Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nkamia aahidi kuwaunganisha Simba

63e7be73fc4e9fa04bce780aebde08ec Nkamia aahidi kuwaunganisha Simba

Thu, 21 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA wa nafasi ya mwenyekiti ndani ya klabu ya Simba, Juma Nkamia amesema moja ya kipaumbele chake kama atachaguliwa atahakikikisha anashirikiana na wanachama nchi nzima kuwapa uhuru wa kuchangia mawazo kwa ajili ya maendeleo ya timu.

Nkamia ambaye alikuwa Mbunge wa Chemba, Dodoma, yupo kwenye kinyang’anyiro hicho na Martaza Mangungu ambaye naye alikuwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Swedi Nkwabi katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika Februari 7, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Nkamia alisema sio mgeni ndani ya klabu hiyo kwani alishawahi kuwa katibu mwenezi wa Simba, hivyo anafahamu matamanio na maono ya wanachama wa timu hiyo.

“Niwaombe wapenzi na wanachama kunipa fursa ya kunichagua siku ya uchaguzi, pamoja na kuwa na vipaumbele vinne ambavyo naamini vimekuwa vikiwasumbua Simba.”

“Nitawaunganisha wanachama nchi nzima na kuwapa fursa ya kutoa mchango wa mawazo kwa maendeleo ya timu,” alisema Nkamia aliyewahi pia kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Alisema vipaumbele vingine ni kusimamia mabadiliko ambayo mchakato wake umeshaanza kufanyika kwa kushirikiana vyema na Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo, kutatua baadhi ya changamoto ikiwamo kinachoendelea dhidi ya tume ya ushindani (FCC) kwa kufanya kikao cha pamoja kumaliza tofauti.

Pia alisema kwakuwa mchezo wa soka unahitaji uwekezaji mkubwa, akipewa ridhaa hiyo atashirikiana na viongozi wengine kuongeza vyanzo vingine vya mapato kwa maslahi ya timu.

Alisema kampeni zake anatarajia kuzindua keshokutwa jijini Dar es Salaam na baada ya hapo atafanya kikao na waandishi wa habari kabla ya kutangaza ratiba ya kwenda mikoa mingine.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Simba, Boniface Lihamwike ametoa wito kwa wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni ya wagombea ili kuwapima na sera zao waweze kuchagua kiongozi bora.

“Wanachama wasibeze na kususia kampeni wajitokeze kwa wingi kuwapima wagombea kwani tumetoa kipindi kikubwa cha wagombea kupita kujinadi kuomba kura wapate fursa ya kuchaguliwa,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz