Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Njooni mhesabu

Mashabiki Yanga Vs Ruvu Mashabiki wa Yanga

Mon, 23 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga inarudi tena uwanjani leo kuvaana na Ruvu Shooting katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku mashabiki wa timu hiyo wakiwa na hamu kubwa ya kuona mashine mpya za timu hiyo akiwamo beki Mamadou Doumbia aliyetambulishwa juzi.

Mechi hiyo inapigwa kuanzia Saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, huku ikielewa Wananchi wana jambo lao dhidi ya maafande hao ambao katika mechi 21 walizokutana, wameshinda mara moja tu.

Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 53, zikiwa ni 39 zaidi na ilizonazo Ruvu iliyopo mkiani na pointi 14.

Kiu kubwa ya Yanga mbali na kutaka kuongeza pointi tatu ili ijiweke pazuri kutetea taji, lakini ni kutaka kuona kama straika Fiston Mayele anayeongoza kwa mabao ataendelea moto ili kutwaa tuzo kwa msimu huu baada ya msimu uliopita kuzidiwa na George Mpole aliyekuwa Geita Gold.

Mayele katika misimu miwili ya kucheza soka nchini hajawahi kuifunga Ruvu, hivyo kama leo atafunga atakuwa amekamilisha deni alilonalo kwa timu hiyo baada ya kuzitungua timu zote.

Ukija kwenye rekodi baina ya timu hizo zinawaweka katika nyakati ngumu zaidi Ruvu kwani katika mechi 21 tangu waanze kukutana wamewahi kushinda mara moja pekee ilikuwa Agosti 28,2019 wakishinda kwa bao 1-0 zaidi ya hapo walitoa sare mbili na kufungwa 19.

Yanga itashuka tofauti leo ikiwa na nafasi kubwa wakajaribu mfumo mpya kwa kucheza na washambuliaji wawili mbele Mayele na Kennedy Musonda aliyeanza kwa moto akifunga katika mchezo wa kirafiki juzi, Yanga ikishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Dar City.

Kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze kuelekea mchezo huo alisema licha ya kutambua ugumu mchezo wao dhidi ya Ruvu kitu bora kwao ni kupata siku 7 za maandalizi ya kikosi chao na kupumzika vizuri tayari kwa mechi hiyo ambayo ni kati ya mbili zinazopigwa leo ikiwamo ile ya Singida Big Stars na Azam itakayopigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Liti, mkoani Singida.

“Kitu cha kwanza tumekuwa na wiki nzuri tumepata siku saba za kupumzika, siku hizo zimetupatia muda wa kuongeza utimamu wa mwili kwa wachezaji sasa ninaweza kusema ilikuwa ni wiki nzuri ya pumzika na kurekebisha mambo mengi katika timu,”alisema Kaze.

“Mechi yetu na Ruvu haijawahi kuwa nyepesi kabisa, kama inakumbukwa kule Kigoma (msimu uliopita) tulisulu, pointi tatu za kesho (leo) ni muhimu sana katika kukusanya zile za kuelekea kwenye ubingwa.”

Katika ukatili mkubwa Yanga jana ilikuwa inapima utimamu wa mwili wa beki wao mpya Mamadou Doumbia kama ataweza kucheza mchezo huo baada ya raia huyo wa Mali aliyechomolewa kwenye Fainali za Mataifa Afrika (CHAN) kupata vibali vya kazi.

Kocha msaidizi wa Ruvu, Frank Msise ambaye kikosi chake katika mechi zao 10 zilizopita haijashinda kwani imetoa sare 4 na kupoteza 6, alisema wamefanya maandalizi ya kutosha kupigania pointi tatu mbele ya Yanga ambayo inaonekana kuwa bora ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

“Maandalizi yetu yamekamilika, tunajua tunakwenda kukutana na Yanga ambayo ina timu bora ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati, kutokana na ubora wao tumefanya maandalizi ya kutosha, tunajua haitakuwa mechi rahisi,” alisema Msise.

Chanzo: Mwanaspoti