Mshambuliaji wa Kitayosce, Yohana Nkomola amesema bado anajitafuta kutokana na kutocheza Ligi Kuu muda mrefu, lakini anatambua majukumu aliyonayo kuisaidia timu hiyo iliyopanda msimu huu.
Mara ya mwisho Nkomola kucheza ligi hiyo ilikuwa 2019 akiwa Yanga kisha akajiunga na Vorskla Poltava (2019-2022) iliyomtoa kwa mkopo Inhulets Petrove (2020/21), akatolewa tena kwa mkopo Hirnyk-Sport, kisha akarejea nchini baada ya Ukraine kuwepo vita na Russia.
“Ingawa nilikuwa nafanya mazoezi sana baada ya kurejea nchini na kucheza mechi huko mtaani ili kujiweka fiti, siwezi kufananishwa na mtu anayecheza mechi za mashindano muda mrefu, ndio maana nasema lazima nipambane ili niwe na msimu mzuri,” alisema Nkomola.
“Msimu ulioisha nilifuatilia Ligi Kuu. Hilo limenisaidia kujua nianzie wapi, kwani nauona ushindani unakuwa mkubwa. Hilo linafanya mchezaji asibweteke anapopata nafasi ya kucheza aithamini na kuitendea haki.”
Alisema kikosi cha timu hiyo kina wachezaji wazuri ambao wanamfanya ajitume kushindania namba.
“Ushindani wa namba ni mkubwa, lakini kila mchezaji yupo kwenye timu anatamani kucheza. Kwangu nafurahia kwa sababu inanisaidia kuongeza bidii ya kujituma, ili kupata nafasi ya kucheza,” alisema.