Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nkana lazima wakae

33033 Simba+pic Tanzania Web Photo

Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakuna namna nyingine unayoweza kusema zaidi ya kusema lazima Simba ishinde kulinda heshima ya Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Timu hizo zinapambana leo katika mchezo wa marudiano wa michuano hiyo mikubwa ngazi ya klabu Afrika. Mchezo wa kwanza uliofanyika Kitwe siku 10 zilizopita, Simba ilifungwa mabao 2-1.

Unaweza kusema ni kufa au kupona kwa Simba kwenye mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni huku Simba wakihitaji ushindi wa bao 1-0 tu ili waweze kutinga hatua ya makundi.

Hata hivyo, pamoja na kwamba Simba inahitaji bao moja tu kuingia makundi, lakini linaweza kuwa gumu na kushangazwa kwani Simba haitakiwi kuingia kama washindi wakiamini watafunga kirahisi.

Pia Simba haitakiwi kuruhusu bao katika mchezo huo kwani itazidisha ugumu wa mchezo wenyewe.

Mara ya mwisho Simba kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo ilikuwa mwaka 2003 ikiwa ni miaka miaka 15 hakuna timu yoyote hapa nchini iliyowahi kufanya hivyo tena.

Katika hatu ya hiyo ya makundi Simba ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa kundi moja na vigogo vya soka Enyimba ya Nigeria, ASEC Mimosas ya Ivory Coast na Ismaily ya Misri.

Mara ya mwisho Simba kukutana na Nkana hapa Tanzania ilikuwa mwaka 2002 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro ambapo Simba ilishinda mabao 3-0 katika mchezo wa hatua ya 32 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mchezo wa kwanza Simba ilifungwa mabao 4-0.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika wiki iliyopita ugenini Simba ilionekana kupooza huku wenyeji Nkana wakitawala kwa kiasi kikubwa huku kipa Aishi Manula akiendelea kufanya makosa yale yale ya kuruhusu mabao ya mbali.

Pia Simba leo inatakiwa kuwachunga washambulaiji hatari wa Nkana, Walter Bwalya na Ronald Kampamba ambao wamekuwa na ushirikiano mzuri na wasumbufu kwa mabeki.

Hata hivyo, Wachezaji wa Simba wameapa kufia uwanjani leo ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo huku wakiwataka mashabiki kuzima Tv na kwenda uwanjani kuwapa sapoti kwani uwepo wao utachangia kwa kisai kikubwa wao kupata ushindi.

Winga kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo, Shiza Kichuya alisema kama Nkana walitumia vema uwanja wao kule Kitwe basi nao leo watatumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kwa kuhakikisha wanapata ushindi mnono.

“Mashabiki kuujaza uwanja ni kawaida yenu, njooni kwa wingi mkaisapoti timu yenu. Tuunganishe dua na sala zetu kuiombea Simba ipeperushe vyema bendera yetu,” aliandika Kichuya katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Naye kiungo James Kotei alisema: “Mashabiki msiwe na wasiwasi kwani tutarudi katika mchezo huo tukiwa na nguvu zaidi na kutinga hatua ya makundi. Subirini muone.

Cletous Chama aliandika: “Ni muda wa kusahau yaliyopita na kuangalia yajayo. Tunarejea tukiwa na nguvu kubwa.

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema matokeo ambayo waliyapata katika mechi ya kwanza si ya kukatisha tamaa na wana uwezo wa kupindua meza katika mchezo wa kesho (leo).

“Matokeo hayakuwa mabaya sana kama wachezaji tutapambana zaidi ili kubadili matokeo na kupata yale ya kusonga mbele lakini hata benchi la ufundi nina imani litafanya kazi ya kuingia na mbinu nzuri ili kulifanikisha hili,” alisema Bocco ambaye aliifungia Simba bao la pekee katika mechi ya kule Kitwe.

Naye kiungo Haruna Niyonzima alisema nafasi ya timu yao kusonga mbele katika mechi ya marudiano ni kubwa lakini kazi kubwa ipo kwa wachezaji kupambana kwa dakika zote.

“Kiu ya timu ni kufanya vizuri katika mashindano haya na kucheza hatua ya makundi na mechi hii ndio imeshika hatma yetu kwa hiyo tunafahamu na kuelewa umuhimu wa mechi hii,” alisema Niyonzima.

Beki wa kulia wa Simba Nicholas Gyan alisema mechi ni ngumu kulingana na matokeo ya mechi ya kwanza yalivyokuwa kwani kila timu ina nafasi ya kusonga mbele.

“Kama wao walitufunga katika mechi ya kwanza huko kwao nasi tunaweza kufanya hivyo hapa nyumbani,” alisema Gyan.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema amekiandaa kikamilifu kikosi chake kwa ajili ya kupata ushindi katika mchezo huo.

“Tumejipanga vizuri na tuko nyumbani hivyo tutapata nguvu kubwa kutoka kwa mashabiki wetu, ninaamini kila mchezaji anatambua wajibu wake wa kuhakikisha tunaweka historia mpya kwenye mashindano hayo,” alisema Aussems.

Kikosi kinachoweza kuanza

Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ’Tshabalala’, Erasto Nyoni, Serge Pascal Wawa/Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Cletous Chama, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.



Chanzo: mwananchi.co.tz