Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Njooni mhesabu mibao ya Saido

Saido Pic Data Njooni mhesabu mibao ya Saido

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: mwanaspoti.co.tz

YANGA wamepania kuitumia Dodoma Jiji kumtambulisha staa wao mpya, Said Ntibazonkiza lakini Dodoma wameahidi soka la maana na ushindi juu.

Mmoja wa vigogo wa Yanga, Hersi Said amesisitiza kwamba wanatarajia kuona ufundi wa Said kwa mara ya kwanza leo baada ya Kocha Cedrick Kaze kuwahakikisha atacheza baada ya kukamilika kwa vibali vyake kwenye usajili mpya ulioanza juzi. Kaze amekiri kwamba Said ni miongoni mwa wachezaji watakaokuwa kwenye kikosi chake leo na mashabiki watamfurahia kwavile ni miongoni mwa mafundi alionao kikosini.

Said maarufu kama Saido alianza kuonekana kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Singida United alipotupia mbili timu hiyo ikishinda mabao matatu.

Lakini baada ya kuwakosha mashabiki wa Yanga dhidi ya Singida United, leo Ntibazonkiza anasubiriwa kwa hamu Jijini hapa huku jezi za klabu hiyo zikiuzwa kila kona kama njugu kuashiria kwamba mechi hiyo itakuwa na nyomi la aina yake. Timu hizo mbili hazijawahi kukutana sio tu kwenye Ligi Kuu bali hata mashindano mengine na mechi za kirafiki na hii ni mara kwa kwanza kwao kufanya hivyo.

Dodoma Jiji wanaingia katika mchezo huo wakiwa na rekodi isiyovutia katika mechi wanazocheza nje ya mkoa wa Dodoma ambapo hawajawahi kupata ushindi katika mechi hata moja kati ya saba ilizocheza.

Kwenye mechi hizo saba ambazo Dodoma Jiji FC ilicheza nje ya jiji la Dodoma, imetoka sare mara mbili na kupoteza tano, haijafunga bao hata moja na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa (9). Wakati hali ikiwa hivyo wa wageni Dodoma Jiji, Yanga yenyewe ina matokeo mazuri katika mechi inazocheza nje ya jiji la Dar es Salaam ambapo msimu huu haijapoteza mechi hata moja kati ya sita ilizocheza.

Chanzo: mwanaspoti.co.tz