BEKI wa kati wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ametaja washambuliaji watatu wanaomsumbua kwenye Ligi Kuu Bara (VPL) kila anapokutana nao.
Ninja aliwataja mastraika hao kuwa ni Meddie Kagere (Simba), Prince Dube (Azam) na Yusuph Mhilu (Kagera Sugar) waliopo juu kwenye msimamo wa wafungaji.
Dube ndiye kinara akiwa na mabao 13, Kagere yupo nafasi ya pili akiwa na mabao 11 akishikilia pia rekodi ya kuibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo.
Upande wa Mhilu hayupo nyuma kwani licha ya timu yake kusuasua ameifungia mabao manane mpaka sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ninja alisema inapotokea Yanga wanacheza na timu ambazo wachezaji hao watatu wapo hufanya mazoezi na maandalizi ya kutosha.
“Ninapokutana nao uwanjani kunakuwa na ushindani kati yao na muda mwingi huwa makini pindi wanapokuwa na mpira hata wasipokuwa nao,” alisema.
Mwanzoni mwa msimu Ninja hakuwa na wakati mzuri kwenye timu kwani alikuwa hapati nafasi kucheza mara kwa mara ingawa chini ya makocha, Juma Mwambusi na Nasreddine Nabi mambo yamekuwa tofauti kwake kwani anatumika kikosi cha kwanza.
Kwa upande wake, Mhilu alisema kuna mabeki wanaopambana na kila akikutana nao hufanya jambo la tofauti. “Kuna mabeki ambao nikikutana nao naona kweli kuna kazi ambayo natakiwa kuifanya,” alisema Mhilu.