu mazito kuzidi uwezo

Mon, 25 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wengi wanavutiwa na uchezaji wa kiungo wa Taifa Stars, Novatus Dismas Miroshi na unapowauliza sababu watakwambia pasi zake zinafika halafu anakaba sana.

Kwa hiyo hata alipohamishiwa nafasi ya kiungo wa chini kutoka beki wa pembeni upande wa kushoto, wengi waliona sawa na hasa zile siasa za kuwapa nafasi vijana zinapokolea. Ndio Novatus anaendelea kuikamata nafasi hiyo akifurahisha watu kwa pasi zake fupifupi na wakati mwingine kupiga ndefu kukatisha uwanja, wenyewe huziita diagonal au switching.

Alifanya hivyo katika mechi iliyopita dhidi ya Bulgaria nchini Azerbaijan, lakini bado wapinzani wakatumia muda mwingi golini kwa Taifa Stars, ambayo ilikwenda mbele kwa nadra na hasa timu hiyo kutoka barani Ulaya ilipopoteza mipira wakati ikianza kuchakata mashambulizi.

Kwa nini Nova atoe pasi nyingi zinazofika lakini timu haisogei mbele kuhamia nusu ya wapinzani?

Ni kwa sababu pasi zake fupifupi hazilengi kuwasukumu wapinzani kurudi golini kwao kuweka ukuta, bali huiwezesha Taifa Stars kumiliki mpira kwa muda tu.

Na pale anapojaribu kuhamisha mpira kwa pasi ndefu, mara nyingi huishia ama miguuni au vichwani mwa mabeki au hutua kwa mchezaji mwenzake ambaye anakuwa eneo ambalo wapinzani wamekamilika (balanced) na hivyo haiwi hatari kwao.

Timu inapokuwa imebanwa kwenye nusu yao, Nova huishiwa maarifa ya nini afanye na hivyo kuendelea na zilezile pasi fupi ambazo mara nyingine hunaswa au zile ndefu ambazo hukuta mabeki wa upinzani wamejipanga vizuri.

Hushindwa kuamua kuibeba timu mabegani mwake na kuivusha mstari wa kati kwa ajili ya kuwawahi wapinzani kabla hawajajipanga vizuri au wakati wana idadi ndogo ya watu baada ya kupoteza mpira wakati wakishambulia.

Kuuchukua mpira kwa kutumia uwezo wake na kulazimisha wenzake wakimbie naye kwenda nusu ya wapinzani ni moja ya silaha kubwa za viungo wa chini wanapoona timu imezuiwa kwenye nusu yao na majaribio yote ya kupenyeza mipira hushindikana.

Na wakati mwingine, badala ya kucheza pasi zinazosogeza wapinzani warudi kwenye nusu yao, ni muhimu kwa kiungo wa chini kugongeana na wenzake pasi ambazo zinaiondoa timu yake golini kwao na kwenda kuwazonga wapinzani kwenye nusu yao. Nova alishindwa kutumia uwezo huo binafsi kuiondoa timu golini kwake mbele ya Wabulgaria.

Kwa kifupi, Novatus anapangwa nafasi ambayo ina majukumu makubwa kuliko uwezo wake ambao ni mkubwa lakini unakosa uzoefu na uamuzi wa kujiamini kuwa anaweza kufanya jitihada binafsi kuiondoa timu matatizoni.

Kiungo wa chini ni roho ya timu ambayo huwa na kazi kubwa ya kuikinga safu yake ya ulinzi, kuituliza timu na kuiunganisha wakati inapotoka golini, kuchakata mpira wakati wa kutafuta mbinu za kuichana ngome na zaidi ya yote kutumia uwezo binafsi kuibeba timu wakati inaposakamwa mfululizo kwenye nusu yao.

Bado Novatus anahitaji kuendelea kucheza kama beki wa pembeni kama anavyopangwa kwenye klabu yake na taratibu ahamie katikati kama ilivyokuwa kwa mabeki kama Phillip Lahm, ambaye alicheza kwa muda mrefu kama beki wa kulia wa Bayern Munich kabla ya kuhamia kiungo cha chini, na Joshua Kimmich, ambaye alianzia beki wa kulia Bayern Munich na baadaye kuhamia kiungo wa chini.

Na ndivyo ilivyokuwa kwa Erasto Nyoni ambaye alikuwa beki wa pembeni wakati akihamia Azam kutoka Vital’O ya Burundi na pia timu ya taifa, kabla ya kuhamia beki wa kati na baadaye kiungo wa chini, nafasi ambayo anaicheza hadi sasa.

Kwa kawaida viungo wengi wazuri wa chini ni wale wenye uzoefu mkubwa, uwezo wa kuusoma mchezo na wenye uamuzi mgumu. Si kwamba vijana hawawezi, la hasha! Lakini uzoefu ni kitu muhimu kwa nafasi kama hiyo yenye majukumu makubwa kwa timu.

Na Novatus Dismas Miroshi bado hajapata uzoefu huo wa kujazia kwenye kipaji chake cha kukaba, kutawanya mipira na kufanya uamuzi mgumu. Bado uzoefu wake haujatosha kumbebesha majukumu mazito.

Chanzo: Mwanaspoti